Rev. George Mamuya

Rev. George Mamuya Bwana Yesu asifiwe wapendwa. Karibu sana kwenye ukurasa huu kwa ajili ya kujadili masuala ya kiimani na kuona makuu ambayo Mungu anatendea watu wake

KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI THEOLOJIA YA MFUNGO KULINGANA NA KANISA LA KILUTHERI NA MCHUNGAJI GEORGE MAMUYA. Mfungo wa Kw...
27/02/2026

KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI THEOLOJIA YA MFUNGO KULINGANA NA KANISA LA KILUTHERI NA MCHUNGAJI GEORGE MAMUYA.

Mfungo wa Kwaresma katika Kanisa la Kilutheri ni kipindi cha siku 40 (bila kuhesabu Jumapili) kinachoanza Jumatano ya Majivu na kuishia Jumamosi Kuu, kikilenga toba, tafakari, sala, na kujinyima ili kumkaribia Mungu. Ni wakati wa kiroho wa kujiandaa kwa Pasaka, ukisisitiza kusikiliza Neno la Mungu, kutoa sadaka, na matendo ya huruma.

Ni vigumu kuepuka mada ya kufunga wakati Kwaresima inapoanza kila mwaka. K**a ilivyo kwa sehemu zote za maisha ya Kikristo, inategemea motisha ya moyo wako.

 Kwa upande mmoja Haupaswi kuacha kitu ikiwa motisha yako ni kuteseka kidogo na Yesu au kufuata sheria.

 Na kwa upande wa pili Unaweza kuacha kitu ikiwa motisha yako ni kukua katika imani yako.

Kufunga kulikuwa kumefanywa kwa hiari katika kanisa la kwanza, lakini umonaki ulipokuja, uliilazimisha k**a desturi ya lazima na kuwafanya watu waifikirie k**a tendo la kujihesabia haki. Ni kwa sababu hii kwamba Kanisa la Kilutheri kwa sehemu kubwa limeepuka kuhimiza kufunga. Ukisoma Ungamo la Augsburg lisilobadilika kifungu cha 22 kinasema

“Sikukuu za kanisa, kalenda na sherehe ni muhimu kwa ajili ya maadhimisho ya kidini, lakini maadhimisho na ibada hiyo si muhimu kwa ajili ya wokovu. Mila za kibinadamu (k**a vile maadhimisho ya kitu/jambo fulani, Kufunga, kutoshiriki aina Fulani ya chakula k**a nyama kipindi fulani) ambazo hufundishwa k**a njia ya "kustahili" neema, hufanya kazi kinyume na Injili.”

 Ingawa mfungo unasisitiza nidhamu ya kiroho, Kanisa la Kilutheri linaweka mkazo zaidi kwenye mabadiliko ya moyo na maisha (toba ya kweli) kuliko sheria kali za chakula. Ni kipindi cha kutambua umuhimu wa ukombozi wetu kupitia Kristo

 Kufunga kunaweza kufanya mambo mema kwako. Katika Katekisimu Ndogo ya Dr. Martin Luther anasema, kwenye Fungu la tano, sakramenti ya meza ya Bwana sehemu ya nne

"Nani anayestahili kupewa Sakramenti hii? Kufunga chakula na kujitengeneza kimwili ni mazoezi mema, lakini mwenye kustahili na kuwa tayari kuipokea ni yeye ayaaminiye maneno haya. Mwili umetolewa na damu inamwagika, kwa ajili yenu, kwa ondoleo la dhambi. Lakini asiyeamini maneno hayo na kuona mashaka haistahili kabisa. Kwani neno hili "kwa ajili yenu" linataka mioyo yenye imani kabisa." Maneno ya Biblia: K*t. 12: 3-8; 25-27, Yn. 4: 10; 6: 1-10; 48-59, 1Kor. 11: 26-29, Ufu. 3:20.

 Kufunga kunaweza kutukumbusha kuhusu kumtegemea Mungu badala ya rasilimali za ulimwengu huu

 Kufunga kunaweza kuwa njia ya kuokoa rasilimali ili ziweze kutolewa kwa maskini. Kufunga ni njia ya kujidhibiti katika ulimwengu ambapo kujikana kunaonekana k**a uhalifu dhidi ya ubinadamu.

 Tunapaswa kufahamu wazi kuwa kufunga hakutupi msamaha wa dhambi zetu, lakini unaweza kutusaidia kuzingatia mawazo yetu juu ya maisha, kifo, na ufufuo wa Yesu, ambao husamehe dhambi zetu. Na kuchagua kumfuata maishani Yesu alizungumzia kufunga k**a desturi ya kawaida katika siku zake, na hakushutumu matumizi yake (Mt. 6:16-18). Yeye mwenyewe alifunga, kwa mfano, alipojaribiwa jangwani. Lakini wanafunzi wake hawakufanya hivyo; wala hakuamuru ifanywe. Soma jibu la Yesu katika Luka 5:33-39 kuhusu kwa nini wanafunzi wake hawakufuata desturi ya kufunga. Mafarisayo wa siku za Yesu waliona kufunga k**a kazi yenye sifa nzuri (Luka 18:12), bila kutambua kwamba mbele za Mungu mtu "huhesabiwa haki kwa imani katika Kristo na si kwa kushika sheria" (Gal. 2:16).

