10/05/2026
REV MATHEW J TSUUT
MUHIMU WA KUBATIZWA NA KUJAZWA ROHO MTAKATIFU
ANDIKO KUU
Mathayo 3:11-12, Matendo ya Mitume 1:8, Warumi 8:26-28
UTANGULIZI
Katika nyakati hizi watu wengi wanazungumzia mafanikio, miujiza, na baraka, lakini wameacha kuzungumzia habari za Roho Mtakatifu. Yesu mwenyewe aliacha agizo wazi kwamba waamini wanapaswa kubatizwa na kujazwa Roho Mtakatifu ili wawe na nguvu, ujasiri, na maisha ya ushindi.
Kubatizwa na Roho Mtakatifu si jambo la hiari kwa Mkristo; ni hitaji muhimu kwa maisha ya wokovu na huduma.
MAANA YA KUBATIZWA NA KUJAZWA ROHO MTAKATIFU
1.KUBATIZWA NA ROHO MTAKATIFU
Ni tukio la kwanza ambapo mwamini anapokea nguvu na uweza wa Roho Mtakatifu ndani yake.
Mathayo 3:11
“Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.”
Yesu ndiye mbatizaji wa kweli wa Roho Mtakatifu.
2.KUJAZWA ROHO MTAKATIFU
Ni hali ya kuendelea kujazwa uwepo, nguvu, na uongozi wa Mungu kila siku.
Waefeso 5:18
“... mjazwe Roho.”
Mkristo hawezi kutegemea uzoefu wa zamani pekee; anahitaji kujazwa kila mara.
UMUHIMU WA KUBATIZWA NA KUJAZWA ROHO MTAKATIFU
1.HUTUPA NGUVU NA UJASIRI
Matendo 1:8
“Mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu.”
Petro aliyemkana Yesu aliweza kusimama kwa ujasiri baada ya kujazwa Roho Mtakatifu.
Bila Roho Mtakatifu:
Tunaogopa,
Tunarudi nyuma,
Tunashindwa kusimama katika kweli
Lakini kwa Roho Mtakatifu:
Tunakuwa mashahidi,
Tunanena kwa ujasiri,
Tunashinda majaribu.
2.HUTUFUNDISHA KWELI YOTE
Yohana 16:13-14
“Atawaongoza awatie kwenye kweli yote.”
Roho Mtakatifu:
Hufungua akili kuelewa Neno,
Hututenga na uongo,
Hutuonyesha mapenzi ya Mungu.
Bila Roho Mtakatifu mtu anaweza kuwa kanisani lakini asiijue kweli.
3.HUTUSAIDIA KUOMBA
Warumi 8:26-27
“Roho naye hutusaidia udhaifu wetu...”
Wakati mwingine:
Hatujui tuombe nini,
Hatuna maneno,
Tunaelemewa na mizigo.
Lakini Roho Mtakatifu:
Hutuamsha kuomba,
Hutufundisha kuomba,
Hutuombea mbele za Mungu.
Bila Roho Mtakatifu maombi yanakuwa ya kawaida na yasiyo na nguvu.
4.HUTUSAIDIA KUMWABUDU MUNGU KATIKA ROHO
Yohana 4:24
“Mungu ni Roho...”
Ni ibada inayotoka moyoni kwa msaada wa Roho Mtakatifu.
Pasipo Roho Mtakatifu:
Ibada inakuwa mazoea,
Huduma inakuwa kazi,
Ukristo unakuwa mzigo.
HITIMISHO
Kanisa la leo linahitaji kurudi katika nguvu za Roho Mtakatifu.
WITO
Je, umebatizwa na Roho Mtakatifu?
Je, bado unajazwa kila siku?
Je, maisha yako yanaonyesha matunda ya Roho?
Leo Mungu yuko tayari kukujaza upya kwa Roho Mtakatifu.