Joseph & Grace Mbofu-Injili Ministry.

Joseph & Grace Mbofu-Injili Ministry. Yesu yu karibu kurudi....Okoka

15/12/2022

VIJUE VYANZO VYA NDOTO NA KUVIOMBEA IPASAVYO.

CHANZO CHA KWANZA: NDOTO KUTOKA KWA MUNGU.

Ayu.33:14-15”Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali.Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu,
Katika usingizi kitandani;”
Hes.16”...Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, BWANA,… Nitasema naye katika ndoto.”
Zab.89:19”Ndipo ulipowaambia watakatifu wako kwa njozi(Ndoto),Ukasema...”

MAOMBI:Omba Mungu akusaidie kusikia k**a kile kitu kimetoka kwa Mungu. (Omba upate kusikia na kuelewa k**a kweli jambo hilo limetoka kwa Mungu).

CHANZO CHA PILI:SHETANI AU NDOTO KUTOKA KWA SHETANI.

Kumb.13:1-4”Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu,ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda BWANA, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote.Tembeeni kwa kumfuata BWANA, Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushik**ana naye.
MAOMBI:Jifunze kuombea lango la ndoto katika ulimwengu wa roho kwa kulifunika na damu ya Yesu ili Shetani asipitishe ndoto zake.

CHANZO CHATATU:NDOTO KUTOKA KWENYE MAZINGIRA YA SHUGHULI NYINGI.

Mhu.5:3”Kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi; na sauti ya mpumbavu kwa njia ya wingi wa maneno”

MAOMBI;Jifunze kumwomba Mungu akupangilie siku yako na aongoze siku yako.

CHANZO CHA NNE:NDOTO KUTOKA KWENYE HALI YA KIROHO YA MAHALI ULIPOLALA.

Mwa.28:10-12”Yakobo akatoka Beer-sheba, kwenda Harani.Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale.Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake.”

Yakobo aliota ndoto mahali alipolala palipokua na madhabahu(Betheli) Mungu aliyehai aliyoijenga babu yake mzee Ibrahimu.

Yakobo alilala mahali ambapo paliunganishwa na mbingu umewahi jiuliza umelala sehemu yenye umiliki au maagano na miungu mingine ya kishetani hali yako itakuwaje?

MAOMBI: Jifunze kuombea hali ya kiroho ya mahali unapolala kabla ya kulala hapo.

UHUSIANO WA ARDHI NA KUFANIKIWA AU KUKWAMA KWAKO KIMAISHA.Kipindi cha nne.Bwana Yesu Asifiwe.Lengo la somo hili ni kujif...
27/04/2021

UHUSIANO WA ARDHI NA KUFANIKIWA AU KUKWAMA KWAKO KIMAISHA.

Kipindi cha nne.

Bwana Yesu Asifiwe.

Lengo la somo hili ni kujifunza mbinu za kuombea ardhi ili itumike kutufanikisha kimaisha.

MFANO WA NNE

Yeremia 22:29-30
"Ee nchi, nchi, nchi, lisikie neno la Bwana. Bwana asema hivi, Andikeni habari za mtu huyu kwamba hana watoto, kwamba mtu huyu hatafanikiwa siku zake zote; maana hapana mtu katika wazao wake atakayefanikiwa, akiketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na kutawala tena katika Yuda."

Kibiblia nchi siyo mataifa k**a Tanzania, Kenya, Maekani, China, Sudan n.k.

Kibiblia nchi ardhi.

Katika hili andiko Mungu alizungumza na nchi aliposema;

1: "Ee nchi, nchi, nchi, lisikie neno la Bwana"-> hii ina maana nchi inasikia maneno.

Kwa hiyo mtu aweza kutamka maneno na ardhi ikasikia.

2: "Andikeni habari za mtu huyu..."->Hii ina maana ardhi inaweza kuandika na kutunza kumbukumbu ya ilichosemeshwa.

Kwa hiyo mtu aweza kutamka maneno na ardhi ikayaandika na kutunza kumbukumbu ya hayo maneno.

3: "...kwamba hana watoto, kwamba mtu huyu hatafanikiwa siku zake zote; maana hapana mtu katika wazao wake atakayefanikiwa..."->Hayo maneno yalitamkwa na kuelekezwa kwenye ardhi. Ardhi ikayaandika na kutunza kumbukumbu. Hiyo kumbukumbu inaweza kufuatiliwa kizazi hadi kizazi.