Vipengele Muhimu vya Kwaresma Kilutheri:
1. Toba na Tafakari: Waamini wanahimizwa kuchunguza mioyo yao na kutubu dhambi, wakitafakari mateso na kifo cha Yesu Kristo.

2. Kufunga na Kujinyima: Kujinyima chakula au anasa fulani k**a ishara ya njaa ya kiroho na utii kwa Mungu.

3. Ibada na Neno: Kuongezeka kwa ibada za katikati ya wiki na usomaji wa Biblia.

4. Matendo ya Huruma: K*toa sadaka kwa wahitaji, kutembelea wagonjwa, na wafungwa.

Wavulana Vs Wasichana. NANI MSHINDI?
26/10/2024

Wavulana Vs Wasichana. NANI MSHINDI?

KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI JIMBO LA KILIMANJARO MASHARIKI USHARIKA WA HIMO  MAHUBIRI YA SIKU YA BWANA YA 6 BAADA YA UTAT...
06/07/2024

KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI JIMBO LA KILIMANJARO MASHARIKI USHARIKA WA HIMO

MAHUBIRI YA SIKU YA BWANA YA 6 BAADA YA UTATU, SIKUKUU YA VIJANA TAREHE 07/07/2024

MADA: BIDII YA KIJANA, MAFANIKIO YA KANISA

MASOMO: ZABURI 119:9 – 16, 1 YOHANA 2:13 – 17, *MITHALI 21:5

SHABAHA: Wasikilizaji watambue kuwa Kijana anayo matokeo mazuri kwa kanisa k**a akitumia juhudi alizopewa.

UTANGULIZI
Bwana Yesu asifiwe, leo 07/07/2024 ambayo ni kilele cha mwezi wa Vijana kwa mwaka huu wa 2024 tumepewa mada isemayo bidii ya Kijana, Mafanikio ya Kanisa. Ili kuweza kuchambua mada hii lazima tuanze kwa kuangalia maana ya maneno Kanisa, Kijana, Bidii na Mafanikio.

Kanisa linaweza kuelezwa katika maana mbili:-
a. Kanisa ni nyumba au jengo ambalo wakristo wanakutana kumwabudu Mungu wao. (
1Kor 11:18)
b. Kanisa ni jumuiya ya watu wote wanaomwamini Yesu Kristo ulimwenguni kote. (Mt 18:15 – 17, Mdo 12:5, Mdo 9:31, Mdo 2:41 – 42, Efe 2:20 – 22, 1Kor 12:28)

Kijana tunaweza kuangalia maana yake kulingna na vyanzo mbalimbali:-
a. Kijana kutokana na tafsiri ya kanisa ni mtu yeyote aliyepata kipaimara hadi miaka 35 na wengnine husema miaka 45.

b. Kulingana na mafundisho ya kijamii ni mtu yeyote aliyefikisha umri wa miaka 18 hadi miaka 35.

c. Kulingana na Wayahudi wao wanafundisha kuwa kijana ni yule mwenye miaka 20 hadi miaka 60. wayahudi walliwatambua vijana kwa umri huo kwa sababu walijua kuwa wao ndio watu wenye uwezo wa kuzalisha katika jamii na hata kulipa fidia na waliwatoza ghali kuliko makundi mengine yoyote.

Bidii (kutoka neno la Kiarabu) ni ile hali ya kuonyesha juhudi za dhati katika kufanya jambo fulani. Bidii ya mtu inaweza ikamfanya afikie malengo makubwa anayotaka na kujiona yeye ni wa juu.

Mafanikio ni ukamilishaji wa malengo yanayoipatia nchi, jamii au mtu binafsi ustawi, afya njema au hadhi. Mafanikio pia hujulikana k**a ufanisi, maendeleo au neema. Mafanikio hupatikana baada ya kumaliza shughuli fulani au kitu fulani.

Kijana akionyesha juhudi atakamilisha malengo yote yaliyowekwa na kanisa analolitumikia. Na katika kulitafakari hili tuepewa neno kutoka Kitabu cha Mithali 21:5

Mithali nyingi za Suleiman huwa na pande mbili ili kulinganisha na kutofautisha ili kupata somo kamili. Na katika mstari huu ameweka pande mbili ambapo upande wa kwanza zinamuelezea mtu mwenye lengo la kuwa tajiri na upande wa pili ni sifa ya mtu anayataka kuwa maskini.

