28/08/2026
UCB yazindua mikopo kwa mama Lishe na baba Lishe Kilimanjaro
Moshi
Benki ya Uchumi Commercial Bank (UCB) imezindua mikopo ya fedha na nishati safi kwa Mama Lishe na Baba Lishe, mpango unaolenga kuwawezesha wajasiriamali hao kukuza shughuli zao za kiuchumi na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara.
Uzinduzi wa mpango huo, unaojulikana k**a UMALITA, umefanyika katika Soko la Manyema mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na changamoto ya mitaji na matumizi ya nishati safi miongoni mwa wafanyabiashara hao.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Uchumi Commercial Bank Limited (UCB), Cornel Alois, amewataka Mama Lishe na Baba Lishe kujiunga katika vikundi ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo hiyo.
Amesema mikopo hiyo inaweza kutolewa bila wafanyabiashara kuhitajika kuwa na dhamana ya mali, hatua inayolenga kuwawezesha wajasiriamali ambao mara nyingi hukabiliwa na changamoto ya kukosa dhamana wanapohitaji mikopo kutoka taasisi za fedha.
Mikopo hiyo inajumuisha mkopo wa fedha kwa ajili ya kuendeleza na kukuza biashara, pamoja na mkopo wa mitungi ya gesi kwa wafanyabiashara wanaotaka kutumia nishati safi katika shughuli zao za upishi.
Kwa upande wake, Afisa Tarafa wa Moshi Mashariki, Halima Idrisa, akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi, ameipongeza UCB kwa kuiunga mkono serikali katika kuwawezesha wajasiriamali hao na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Naye Mama Lishe, Asha Olotu, ameishukuru Serikali na UCB kwa kuliona na kulikumbuka kundi hilo, akisema mikopo hiyo itawapa fursa ya kukuza biashara na kujikwamua kiuchumi.
Uzinduzi huo unatarajiwa kuwa chachu kwa Mama Lishe na Baba Lishe kuongeza uzalishaji, kuboresha biashara zao na hatimaye kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa jamii na taifa kwa ujumla.