Wakati adhabu inatolewa kwa mtu huyu alikuwa bado hana watoto, lakini kumbukumbu iliandikwa kwenye ardhi kuwa hata watoto wake wakija nao wasifanikiwe.

Fikiria wewe ni mtoto na umeingia kwenye adhabu ya baba au mama na unatafuta kufanikiwa na haufaninikiwi sio kwamba akili huna bali unazo lakini umezuiliwa kufanikiwa na ardhi kwa sababu ya kosa la baba yako na mama yako je unaombaje?

Usikose kipindi cha tano.

01/04/2021

UNYAKUO WA KANISA UTAKAVYOKUWA.

Kipindi cha pili.

Bwana Yesu Asifiwe.

ITAKAVYOKUWA SIKU YA UNYAKUO WA KANISA.

Siku ya kunyakuliwa kwa watu waliookoka sehemu nyingine duniani itakuwa usiku, sehemu nyingine itakuwa mchana, maana majira duniani yanatofautiana.Jua hutua sehemu moja duniani na huchomoza sehemu nyingine ya dunia.

Wakati wa kunyakuliwa kwa watu waliookoka hapa Tanzania, hatufahamu itakuwa mchana au usiku, maana siku ile inakuja k**a mwizi au k**a uchungu umjiavyo mwenye mimba (1 Wathesolanike 5:1-3).

Unyakuo utakuwa ni kwa dakika moja kufumba na kufumbua. Ndani ya hiyo dakika wafu waliookoka watafufuliwa na watu tuliookoka ambao tutakuwa hai duniani tutaungana pamoja nao, na wote kwa pamoja watabadilishwa miili yetu hii na kuvaa miili ya utukufu yaani miili isiyoharibika.

Hii ni k**a ilivyoandikwa katika 1 Wakorintho 15:52-53 Bibilia inasema,” Kwa DAKIKA MOJA, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda Italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika. Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa.”

Hapa naomba unielewe; kutakuwa na makundi manne ya watu.
1: Wafu waliookoka,
2:Wafu wasiookoka,
3:Walio hai waliookoka na
4:Walio hai wasiookoka.

Watanyakuliwa 1 na 3. Wataachwa 2 na 4

Luka 17:34-36
[34]Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa katika kitanda kimoja; MMOJA ATATWALIWA, mmoja ataachwa.
[35]Wanawake wawili watakuwa wakisaga pamoja; MMOJA ATATWALIWA, mmoja ataachwa. [
[36]Watu wawili watakuwa shambani, mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.]

Unaona hapo kuna kutwaaliwa(Kunyakuliwa na kuachwa!!!!

Kundi 1 na 3 hapo juu watatwaliwa na kwenda angani kwenye harusi ya mwana kondoo ambayo, itafanyika kwa muda wa miaka saba.
Kundi 4 hapo juu watakaoachwa duniani, watakuwa katika mateso ya dhiki kuu muda wa miaka saba.

Kundi 2 hapo juu wataendelea kubaki kwenye mateso ya jehanamu ya moto(Mahabusu/Selo) mpaka wakati wa ufufuo wa pili wa aibu ili watupwe ziwa la moto(Gerezani)

Tukutane kipindi cha tatu.

20/07/2020

DAMU YA YESU INAVYOONDOA UGOMVI/KUTOKUPATANA KATI YA MTU NA MTU.

Bwana Yesu Asifiwe.

Karibu sana tupate maarifa ya Neno la Mungu.

Tusome Waefeso 2:12-17
“Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali(HAMPATANI/NI MAADUI) hapo kwanza mmekuwa karibu kwa DAMU YAKE KRISTO. Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati KILICHOTUTENGA. Naye akiisha kuuondoa ule UADUI KWA MWILI WAKE; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa MTU MPYA MMOJA(WAPATANE) ndani ya nafsi yake; akafanya AMANI. AKAWAPATANISHA WOTE WAWILI na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya MSALABA, AKIISHA KUUFISHA ULE UADUI KWA HUO MSALABA”.

Katika hilo fungu tunaona jinsi ambavyo kuna UWEZO KATIKA DAMU YA YESU KRISTO kuwapatanisha watu wawili ambao hawaelewani/waliogombana.

Wewe uliyeokoka una uhalali wa kuitumia Damu ya Yesu na ikaondoa uadui kati yako na mtu mwingine anayekuchukia au kati ya watu wawili wanaogombana au wanaochukiana.

Hii ni kwa sababu ndani yako Mungu ameweka huduma ya upatanisho kwa njia ya kutamka tu neno la upatanisho ukitumia Damu ya Yesu.

“Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya. Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha nafsi yake kwa Kristo, naye ALITUPA HUDUMA YA UPATANISHO; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu NENO LA UPATANISHO! Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba MUNGU ANASIHI KWA VINYWA VYETU; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu” (2Wakorintho 5:17-20).

Kila mtu aliye ndani ya Kristo (aliyeokoka), Mungu mwenye uwezo wa kupatanisha anakaa ndani yake, naye amempa HUDUMA YA UPATANISHO na NENO LA UPATANISHO.

Ndiyo maana kila aliyeokoka anajukumu la kuwaongoza wengine sala ya toba ili wapatane na Mungu(waokoke) kwa njia ya Damu ya Yesu.

Upatanisho kati ya mtu na mtu kwa njia ya Damu ya Yesu hufanyika kwa kutamka maneno tu.
Marko 11:22-23“Yesu akajibu, akamwambia, Mwamini Mungu. Amin, nawaambia, Yeyote ATAKAYEUAMBIA mlima huu ng’oka ukatupwe baharini, wala ASIONE SHAKA MOYONI MWAKE ila aamini kwamba hayo ASEMAYO yametukia, yatakuwa yake.”

Mlima unawakilisha tatizo lolote mfano ugonjwa, umaskini, laana, ugomvi, vifungo n.k

UNATAKIWA KUSEMA KILE UNACHOKIAMINI WALA USIONE SHAKA MOYONI MWAKO, BALI UAMINI KWAMBA KILE UKISEMACHO KIMETUKIA NACHO KITAKUWA CHAKO!!👏👏👏

Uamini kitu gani?

Kwa mujibu wa somo hili amini kuwa kuna uwezo katika Damu ya Yesu Kristo kupatanisha watu wawili wasiopatana au waliogombana.

Kwa hiyo k**a unaona kuna uzito fulani kati yako na mtu mwingine na hata kusababisha kutoelewana au tayari hamuelewani na wewe umeokoka; sema maneno haya;

“ Katika jina la Yesu Kristo nanyunyiza damu ya Yesu Kristo juu ya Uadui na Kiambaza kinachotufanya tusielewane mimi na – (nataja jina la mtu huyo). Uadui na ugomvi uondoke kwa damu ya Yesu Kristo, tupatane na tuwe na Amani na maelewano – Amina”.

Halafu baada ya kusema hivyo, amini kuwa hayo uliyoyasema yametukia, nayo yamekuwa yako – yaani uadui haupo tena, bali mmepatanishwa na Damu ya Yesu Kristo.

Damu ya Yesu Kristo ibarikiwe! Jina la Yesu Kristo libarikiwe! Usikate tamaa unapokosa maelewano na mtu, kuna uwezo katika Damu ya Yesu Kristo wa kukupatanisha naye.

Utakapoiachilia damu ya Yesu utashanga ghafla uadui unaondoka na amani na maelewano yanakuwepo.

Glory to God.

08/06/2020

IMANI POTOFU ZA KUJITENGA NAZO MAPEMA SANA.

Kipindi cha kwanza:VIGEZO SABA VYA KUTATHIMINI IMANI YAKO.

“Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri k**a ungekuwa baridi au moto.Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu”(Ufunuo 3:15-16)

Kumekuwako na mlipuko wa madhehebu mengi ya kiimani katika Urkisto hata hivyo mengi ya madhehebu haya ni madhehebu ya Uongo.

Biblia iko wazi hapo kwamba michanganyo ya kweli na uongo husababisha mtu kuwa vuguvugu kiimani hivyo Yesu akija kulinyakua kanisa mtu/ watu k**a hao hawatanyakuliwa!!

Tutawezaje kujua kuwa imani fulani ni ya kweli au ni ya uongo?

Baadhi ya vigezo vya kuvitumia:

1. Yeyote anayepingana na Utatu
Isaya 48; 16, Mathayo 3; 17,28;19,1Timotheo 2;5

2. Yeyote anayepinga uungu wa Yesu Kristo
Yohana 1;1, 14, Isaya 7;14 Warumi 1;4

3. Yeyote anayepinga uungu wa Roho Mtakatifu.
Yohana 15;26, 16;8,13,14;17,Matendo 2;1-4

4. Yeyote anayekataa kuwa Dhambi ni hali halisi ya mwanadamu
Warumi 3; 10, 23. 14;23; 1Yohana 3;4,5;17

5. Yeyote anayekataa ukombozi kupitia Damu ya Yesu
Efeso 1;7, Wakolosai 1;20, Waebrania 10;12.

6. Yeyote anayekataa wokovu kuwa ni zawadi ya Neema ya Mungu
Efeso 2;8, Yohana 1;12,3;36

7. Yeyote anayekataa kuwa kuna hukumu baada ya kufa
Warumi 6; 23, Waebrania 9; 27,2Thesalonike 1;7,8

Barikiwa .

