21/02/2026
MASOMO YA MISA DOMINIKA YA 1 KWARESIMA MWAKA A, 22 FEBRUARI 2026
ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.91:15-16
Ataniita nami nitamwitikia; nitamwokoa na kumtukuza, kwa siku nyingi nitamshibisha.
KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi, utujalie tuzidi kulifahamu fumbo la Kristo, kwa njia ya mazoezi ya kipindi cha Kwaresima tunachojaliwa kila mwaka. Na kwa njia hiyo, tuyafuate yale yanayotokana na fumbo hilo, kwa mienendo inayostahili. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1:
Mwa.2:7-9,3:1-7
Bwana Mungu alimfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai. Bwana Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya. Bwana Mungu akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu: Msile matunda ya miti yote ya bustani? Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa k**a Mungu, mkijua mema na mabaya. Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala. Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.51:1-4,10-12,15
1. Ee Mungu, unirehemu,
Sawasawa na fadhili zako.
Kiasi cha wingi wa rehema zako,
Uyafute makosa yangu.
Unioshe kabisa na uovu wangu,
Unitakase dhambi zangu.
(K) Uturehemu, ee Bwana,
Kwa kuwa tumetenda dhambi.
2. Maana nimejua mimi makosa yangu,
Na dhambi yangu i mbele yangu daima.
Nimekutenda dhambi Wewe peke yako,
Na kufanya maovu mbele za macho yako. (K)
3. Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
Usinitenge na uso wako,
Wala roho wako mtakatifu usiniondolee. (K)
4. Unirudishie furaha ya wokovu wako;
Unitegemeze kwa roho ya wepesi.
Ee Bwana, uifumbue midomo yangu,
Na kinywa changu kitazinena sifa zako. (K)
SOMO 2:
Rum.5:12-19
K**a kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi. Maana kabla ya sheria dhambi ilikuwamo ulimwenguni, lakini dhambi haihesabiwi isipokuwapo sheria; walakini mauti ilitawala tangu Adamu mpaka Musa, nayo iliwatawala hata wao wasiofanya dhambi ifananayo na kosa la Adamu, aliye mfano wake yeye atakayekuja. Lakini karama ile haikuwa k**a lile kosa; kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi. Wala kadiri ya yule mtu mmoja aliyefanya dhambi si kadiri ya kile kipawa; kwa maana hukumu ilikuja kwa njia ya mtu mmoja ikaleta adhabu; bali karama ya neema ilikuja kwa ajili ya makosa mengi, ikaleta kuhesabiwa haki. Kwa maana ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo. Basi tena, k**a kwa kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu wote walihesabiwa haki yenye uzima. Kwa sababu k**a kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki.
SHANGILIO:
Mt.4:4
Mtu hataishi kwa mkate tu,
ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.
INJILI:
Mt.4:1-11
Baada ya kubatizwa, Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Ibilisi. Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa. Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate. Naye akajibu akasema, Imeandikwa: Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa: Atakuagizia malaika zake; na mikononi mwao watakuchukua; usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Yesu akamwambia, Tena imeandikwa: Usimjaribu Bwana Mungu wako. Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake, akamwambia, Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia. Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa: Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake. Kisha Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja malaika wakamtumikia.
Injili ya Bwana, Sifa kwako Ee Kristo
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Yesu alipangiwa na Mungu Baba kutuletea ukombozi. Shetani alimkaribia Yesu ili amshawishi kumwasi Baba yake na kuchagua njia ya ukombozi inayopingana na mpango wa Mungu.
1. Ee Bwana Yesu, ulishawishiwa kutumia nguvu ya kimungu kwa ubinafsi: Utufungue macho yetu ili tutambue kwamba hatuishi kwa mambo ya dunia tu, ila kwa baraka za Mungu Baba.
2. Ee Bwana Yesu, ulishawishiwa kuchagua njia ya siasa ili kutukomboa. Utufundishe kutambua kwamba Ufalme wa Mungu si ufalme wa kupigania mamlaka na madaraka, bali ni kutimiza amri zako.
3. Ee Bwana Yesu, ulishawishiwa kutegemea umungu wako ili kujionesha k**a mkubwa. Utusaidie tutambue kwamba imani yetu inatufundisha kuvumilia shida za duniani ili kustahili tuzo ya mbinguni.
4. Ee Bwana Yesu, ulimpinga mshawishi kwa imani imara kabisa: Utuimarishe kwa nguvu ya imani ili tuweze kushinda vishawishi tunavyokumbana navyo hasa tamaa ya madaraka na mali.
5. Ee Bwana Yesu, ulisema kwamba hakuna mtu atakayeshawishiwa kupita nguvu zake. Utusaidie tunapokuwa katika hatari za vishawishi na utuimarishe kwa nguvu yako tuvishinde.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba utufanye tustahili kukutolea inavyofaa vipaji hivi, vinavyotusaidia kuadhimisha mwanzo wa kipindi hiki kitakatifu cha Kwaresima. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
UTANGULIZI
Kujaribiwa kwa Bwana
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Yeye kwa siku arobaini alijinyima chakula cha kidunia, akaonesha hivyo namna ya kufanya kitubio. Yeye, kwa kupindua hila zote za nyoka wa kale, alitufundisha kushinda chachu ya uovu, ili kwa kuadhimisha fumbo la Pasaka kwa mioyo inayostahili, hatimaye tuifikie Pasaka ya milele.
Kwa hiyo, sisi pamoja na umati wa Malaika na Watakatifu, tunakuimbia utenzi wa sifa, tukisema bila Mwisho.
Mtakatifu, Mtakatifu,Mtakatifu, Bwana Mungu wa majeshi.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Mt.4:4
Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.
AU: Zab.91:4
Bwana atakufunika kwa manyoya yake, chini ya mbawa zake utapata kimbilio.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tumekula mkate wa mbinguni unaolisha imani, kuhamasisha tumaini na kuyatia nguvu mapendo. Tunakuomba, tujifunze kumtamani Yeye aliye mkate hai na wa kweli, na tuweze kuishi kwa kila neno litokalo kinywani mwako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
SALA YA KUWAOMBEA WAAMINI:
Ee Bwana, tunakuomba baraka yako iwashukie kwa wingi watu wako; ili, palipo na taabu, matumaini yaongezeke; palipo na kishawishi, nguvu ithibitishwe; na wajaliwe wokovu wa milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.