Mtu mwenye bidii wakati wote anaelekea Utajiri kwa sababu anajua haya yafuatayo ( Mithali 10:4;Mithali 12:11; Mithali 13:4; Mithali 14:4; Mithali 22:29; Mithali 27:18; Mithali 28:19; Mhubiri 10:10)

 Kujituma: Watu wanaotafuta utajiri wanajituma kwa bidii na wanafanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo yao ya kifedha.

 Ubunifu: Wanaweza kuwa na uwezo wa kutafuta njia mpya na za ubunifu za kujipatia utajiri au kufikia malengo.

 Kujiamini: Kujiamini ni muhimu sana katika kufanikiwa katika biashara na uwekezaji, na watu hawa mara nyingi wana imani kubwa katika uwezo wao.

 Ujuzi wa Kifedha: Wanaweza kuwa na uelewa mzuri wa masuala ya kifedha na uwekezaji, na wanaweza kutumia maarifa haya kwa faida yao.

 Uwezo wa Kuchukua Hatari(Risk takers): Watu wanaotafuta utajiri mara nyingi wanaweza kuchukua hatari kwa kufanya uwekezaji au kuanzisha biashara mpya na kufikia malengo.

 Kujifunza na Kuboresha(Continuos Improvement): Wana uwezo wa kujifunza kutokana na makosa yao na kuboreka katika njia wanazotumia kutafuta utajiri.

 Kujitolea/Kujinyima(Self Sacrifice): Wanaweza kuwa na nguvu ya kujitolea katika kufikia malengo yao.

 Mtandao wa Kijamii(Network): Wanaweza kuwa na mtandao mzuri wa kijamii ambao unaweza kuwasaidia katika biashara zao na kutafuta fursa za kukamilisha malengo

 Kujitambua(Self Awareness/Knowledge): Wanaweza kuwa na uelewa mzuri wa malengo yao na wanajua wanataka nini katika maisha.

 Kujielekeza(Focus): Wana uwezo wa kujiwekea malengo na kuwa na mkakati wa kufikia malengo hayo.

 Kufanya Kazi Kwa Bidii(Hard work): Wanaweza kuwa tayari kufanya kazi kwa saa nyingi na kwa bidii ili kufikia malengo yao.

 Uwezo wa Kujisimamia: Wanaweza kuwa na uwezo wa kujisimamia wenyewe na kuwa na nidhamu katika matumizi yao ya muda na rasilimali.

 Kufanya Maamuzi Bora ya Fedha: Wanaweza kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi bora ya kifedha kwa kuzingatia faida na hasara.

Mvivu ambaye anayeelekea kwa mhitaji huwa anajijali mwenyewe hapokei Ushauri na wala hana uvumilivu katika kukabiliana na mambo (Mithali 26:16, 20:21;28:20,22;) na wana sifa zifuatazo

 K*tumia muda mwingi kuangalia TV, sinema au tamthilia. Dalili moja ya mtu kuwa masikini siku za mbeleni inatajwa kuwa utaratibu wa kutumia muda mwingi kuangalia TV badala ya kufanya shughuli za kuingiza kipato au hata shughuli za ziada zenye kuongeza manufaa fulani hata k**a sio pesa moja kwa moja.

 Kununua chakula (Fast food) Hii ni tabia nyingine ambayo inatajwa ambayo k**a hairekebishwi hupelekea umaskini. K**a haukumbuki ni lini ulipika mwenyewe nyumbani kwako kwasababu unanunua chakula wakati wote basi hiyo ni dalili mbaya.

 Kuchelewa kuamka. Tabia hii kufanyika katika umri wa ujana inaelezwa kuwa ni dalili ya kuukaribisha umaskini katika siku za mbeleni. Vijana ambao wanakuwa wazembe kufanya kazi kwa bidii kwenye kipindi chao cha ujana, hufanya kazi zaidi na kwa tabu wakifika umri wa kuanzia miaka 40 tena yawezekana bila malipo makubwa, na hii ni kwasababu hawakutumia vizuri muda wao wa ujana kufanya kazi na kuwekeza kwa ajili ya miaka ya mbeleni.

 Kulaumu wengine kwa matatizo unayopitia. Wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa moja ya tabia zinazoweza kumfanya mtu awe maskini ni pamoja na kulaumu watu wengine kutokana na kutofanikiwa kwako.

 K*toweka akiba. Akiba ni jambo la msingi sana katika mapato yoyote yanayopatikana. Akiba ya pesa husaidia pindi likitokea tatizo, inaweza kuwa ugonjwa, safari ya dharura na kadhalika. K**a huna akiba likitokea tatizo itakubidi uuze mali yako yoyote au uchukue mkopo ili kutatua tatizo hilo.

 Kufanya manunuzi yasiyo kwenye mpangilio. Hii ni pamoja na kununua vitu ambavyo havikuwa kwenye bajeti au mpangilio. K*tokana na hili, wataalamu wanashauri kufanya manunuzi ukiwa tayari umeandika orodha ya vitu unavyotaka kununua na sio kwenda sokoni au dukani na kuangalia kilichopo ili ufanye manunuzi.