Usikose kipindi cha pili.

16/05/2020

JENGA IMANI KWA MISINGI YA AGANO JIPYA.

Sehemu ya Tatu: AGANO JIPYA NI BORA ZAIDI YA AGANO LA KALE.

Bwana Yesu Asifiwe.

Duniani kuna watetezi wa agano la kale ambao husema kwamba ujumbe wa agano la kale uko na uzito sawasawa na ujumbe wa agano jipya kwa kuwa yote ni maandiko matakatifu kwa wote.

Lakini kwa mujibu wa maandiko; ubora wa agano la kale umepitwa na ubora wa agano jipya.

Ukisoma Ebr.8:6 utagundua kwamba kazi ya ukombozi wa Yesu Kristo imekubalika mbele za Mungu kuwa “huduma iliyo bora! na hivyo kumfanya Yesu kuwa “mdhamini wa agano lililo bora”, tena lenye “ahadi zilizo bora” (Ebr.7:22).
Kwa hiyo agano jipya ni bora,lina huduma bora na ahadi bora!!!! Oh hallelujah!!! (Sina maana kwamba agano la kale tulichane...HAPANA, Tunapaswa kulisoma ila tujenge imani kiagano jipya, agano bora zaidi ya agano la kale).

Hii ni kwa sababu agano la kale ni dhaifu na lenye upungufu: “Maana k**a lile la kwanza lingalikuwa halina upungufu, nafasi isingalitafutwa kwa lile la pili….” (Ebr.8:7)

Na mwisho kabisa maandiko yameweka bayana kuwepo kwa agano jipya kumelifanya agano la kale kuwa chakavu: “Kwa kule kusema agano Jipya, amelifanya lile la kwanza kuwa kuukuu. Lakini kitu kiaanzacho kuwa kikuukuu na kuchakaa ki karibu na kutoweka.” (Ebr.8:13)

"JIKITE KWENYE AGANO BORA YAANI AGANO JIPYA."

Ubarikiwe sana.

10/05/2020

UNYAKUO WA KANISA NA DHIKI KUU IJAYO.

Sehemu ya kwanza.

Bwana Yesu Asifiwe.

‘Kunyakuliwa’ ni tendo la kuchukuliwa kwa kitu ghafla, kwa kasi kubwa na kuondolewa pale kilipokuwa; katika hali ya kuwaacha watu wamepigwa butwaa, kwa jinsi wasivyoweza kukipata kitu hicho tena.

Kutokana na dalili ya mwisho kabisa ya mwisho wa dunia kutimia(Math.24:14) tukio la kunyakuliwa kwa kanisa(watu waliookoka) liko karibu sana kuanzia sasa.

Yesu anakuja kufanya kazi hii, haraka na wala hatokawia (Waebrania 10:37).

1 Wathesolanike 4:15-17 Biblia inasema, “Kwa kuwa twawambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakao salia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti. Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya Malaika mkuu, na parapanda ya Mungu nao walio kufa katika Kristo, watafufuliwa kwanza kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki bwana hewani na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele.”

Kwa hiyo, watu waliookoka muda si mrefu ujao, watanyakuliwa kwa jinsi hii na Bwana Yesu Kristo.
Siku ya kunyakuliwa kwa watu waliookoka sehemu nyingine duniani itakuwa usiku, sehemu nyingine itakuwa mchana, maana majira duniani yanatofautiana. Jua likitua sehemu moja duniani, linachomoza sehemu nyingine ya dunia. Wakati wa kunyakuliwa kwa watu waliookoka hapa Tanzania, hatufahamu itakuwa mchana au usiku, maana siku ile inakuja k**a mwizi au k**a uchungu umjiavyo mwenye mimba (1 Wathesolanike 5:1-3). Ikiwa ni mchana watu wote waliokufa tangu zamani wakiwa katika hali ya utakatifu na wakawa wamekwenda mbinguni, watafufuliwa na kutokea tena duniani, na kila mmoja atawaona.

