10/02/2023
ALHAMISI: 09-02-2023
SOMO:MAMBO 10 YA KUFANYA KILA SIKU NA KILA WAKATI, ILI KUFANYA SIKU YAKO IWE YA BARAKA
MHUBIRI: MCHUNGAJI KATANA MWANGOME M'BAYA.
KANISA: HEKALU LA NEEMA- BIGWA- MOROGORO
Katika maisha kuna vitu unatakiwa uvifanye kila siku, mara kwa mara, ni mambo ya ki-Mungu, Usipoyafanya utakosa amani kwenye maisha yako.
1) Kusifu na kuabudu.
Sio kuimba tu bali unamueleza Mungu sifa zake, uweza wake, nguvu zake,unampa Mungu dhabihu ya sifa kwa maneno ya kinywa chako.
Waebrania 13:15
Basi, kwa njia yake yeye, na tumpe Mungu dhabihu ya sifa daima, yaani, tunda la midomo iliungamayo jina lake.
Unapoamka asubuhi unamsifu Mungu, itakufanya uwe na amani. Mungu anakaa katika sifa zake.
2) Kuhubiri na kutangaza habari njema.
1 Mambo ya Nyakati 16:23-27
Mwimbieni BWANA, nchi yote;
Tangazeni wokovu wake siku kwa siku.
Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
Na watu wote habari za maajabu yake.
Kwa kuwa BWANA ni mkuu mwenye kusifiwa sana;
Na wa kuhofiwa kuliko miungu yote.
Maana miungu yote ya watu si kitu;
Lakini BWANA ndiye aliyezifanya mbingu.
Heshima na adhama ziko mbele zake;
Nguvu na furaha zipo mahali pake.
Waambie watu habari za utukufu wake, watu unaokaa nao, unaoishi nao, kazini kwako. Waambie wajue ukuu wake Mungu wako unaemwamini, alipokutoa na jinsi alivyokupigania.
3) Kukusanyika katika ibada ( Fellowship).
Matendo ya Mitume 2:46
Na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe,
Usiache kuwa na ushirika na Mungu nenda ibada kwa moyo mmoja kwa kupenda bila kusukumwa na mtu.
4) Kusoma na kutafakari neno la Mungu.
Zaburi 1:2
Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.
Usiache siku ikapita bila hujasoma neno la Mungu ,unaposoma neno kuna vitu utagundua kwenye maisha yako hukutakiwa kuwa navyo.
Kwa kusoma neno utakumbuka ahadi za Mungu Katika neno la Mungu kuna ahadi ulitakiwa uwe nazo unaposoma utakumbushwa ni kipi ulitakiwa uwe nacho.
1 Mambo ya Nyakati 16:17-18
Alilomthibitishia Yakobo kuwa amri,
Na Israeli liwe agano la milele.
Akisema, Nitakupa wewe nchi ya Kanaani,
Iwe urithi wenu mliopimiwa;
5) Tunza furaha.
1 Wathesalonike 5:16
Furahini siku zote;
Kila siku unatakiwa uitunze furaha yako. Furaha haihamishiki huwezi kuhamisha furaha ya Jana ukaileta leo, ukiwa mtu wa kununa utapata magonjwa ,muepuke mtu anayekuondolea furaha yako.
Wafilipi 4:4
Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini
Furahi hata k**a huna kazi ,huna pesa unatakiwa furahia upendo wa kristo.
6) Shukurani
1 Wathesalonike 5:18
shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.
Usiwe mtu wa lawama ,usiwe mtu wa manung'uniko pamoja na changamoto unazopitia, ni mangapi Mungu aliyokutendea unakosa kumshukuru? Kuna watu maisha yao ni lawama tu, jifunze kumshukuru Mungu.
7) Kufanya huduma au kazi ya Mungu.l
1 Wakorintho 15:58
Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana.
Kuna watu wenye huduma ya kuombea, kutia moyo, kushuhudia, kuegemeza, jiimarishe katika Bwana fanya kwa bidii, usiangalie au kuvunjwa moyo na mtu.
8) Maombi(kuomba).
Luka 18:1
Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.
Luka 21:36
Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu.
Usipoomba kuna vitu hutaepushwa, kuna majaribu utaingia, tunapaswa kuomba, kukesha bila kukata tamaa, ukiomba Mungu atakunusuru na mabaya yaliyopangwa juu yako.
Waefeso 6:18-19
kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;
Pia na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili;
Kwa sala, na maombi kudumu kwa kuwaombea watakatifu.
Ukiomba na kuona maombi yako yanaisha mapema, badilisha mazingira ya maombi na mtindo wa kuomba. K**a umepiga magoti, simama au tembea, n.k
Omba unapohisi hatari, unapokuwa njia panda omba, unapokosea au umetenda dhambi usimkimbie Mungu,bali mkimbilie kwa toba.
Kuna aina nyingi za maombi lazima ujue unaomba maombi gani kuna maombi ya Shukurani, vita, kukata rufaa, n.k.
9) Zuia ulimi wako usinene mabaya au hila.
1 Petro 3:10
Kwa maana,
Atakaye kupenda maisha,
Na kuona siku njema,
Auzuie ulimi wake usinene mabaya,
Na midomo yake isiseme hila.
Utakosa raha, utakosa amani, utakosa baraka maishani, k**a kinywa chako kitanena hila au mabaya. Mabaya na hila vinakuondolea furaha yako. Mengine yatakayokuondolea furaha ni;
a) Umbeya/ usengenyaji
Umbeya ni kuongea habari ambazo hujaulizwa. Kusengenya ni kuongea habari za mtu ambaye hayupo ambapo akiwepo huwezi kuziongea
b) Uchonganishi au udhalilishaji
Uchonganishi ni kuwakosanisha watu bila wao kujua.
c) Matusi yasitoke kinywani mwenu.
d) Uongo na uzushi
Maneno ya udhaifu k**a vile, Nitapata kazi kweli?, nitafanikiwa kweli?, nitapona kweli?
10) Utoaji wa sadaka.
Matendo mema, utu, ukarimu, n.k.
2 Wakorintho 9:8-9
Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema;
k**a ilivyoandikwa,
Ametapanya, amewapa maskini,
Haki yake yakaa milele.
Ndugu msomaji na mfuatiliaji wa somo hili, Mungu anatupa maelekezo jinsi ya kutengeneza maisha ya ushindi siku zote. Kubali kufuata na kuyaishi haya, utamwona Mungu maishani.
K**a umeguswa na somo hili na unataka kumpa Yesu maisha yako, yaani kuokoka, au kuzaliwa mara ya pili, karibu kanisani kwetu, au nenda kanisa la kiroho karibu na wewe, mwone mchungaji atakusaidia. Ubarikiwe. Amen.
Kwa msaada zaidi na maombezi, fika kanisani, Hekalu la Neema, Bigwa Morogoro. Au wasiliana nasi kwa simu 0689213966, au kupitia FACEBOOK:Pastor Katana Mwangome M'baya, na kwa YOUTUBE: Pst Katana. Pia unaweza kutoa sadaka yako kwa Mungu kupitia M- pesa 0752119763 au Tigo-pesa 0654894607, Mungu akubariki. Amen