 Kuzaa watoto wengi. K**a wewe ni kijana na una mpango wakuja kuwa na familia yenye watoto wengi, hakikisha hali yako ya uchumi iko imara kabla haujaanza kuzaa watoto hao.

 K*topima afya mara kwa mara. Inawezekana ukaona sio suala la msingi kupima afya mara kwa mara lakini hili ni suala la msingi kwa watu matajiri, kwani kuishi ukiwa na uhakika wa afya ndio msingi wa kuishi maisha ya mafanikio.

 K*tumia pesa kabla ya kuzipata. K**a una tabia ya kukopa pesa kipindi ambacho hauna pesa huku ukitarajia kuzilipa pindi utakapopata pesa, hiyo ni dalili ya umaskini kukunyemelea.

 Kuwa na marafiki wasio na malengo makubwa. Marafiki huweza kukusaidia kufikia malengo yako uliyojiwekea, lakini pia huweza kufanya usifikie malengo yako hayo. Inashauriwa kuwa k**a unataka kufanikiwa hakikisha unatumia muda mwingi zaidi na marafiki ambao wana malengo makubwa ya maisha, wanawaza mambo chanya na sio mambo hasi muda wote, ambao wanakukumbusha kufanya vitu vya msingi.

Kuna jambo kubwa Zaidi linalotegemea bidii ya kijana ambayo ni kumpendeza Mungu kuzishika amri za Mungu ili kuurithi uzima wa milele. Hata mtume petro amesema wazi kuwa inahitaji bidii nyingi ili kuonyesha kuwa umekubaliwa (2 Petro 1:5 – 11) na hasa katika kipindi hiki kilichojaa mafundisho ya uongo na unabii wa uongo tunapaswa kujiadhari Zaidi na kuhakikisha kanisa linasonga mbele (Yohana 1:13, Warumi 9:15 – 16, Mathayo 7:21 – 23)

YANAYOMPASA KIJANA KWA KANISA
 Kanisa k**a ilivyo maana yake kuwa ni jengo linaloabudiwa na wakristo na pia ni jumuiya ya wote wanaomwamini Yesu Kristo kuwa ni Bwana na Mwokozi wao.

 Hivyo tunamuangalia kijana jinsi ambavyo anatakiwa kujihusisha katika hizi sehemu mbili.



YANAYOMPASA KIJANA KWENYE JENGO LA KUABUDIA
 Nyumba ya ibada ni nyumba ya kuabudia na sio ya kufanyia kebehi na karaha ( Mt 2:12
– 13)

 Unapokuwa katika jengo la ibada unapaswa kuvaa nguo za kujisitiri na safi ( Hes 8:21, Mwa 3:21, 1Tim 2:9 – 10, kumb 22;5, Mk 9:43, 1Kor 8:9, Lk 17:1)

 Ukiwa kanisani unapaswa kuwa na nidhamu sio kutembea kwa “madoido”, unapaswa kutuliza macho, unapaswa kutulia usitoketoke hovyo, tusisome magazeti, sms, kutokusinzia, asiongee wa kunongonezana kanisani, asile chochote wala kutumia simu kanisani.

 Kijana anapaswa kupanda maua, kufagia, kudeki, kufuta vumbi, na kuhakikisha mazingira yote ya ndani na nje ya Jengo la kanisa yanatunzika vizuri.

 Kijana anapaswa kumsaidia mchungaji kazi k**a vile kusoma neno, kusoma matangazo, kugonga kengele, nk.

 Kijana anapaswa kujiandaa kuwa kiongozi ( Law 19:30, Zab 29:2)

YANAYOMPASWA KIJANA KWA KANISA K**A JUMUIYA YA WAAMINIO (KWA WAKRISTO WENGINE)
 Kuishi maisha ya ujamaa ( Mdo 2;44 – 45, Mdo 4:32) k**a vile kuwatembelea wagonjwa sababu wanahitaji kufarijiwa ( Lk 1:37)

 Kijana anapaswa kuwahudumia wahitaji k**a vile kutoa damu, huduma ya kwanza, kuwasaidia wazee, vilema, kujihusisha na shunguli za maziko, harusi, kufundisha Sunday school, kushiriki kazi za kitaifa, kukaribisha wageni, kuandaa semina na mikutano ( Mt 25: 39 – 40)

 Kijana anapaswa kutoa sadaka kwa kazi ya kanisa ( Kumb 16:17, 2Kor 8:12, Mt 3:
27, 1Kor 9:13 – 14, 2Kor 9:7, Mt 6:2)

 Kijana anapaswa kufanya uinjilisti na kujitahidi kuyajua maandiko ( Mdo 18: 28) na kuwa wavumilivu ( Tito 3:9)

HITIMISHO
Sisi vijana tujiulize maswali haya:-

 Mimi ni nani?

 Je, baada ya muda Fulani ninataka kuwa nani?

 Je, ninataka kuwa na ujuzi/utaalamu gani?