Watakuwepo watu wengi kwa ghafla, mitaani kila mahali. Hata k**a kwenye makaburi ya zamani ambapo siku hizi kuna jengo la ofisi, watatokea humo humo ofisini na kuujaza uso wa dunia. Dakika moja kufumba na kufumbua, watu waliookoka ambao wako hai duniani nao wataungana pamoja nao, na wote kwa pamoja watabadilishwa miili yao na kuvaa miili ya utukufu yaani miili isiyoharibika. Kadhalika katika kitabu cha 1 Wakorintho 15:52-53 Bibilia inasema,” Kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda Italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika. Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa.”

Katika wale watakaokuwako duniani, baada tu ya parapanda kulia, wale waliookoka watatwaliwa na kwenda angani kwenye harusi ya mwana kondoo ambayo, itafanyika kwa muda wa miaka saba, na wale watakaoachwa duniani, watakuwa katika mateso ya dhiki kuu muda wa miaka saba. Kadhalika na watakatifu waliofufuliwa, watakwenda angani kwenye harusi ya mwanakondoo, wakati wale waliokufa katika hali ya dhambi wataendelea kubaki kwenye mateso ya Jehanamu ya moto mpaka wakati wa ufufuo wa pili.

RIPOTI YA KUTOWEKA KWA WATU DUNIANI.

Tukio la unyakuo, litawachanganya akili watu wote duniani yaani wale watakaobaki. Watakuwepo wawili wakilima shambani, mmoja aliyeokoka atanyakuliwa, naye yule ambaye hajaokoka ataachwa, na hakika atashtushwa sana kwa kitendo cha ghafla cha kutoweka kwa mwenzake. Pia watakuwepo wawili wakitwanga nafaka, na ghafla mmoja aliyeookoka atanyakuliwa na wa pili ambaye hajaokoka ataachwa. Tunasoma katika Mathayo 24:40-41 Biblia inasema “Wakati ule watu wawili watakuwa kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa; wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa; mmoja aachwa.”

Ikiwa tukio hili litakuwa usiku na katika familia fulani kuna mume hajaokoka na mke ameokoka, watoto wakubwa hawajaokoka na kadhalika katika familia hiyo wako watoto wadogo wasiojua mema na mabaya; mume huyo mlevi amayempiga vita mkewe kwa sababu ya wokovu, ataamka asubuhi na kushangaa kuona mkewe kitandani na watoto wadogo wasiojua mema na mabaya hawapo. Atawauliza watoto wakubwa, “Mama yenu yuko wapi?” watajibu “Hatujui”, atatoka nje na kwenda kuuliza. Wakati kuohuo kila mahali itaripotiwa Polisi, kwamba wako watu waliotoweka usiku, pamoja na watoto wote wadogo wasiojua mema na mabaya. Pia kutakuwepo na Polisi waliotwaliwa. Baada ya uchunguzi duniani kote, waandishi wa habari ambao walioachwa watatoa ripoti katika magazeti k**a ifuatavyo, “Mamilioni ya watu kote duniani wameripotiwa kutoweka usiku wa jana. Uchunguzi umeonyesha kwamba waliotoweka ni walokole ambao wamekuwa wakidhaniwa kuwa wamechanganyikiwa au kupotea. Taarifa zaidi zinaeleza kwamba watoto wachanga wote pia wametoweka. Taarifa za uchunguzi zinaonyesha kwamba waliotoweka wamenyakuliwa kwenda kumlaki Yesu mawinguni k**a walokole walivyokuwa wakihubiri!”

Usikose Sehemu ya Pili.

Barikiwa sana.

13/01/2020

NAMNA YA KUTUMIA DAMU YA YESU KATIKA MAOMBI.

SEHEMU YA TATU:NAMNA DAMU YA YESUINAVYOTAMKWA KWENYE MAOMBI.

Bwana Yesu Asifiwe

Katika sehemu ya pili tulijifunza uhusiano wa jina la Yesu na Damu ya Yesu kwamba nguvu ya jina la Yesu imo ndani ya Damu ya Yesu.Hivyo ni budi kutanguliza damu ya Yesu wakati unapoomba kisha jina la Yesu lifuate!!!Soma kwa kutafakari Wafilipi 2:5-11 utagundua hii siri ya ajabu sana na utafanikiwa sana kwenye maombi yako.

Katika hii sehemu ya tatu tutajifunza namna ya kuitumia damu ya Yesu katika maombi.
Utatumia maneno gani kuitamka damu ya Yesu wakati unaomba?

Damu ya Yesu inatumika kwenye maombi k**a ilivyotajwa ndani ya Biblia.
Ukisoma Biblia utakutana na mistari mingi sana inayosema juu ya matumizi ya damu katika agano la kale.
Kwa mfano hebu tusome Ebra.9:18 Kwa hiyo hata lile la kwanza halikuanzwa pasipo damu.19 Maana kila amri ilipokwisha kunenwa na Musa kwa hao watu wote, k**a ilivyoamuru sheria, aliitwaa damu ya ndama na ya mbuzi, pamoja na maji na sufu nyekundu na hisopo, akakinyunyizia kitabu chenyewe, na watu wote,20 akisema, Hii ni damu ya agano mliloamriwa na Mungu.21 Na ile hema nayo na vyombo vyote vya ibada alivinyunyizia damu vivyo hivyo.22 Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo.”

Katika mstari wa 18 inasema agano la kwanza halikuanzwa bila damu ikimaanisha hata agano la pili lazima lianze na damu ya Yesu. Hii inatutaka tujue katika ulimwengu wa roho mambo hayaanzi hivi hivi bila damu!!!!Ndiyo maana ukienda kwa mganga wa kienyeji hawezi akakuomba ukalete samaki au mchicha bali atakuagiza ukalete kuku,njiwa,kondoo n.k ili achinje hao wanyama spate damu ya kutoa kwa mashetani yake ili yatoe msaada wao wa kishetani.Kwa hiyo bila kuanza na damu katika ulimwengu wa roho ni vigumu sana kupata msaada. Kwa hiyo k**a mambo katika ulimwengu wa roho huanza na damu hata sisi yatupasa kuanza mambo yetu yote kwa kuitumia damu ya agano ya Yesu.Anza kusoma kwa damu ya Yesu,anza kazi kwa damu ya Yesu,anza biashara yako kwa damu ya Yesu, anza kilimo kwa damu ya Yesu,anza ndoa kwa damu ya Yesu n.k.

Katika mstari wa 19 Biblia inatuambia kuwa Musa aliitwaa damu ya ndama na ya mbuzi akakinyunyizia kitabu na watu wote.Katika agano la kale ilikuwa ni ruksa mbele za Mungu kutuumia damu za wanyama.Katika agano jipya haturuhusiwi na Mungu kutumia damu za wanyama bali tunatakiwa kutumia damu ya Yesu tu.
Sasa sikia Musa alipoitwaa ile damu ya wanyama aliNYUNYIZA kitabu na watu.Tunapata ufahamu kwamba tunaweza kuitumia damu ya Yesu katika maombi kwa KUNYUNYIZA!!!!.

Usishangae mtu wa Mungu hivyo ndivyo damu ya Yesu inavyotumiwa kimaombi,hebu tusome hapa Ebra.12:24 na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.”
Unaona hapo inavyotumika damu ya Yesu..."kwa kunyunyizwa".
Biblia inasema hiyo damu ya Yesu ikinyunyizwa mahali inaanza kusema mambo mazuri juu ya aliyeinyunyiza mahali.
Inawezekana kabisa mtu amekuendea kwa waganga na kukunenea maneno ya laana,ukitumia damu ya Yesu kwa kunyunyiza mahali kwa imani kabisa;damu ya Yesu itaanza kukutetea katika ulimwengu wa roho kwa kusema mema juu yako.Chukua hatua ya kiimani sasa kuanza kuinyunyiza damu ya Yesu kwenye mambo yako.
Unainyunyizaje?-Unainyunyiza damu ya Yesu kwa kutamka maneno tu!!!Mfano: Sema “nanyunyiza damu ya Yesu ya agano katika…..(taja eneo unalotaka damu ya Yesu ifanye kazi)”.Hivyo ndivyo na Musa alivyofanya(Ebra.9:18-21)