 Je ninahitaji kujiajiri au kuajiriwa?

 Je ninatamani kumiliki nini maishani?

Mungu atusaidie sote ili tuweze kumtumikia Mungu kwa bidii ili kuleta matokeo chanya kwa kanisa letu.
AMEN.

KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI JIMBO LA KILIMANJARO MASHARIKI USHARIKA WA HIMO  MAHUBIRI YA SIKU YA BWANA YA 5 BAADA YA UTAT...
06/07/2024

KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI JIMBO LA KILIMANJARO MASHARIKI USHARIKA WA HIMO

MAHUBIRI YA SIKU YA BWANA YA 5 BAADA YA UTATU TAREHE 30/06/2024

MADA: NINYI NI BARUA YA KRISTO

MASOMO: ZABURI 119:1 – 8, YOHANA 13:12 – 15 *1 THESALONIKE 1:8 – 10

SHABAHA: Wasikilizaji wawe na tumaini hai kwa Yesu ili awafanye kuwa kielelezo na kuwavuta wengine kwake.

UTANGULIZI
Bwana Yesu asifiwe, leo tunakumbuhana kuwa sisi ni Barua ya Kristo. Neno Barua ni ujumbe wa kimaandishi unaotumwa kwa mtu mwingine au watu wengine. Inawezekana kumwachia mtu ujumbe wa kimaandishi yaani barua mahali fulani lakini mara nyingi barua inatumwa kwa njia ya mtume au shirika linalofanya kazi hii kibiashara (Posta).

Barua ni chombo muhimu katika utamaduni wa kila jamii. Zinategemea kuwepo kwa watu wanaojua kusoma na kuandika. Si lazima ya kwamba kila mtu anayetuma barua au kuipokea anajua kuandika au kusoma, maana inawezekana kutumia msaada wa watu wengine. Lakini mawasiliano kwa barua ni uhamasisho mkubwa kwa watu kujifunza na kuboresha elimu hiyo.

Ndiyo maana sisi Wakristo tunaitwa kuwa ni barua ya Kristo, maana yake tumebeba ujumbe wa Kristo ambao tunapaswa tuufikishe kwa watu kwa njia ya maneno na matendo yetu.

Kwahiyo watu wanatusoma sisi Wakristo kuwa tumebeba ujumbe gani kutokana na matendo yetu, hivyo tunafanyika kuwa wajumbe Wakristo, (2Wakorintho 5:20)

Mwandishi anatuambia kuwa kutokea thesalonike mvumo ulisikika. Kuvuma naana yake kutokana na tafsiri ya kiyunani iliyotumika katika kitabu cha wathesalonke ni kuagiza, kuwa maarufu, kutoa taarifa na kufundisha kwa sauti.

Neno la Mungu walilolipokea wathesalonike kwa umaarufu wake walijua ni agizo la kufundisha kwa sauti na kutoa taarifa.

Neno la Mungu ni habari njema ya Yesu Kristo kufa kwa ajili ya dhambi zako na kufufuka tena (Matendo 8:25). Ni lazima kushuhudiwa na kuhubiriwa (Matendo 8:25) na kufundishwa (Matendo 15:35) na kusemwa (Matendo 16:32). Inapaswa kuchapishwa kwa upana wake(Matendo 13:49).

Habari hii njema inapaswa kutukuzwa na kuaminiwa na wale wanaoipokea (Matendo 13:48). Tunahitaji kuomba Habari njema iende bila kuzuiliwa kila mahali inapowasilishwa (2 Wathesalonike 3:1).

Wathesalonike wanatambulika jinsi walivyompokea Mungu kwa namna walivyowapokea watumishi wa Mungu Kupokea kwako neno la Mungu kwa uchangamfu kupitia wajumbe wake ni sehemu ya kielelezo chako muhimu kwa waamini wengine.


Sanamu ni kitu chochote unachokiamini kuwa ni cha thamani kuliko Mungu mwenyewe. Chochote unachokiweka katika nafasi ambayo Mungu pekee ndiye anapaswa kuchukua katika maisha yako ni sanamu. Sanamu zaweza kuwa chakula au vinywaji au watu au mahusiano au pesa au sanamu halisi ya kuchonga ambayo unainamia.

Kwanza, tokeo moja la kumgeukia Mungu ni kwamba sasa unamtumikia. Kumgeukia Mungu huku kunahusisha macho, masikio, na moyo. Inahusisha kuona, kusikia, na kuelewa kile ambacho Mungu anataka kwako.

Kwa hiyo, kumngoja kwako Yesu Kristo kutoka mbinguni ni tokeo moja lisiloepukika la kumgeukia Mungu kutoka kwa sanamu. Mimi na wewe hatungojei kufa tu! Tunamngoja Kristo kutoka mbinguni.

Na huo ndio ufunguo - Yesu ndiye ufunguo. Kristo ndiye anayetuokoa na ghadhabu hii. Tunaokolewa kutoka kwa ghadhabu ya Mungu kupitia Yesu kulingana na Warumi 5: 9. Mungu hakutuweka kwa hasira yake, bali tupate wokovu - kwa Bwana wetu Yesu Kristo (1 Wathesalonike 5:9).

Katika habari hii tunaona mambo sita Muhimu ambayo watu wanapaswa kusoma kwetu:-

1. UINJILISTI NI DAI LA MSINGI KWA MUUMINI
Habari hii njema inapaswa kutukuzwa na kuaminiwa na wale wanaoipokea (Matendo 13:48). Tunahitaji kuomba Habari njema iende bila kuzuiliwa kila mahali inapowasilishwa (2 Wathesalonike 3:1).

2. MKRISTO THABITI IMANI YAKE HAITETERESHWI NA HALI INAYOMKUMBA
Nyakati zote, mahali popote na umbali wowote unamfanya mkristo thabidi kuongeza nguvu ya kumtumikia Mungu na sio kumkatisha tamaa au kumvunja moyo.

3. MUUMINI SAFI ANAWAPOKEA KWA FURAHA WATUMISHI WA MUNGU
Wathesalonike wanatambulika jinsi walivyompokea Mungu kwa namna walivyowapokea watumishi wa Mungu Kupokea kwako neno la Mungu kwa uchangamfu kupitia wajumbe wake ni sehemu ya kielelezo chako muhimu kwa waamini wengine.

4. MKRISTO SAFI HAONI AIBU KUTUBU KWA MAHUSIANO BORA NA MUNGU
Mahusiano na Mungu yanavurugwa na watu kutegemea Sanamu kuliko Mungu. Sanamu ni kitu chochote unachokiamini kuwa ni cha thamani kuliko Mungu mwenyewe. Chochote unachokiweka katika nafasi ambayo Mungu pekee ndiye anapaswa kuchukua katika maisha yako ni sanamu. Sanamu zaweza kuwa chakula au vinywaji au watu au mahusiano au pesa au sanamu halisi ya kuchonga ambayo unainamia. Mkristo anamtanguliza Mungu juu ya vitu

5. MKRISTO ANAYEJUA THAMANI YA WOKOVU WAKE ANAMTUMIKIA MUNGU KWA BIDII
Anayejua ameokolewa na kumgeukia Mungu ni kwamba sasa unamtumikia. Kumgeukia Mungu huku kunahusisha macho, masikio, na moyo. Inahusisha kuona, kusikia, na kuelewa kile ambacho Mungu anataka kwako.

6. MKRISTO WA KWELI HAPOTEZI TUMAINI LAKE KWA MUNGU
Mkristo anamngoja Yesu Kristo kwa bidii. Kumngoja kwako Yesu Kristo kutoka mbinguni ni tokeo moja lisiloepukika la kumgeukia Mungu kutoka kwa sanamu. Mimi na wewe hatungojei kufa tu! Tunamngoja Kristo kutoka mbinguni.

HITIMISHO
Mungu atusaidie kuwa barua safi itakayomvutia kila atakayesoma.

KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI JIMBO LA KILIMANJARO MASHARIKI USHARIKA WA HIMO  MAHUBIRI YA SIKU YA BWANA YA 4 BAADA YA UTAT...
22/06/2024

KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI JIMBO LA KILIMANJARO MASHARIKI USHARIKA WA HIMO

MAHUBIRI YA SIKU YA BWANA YA 4 BAADA YA UTATU TAREHE 23/06/2024

MADA: IWENI NA HURUMA

MASOMO: ZABURI 103:8 – 13, WAEFESO 4:32, *MATHAYO 8:14 – 17

Tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane k**a na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi. (Efeso 4:32)

SHABAHA: Wasikilizaji watambue kuwa wana wajibu kuwabebea wengine mizigo na kuwasamehe ili pendo la Kristo lizidi kujaa mioyoni mwao.

UTANGULIZI
Huruma ina maana ya wema ulio tayari kusaidia na kusamehe. Sifa hiyo kwanza ni wa "Mungu" kadiri ya dini mbalimbali, zikiwemo Uyahudi na Ukristo.

Tunajua kwamba, kulingana na Biblia, Mungu ni "Mungu mwenye huruma na mwenye neema, mwepesi wa hasira , wingi katika upendo na uaminifu "(Zaburi 86:15). Rehema zake hazikomi na ni za milele. Fadhili zake haziwezi hazikomi; ni mpya kila asubuhi (Maombolezo 3: 22-23).

Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, alionyesha sifa zote za Baba, ikiwa ni pamoja na rehema yake. Yesu alipowaona marafiki zake wakiomboleza katika kaburi la Lazaro, aliwahurumia na kulia pamoja nao (Yohana 11: 33-35). Akiwa na rehema kwa mateso ya wengine, Yesu aliwaponya umati mkubwa uliokuja kwake (Mathayo 14:14), pamoja na watu waliotaka uponyaji wake (Marko 1: 40-41). Alipomwona umati mkubwa k**a kondoo bila mchungaji, huruma yake ilimwongoza kuwafundisha mambo ambayo wachungaji wa uongo wa Israeli waliyoacha.