Turudi tena hapo juu kwenye Waebrania 9;ukisoma mstari wa 22 Biblia inatuambia hivi “… katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo.”
Ili kusafisha mambo ya kiroho kwa kuondoa mabaya yote rohoni walitumia damu ya wanyama kwa kuiMWAGA kumbe damu hutumika kwa kumwaga mahali.
Nasi tunaweza kutumia damu ya Yesu kwa kuimwaga mahali sawa na ilivyoandikwa Marko 14:24”Akawaambia, Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi.”
K**a damu ya Yesu ilimwagika kwa ajili yetu inamaanisha tunaweza hata sasa kuimwaga mahali kwa ajili ya kuondoa mabaya yote katika ulimwengu wa roho.
Kumbuka:Damu ya Yesu ipo katika madhabahu ya Mungu katika ulimwengu wa roho;tunaenda pale kwa imani,tunaichukua kwa imani na tunaitumia kwa imani.
Kuna mambo hayaendi maishani mwako?Biblia imesema bila kumwaga damu hayataondoka,achilia damu ya Yesu kwa kutamka tu kwa imani huku ukitaja hayo mambo unayotaka yaondoke maishani mwako.
Namna nyingine ya kuitumia damu ya Yesu ni kwa kuinywa.
1 Wakoritho 11:25 Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.
Tunaposhiriki meza ya Bwana huwa tunatumia viwakilishi vya damu ya Yesu k**a divai,juice,n.k.
Hii ni njia ya kumkumbuka Yesu Bwana na Mwokozi wetu.
Mtu akishiriki meza ya Bwana kwa imani(siyo kidini au kimazoea) lazima Mungu atakutana tu na mahitaji ya huyo mtu na kumvusha kwenda hatua bora zaidi.
Usishiriki meza ya Bwana kimazoea utapata hasara-1Kor.11:27 Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana.28 Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe.29 Maana alaye na kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua ule mwili.”
HITIMISHO:KUNA NAMNA TATU(3)ZA KUITUMIA DAMU YA YESU:
1.KUINYUNYIZA
2:KUIMWAGA
3:KUINYWA
Anza kutumia damu ya Yesu sasa ili ufaidike na ilichobeba kwa ajili yako.
K**a hutaitumia damu ya Yesu;Mungu nae hataitumia kukusaidia!!!
Tunajifunz hilo hapa Kutoka 12:22 Nanyi twaeni tawi la hisopu, mkalichovye katika ile damu iliyo bakulini na kukipiga kizingiti cha juu, na miimo miwili ya mlango, kwa hiyo damu iliyo katika bakuli; tena mtu ye yote miongoni mwenu asitoke mlangoni mwa nyumba yake hata asubuhi.23 Kwa kuwa BWANA atapita ili awapige hao Wamisri; na hapo atakapoiona hiyo damu katika kizingiti cha juu, na katika ile miimo miwili, BWANA atapita juu ya mlango, wala hatamwacha mwenye kuharibu aingie nyumbani mwenu kuwapiga ninyi.”
Mungu alikusudia kuwasaidia wana wa Israeli awatoe utumwani Misri. Ili kutoa huo msaada;Mungu alitaka damu ya mwanakondoo ipakwe kwenye vizingiti vya milango na kwenye miimo ya milango yao. Wana wa Israeli walichinja mwanakondoo na kuweka damu kwenye mabakuli kisha walipaka kwenye hiyo miimo na hivyo vizingiti vya milango yao.
Point ni hii:Damu iliyowasaidia wana wa Israeli ni ile walitoitumia kupaka kwenye miimo na vizingiti vya milango yao. Hiyo ndiyo damu aliyoitumia Mungu kuwasaidia. Damu iliyobaki kwa mwanakondoo haikuwasaidia.
Damu iliyobaki kwenye mabakuli haikuwasaidia.
Kumbe damu ya Yesu iliyoandikwa kwenye biblia haitusaidii bali tunasaidiwa na damu ya Yesu tunayoitumia tu!!!

SEHEMU YA NNE:FAIDA ZA DAMU YA YESU ILIYOTUMIWA.

Shalom.

07/01/2020

Yesu akupenda

18/11/2019

KWANINI YESU ALIKUFA MSALABANI?

SEHEMU YA KWANZA

SABABU YA KWANZA:YESU ALIKUFA MSALABANI ILI KUTUONESHA UHAKIKA KUWA TUKIFA NDANI YAKE(TUKIWA TUMEOKOKA)ATATUFUFUA SIKU YA MWISHO.

“Kwa maana ikiwa tumeungana naye katika mauti Yake, bila shaka tutaungana naye katika ufufuo Wake” (Warumi 6:5)

“Nanyi ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu anakaa ndani yenu, Yeye aliyemfufua Kristo Yesu kutoka kwa wafu ataihuisha pia miili yenu ambayo hufa kwa njia ya Roho Wake akaaye ndani yenu.” (Warumi 8:11)

“Hili ni neno la kuaminiwa: Kwa maana k**a tumekufa pamoja naye, tutaoishi pamoja naye.” (2 Timotheo 2:11) Bwana Yesu alifanya miujiza mingi wakati alipokuwa hapa ulimwenguni. Alimfufua mtoto msichana wa miaka 12 na wanaume wawili ambao walikuwa wamekufa (Marko 5:41-42; Luka 7:14-15; Yohana 11:43-44).