Yohana wa Kwanza 3:17 anauliza, "Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo?'' Mwanzo aliumba mwanadamu kwa mfano wake, ambaye apaswa kuwa mfano wa sifa za Mungu , ikiwa ni pamoja na huruma.

Biblia ni wazi kuwa rehema ni sifa ya Mungu na ya watu wa Mungu pia. "Ikiwa mtu atasema, 'Ninampenda Mungu' na bado anachukia ndugu yake, yeye ni mwongo. Kwa yeyote asiyempenda ndugu yake, ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hajamwona "(1 Yohana 4:20).

Katika mistari hii michache tuliyosoma kwa ujumla tunaweza kusema Yesu anachukua dhambi, hatia, na udhaifu wetu kwa sababu hatuwezi kufanya hivyo wenyewe, na tunaweza kujifunza mambo mengi sana ila nataka tuyaone haya matatu kwa jumapili ya leo.

1. FAMILIA ZA MARAFIKI WA YESU ZINAPITIA MASUMBUFU PIA
Familia nzuri ya Kikristo ni ile inayozingatia kanuni za Biblia na ile ambayo mwanafamilia anaelewa na kutimiza jukumu lake alilopewa na Mungu. Familia si taasisi iliyoundwa na mwanadamu. Iliundwa na Mungu kwa faida ya mwanadamu.

Petro anafahamu hilo na anakuwa mkarimu kwa Yesu na kwa watu wa familia akiwemo mama mkwe wake aliyekuwa mgonjwa.

Tunapotazama masumbufu haya katika familia ya Petro yanatufundisha mambo haya chanya

 Yanakuza huruma ya kijamii. (Yesu alimhurumia mkwe wa Petro)
 Yanaleta sifa za familia. (Uwepo wa Yesu unafanya watu wengi kuipa umaarufu familia)
 Yanaunganisha kaya katika mazoezi ya ibada. (Wwatu kutoka kaya nyingine wanakuja kushuhudia matendo makuu ya Mungu)
 Yanaamsha shukrani za vitendo na za upendo (Mama anapoponywa mara moja anahudumu kwa furaha)

2. UWEPO WA YESU KATIKA FAMILIA NI MWISHO WA MATATIZO YOTE
Yesu alipofika Kwenye nyumba ya Petro yale yaliyokuwa yakisumbua familia ya Petro yalikoma mara moja na watu wengi kupitia uwepo wa Yesu kwenye familia nao waliponywa na kufunguliwa kwenye vifungo walivyokuwa navyo.

Ukarimu wa Petro kwa Yesu unaleta wakovu kwa familia yake na kwa eneo lake lote.

3. BARAKA ZA YESU KRISTO ZINATUVUTA KUMTUMIKIA KWA FURAHA
Mkwe wa Petro anapoponywa, tunaona mara moja anainuka na kuwahudumia Yesu na wanafunzi wake. Na hili lilikuwa ni jukumu la mama kuwahudumia watu chakula na baba alikuwa na jukumu la kuhakikisha mama hakosi chakula cha kuwahudumia wageni. Na hili linatuweka bayana kuwa Mtu anayemtumikia Yesu ni yule aliyeponywa kimwili au Kiroho au vyote viwili yaani mwili na roho.

Maswali ya Kujiuliza hapa:-
 Je, huduma yetu inawezaje kuwa kielelezo cha shukrani zetu kwa Mungu?
 Je, wewe na familia yako mnaweza kupongeza na kuwaombea wengine wanapofikia lengo la utumishi wao? (Luka 4:38)

HITIMISHO
Tukubali Yesu awe katika maisha yetu ili atuwezeshe kuwa na huruma ambayo inaleta wokovu katika familia zetu na watu wote waliotuzunguka.

AMEN

KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI JIMBO LA KILIMANJARO MASHARIKI USHARIKA WA HIMO  MAHUBIRI YA SIKU YA BWANA YA 3 BAADA YA UTAT...
16/06/2024

KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI JIMBO LA KILIMANJARO MASHARIKI USHARIKA WA HIMO

MAHUBIRI YA SIKU YA BWANA YA 3 BAADA YA UTATU TAREHE 16/06/2024 SIKU YA KKKT

MADA: UMOJA WETU, NGUVU YETU

MASOMO: ZABURI 124:1 – 8, YOHANA 17:20 – 21, *NEHEMIA 2:18 – 20

SHABAHA: Wasikilizaji watambue umuhimu wa umoja na wawe tayari kuulinda kwa gharama yoyote.

UTANGULIZI
Bwana Yesu asifiwe, leo tunazungumza juu ya Umoja wetu kuwa ndio nguvu yetu, siku hii muhimu ambayo tunasheherekea sikukuu ya KKKT.