Lakini wale watu ambao aliwafufua hawakuishi milele katika miili hiyo kwani walikufa tena. Wakati Bwana Yesu Kristo alipofufuka kutoka kwa wafu, alishinda nguvu za kifo ili watu wote ambao wamepewa miili ya ufufuo wasije wakakufa tena.

Wakati Mungu alipomfufua Bwana Yesu Kristo kutoka kwa wafu, Mungu alikuwa anasema kwamba Bwana Yesu Kristo alifaulu katika kutulipia fidia ya dhambi zetu. Sadaka ambayo alitoa msalabani ilikubalika na Mungu. Hii ndiyo sababu Biblia inasema, “Alijinyenyekeza hata mauti, naam, mauti ya msalaba! Kwa hiyo, Mungu alimtukuza sana na kumpa Jina lililo kuu kuliko kila jina.” (Wafilipi 2:8-9). Wakati Kristo alipokuwa msalabani alilia kwa sauti akisema, “imekwisha” (Yohana 19:30). Wakati Mungu alipomfufua Kristo kutoka kwa wafu, Mungu alikuwa akisema, “Kweli imekwisha!” Kristo alikuwa amefidia dhambi zetu msalabani na alituondoa katika nguvu za dhambi.

Siku tatu baada ya kifo chake, Kristo alishinda kifo. Kwa sababu alifufuka, kifo hakina nguvu tena za kuwaangamiza miili ya ufufuo wa watu wote. Hii ndiyo sababu Kristo anasema, “Mimi ni Alpha na Omega”, asema Bwana Mungu, “Aliyeko, aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi” (Ufunuo 1:8).

Biblia ni wazi kwamba wale wote ambao wameokoka watafufuliwa kutoka kwa wafu naye Kristo na watakaa naye milele. “Kwa maana ikiwa tumeungana naye katika mauti Yake, bila shaka tutaungana naye katika ufufuo Wake.” (Warumi 6:5). “Kwa kuwa tumeamini kwamba Yesu alikufa na kufufuka, hata hivyo, Mungu kwa njia ya Yesu atawafufua pamoja naye wale waliolala mautini.” (1 Wathesalonike 4:14). “Naye Mungu aliyemfufua Bwana kutoka kwa wafu atatufufua sisi pia kwa uweza Wake.” (1 Wakorintho 6:14).

Biblia inatufundisha jinsi Bwana Yesu alivyoshinda nguvu za kifo. Biblia inasema, “Uchungu wa mauti ni dhambi na nguvu ya dhambi ni sheria.” (1 Wakorintho 15:56). Hii inamaanisha kwamba sisi sote tumetenda dhambi na tutahukumiwa milele. Biblia inaendelea kusema, “Lakini ashukuriwe Mungu, Yeye atupaye ushindi kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.” (1 Wakorintho 15:57). Kwa ufupi hitaji la torati lililipwa kwa maisha na kifo cha Bwana Yesu Kristo. Wakati dhambi zetu zinasamehewa, torati haiwezi kutuhukumu kwani haina nguvu ya kutugusa, hatuwezi kuhukumiwa milele. Badala yake, “Ghafla, kufumba na kufumbua, parapanda ya mwisho itakapolia. Kwa kuwa parapanda italia, nao wafu watafufuliwa na miili isiyoharibika, nasi tutabadilishwa. Kwa hiyo, mwili huu wa kuharibika utakapovaa kutoharibika, nao huu mwili wa kufa utakapovaa kutokufa, ndipo lile neno lililoandikwa litakapotimia: ‘ Mauti imemezwa kwa kushinda’ ” (1 Wakorintho 15:52;54). Hii ndiyo sababu Yesu anakuita uje kwake. “Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi” (Yohana 11:25).

Shalom,

USIKOSE SEHEMU YA PILI

24/08/2019

✅"...msizuie kunena kwa lugha..."(1 Wakoritho 14:39)
✅"Nami nataka ninyi nyote mnene kwa lugha,.."(1 Wakoritho 14:5)
✅"Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake;..."(1 Wakoritho 14:4)

Address

Mwanza

Telephone

+255757045076

Website

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when Joseph & Grace Mbofu-Injili Ministry. posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Contact The Place Of Worship

Send a message to Joseph & Grace Mbofu-Injili Ministry.:

Share