Biblia inahimiza umuhimu wa umoja na muungano. Umoja kati ya wengine ni mzuri na wa kufurahisha (Zaburi 133:1). Umoja ni muhimu kwa sababu kanisa ndio mwili wa Kristo (1Wakoritho 12:27), na mwili huezi kujitenganisha au kujikosesha amani. Utengano ukifanyika, basi kanisa linakoma kuwa mwili na kubaki kuwa kundi la watu waliotengana.
Mpango wa Yesu kwa kanisa lake ni watu washirikiane kwa imani.

Siri ya umoja inaanza na jinsi tunavyojiona sisi wenyewe kimwili na jinsi tunavyoona wengine. Neno la Mungu toka Wafilipi 2:3: linasema "Msitende neno lolote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake." Utengano mara mingi hutokea kanisani wakati tunapokua na tamaa na kujiona wazuri kuliko wengine.

Umoja ndio dai kubwa kwa kanisa tangu wakati wa Yesu alipoliombea kanisa lililokuwepo na litakalotokea baadae. Na Umoja huu ujengwe katika upendo utayapata hayo ukisoma injili iliyoandikwa na Yohana ule mlango wa 17. Dai hili kwa kanisa halijawahi kukosa nguvi hata siku moja hata k**a kumeendelea kuonekana mgawanyiko mkubwa ndani ya kanisa.

Mwaka 1938 makanisa saba ya Kilutheri yaliungana k**a Muungano wa Makanisa ya
Kilutheri Tanganyika, na tarehe 19 Juni 1963 yalikuwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania.

Makanisa hayo saba ni:-
a) Kanisa la kiinjili la Kilutheri la Iraqw
b) Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la kaskazini mwa Tanganyika
c) Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Kaskazini Magharibi mwa Tanganyika
d) Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Kati mwa Tanganyika
e) Kanisa la kiinjili la Kilutheri la Kusini mwa Tanganyika
f) Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Usambara Digo
g) Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Uzaramoni – Uluguru

Siku ya leo tunaadhimisha miaka mia moja na thelathini na saba (137) ya ulutheri Tanzania.

Lengo la KKKT ni kuwapa watu nafasi ya kumfahamu Yesu Kristo ili kupata uzima wa milele.

Kanisa limejengwa juu ya msingi wa Yesu Kristo, linaongozwa na Neno la Mungu k**a linavyopatikana katika Agano la Kale na Agano Jipya (Biblia ya Kikristo), na limeimarishwa katika sakramenti.

Mwaka huu tunajifunza kutoka kitabu cha Nehemia, Nehemia alitambua kuwa Yerusalemu walikuwa katika dhiki na mashutumu mengi huku ukuta wa mji pamoja na malango yake yalikuwa yaeharibika sana. Hivyo aliamua kukaa chini na kuweka mpango jinsi gani angeweza kurudisha matuaini kwa waisrael na kuwakumbusha juu ya nguvu zao katika kuifanya kazi kwa sababu wanamtegemea Mungu. Wayahudi walipokea katika mtazamo mkubwa wa Umoja yale aliyowashirikisha Nehemia ila waliinuka wapinzani na kupinga umoja kwa kuwadharau, kuwaonyesha uchungu, huzuni mashambulizi ya vita, kuwasemea uongo na hata kutumia manabii wa Uongo ili umoja usiwepo ila Nehemia na watu wake hawakukata tamaa hadi ukuta ulipokamilika. Tunajifunza nini katika habari hii?

1. ASIYEPENDA UMOJA NI ADUI MKUBWA WA MAENDELEO
Nehemia alitamani kurejesha mji wa Yerusalemu katika umaridadi wake, na alitambua kuwa ili hilo liwezekane ilimbidi kuhakikisha umoja unakuwepo miongoni mwa wayahudi. Nehemia alimuomba Mungu, akaweka mipango akatafuta kibali akawashirikisha watu na wote wakaona umuhimu wa umoja kwa maendeleo yao isipokuwa wachache tu.

Ili kuwa na mafanikio ya Kimwili na kiroho tunahitaji kuwa na umoja wa kweli na tukubali kugharimika ili umoja uzidi kuwepo.

2. UMOJA UNATHAMANI KUBWA MAISHANI TUULINDE KWA HEKIMA
Nehemia kwa kutambua thamani na Umoja alimuomba sana Mungu ampe kibali cha kuulinda umoja hata k**a kungetokea upinzani.

Umoja ni kitu kizuri ila sio wote wanaopenda umoja, na wote wasiopenda umoja wana sababu zao ila wewe unapaswa kujikumbusha wakati wote kuwa maendeleo yanatanguliwa na umoja unaoleta Amani miongoni mwetu.

3. WAPINZANI WAKUWEZESHE KUTUNZA UMOJA ZAIDI
Wapinzani wa Nehemia walitumia silaha za kawaida kabisa ili kutaka kumshinda, silaa hizo ni k**a vile Uongo, kudharau, dhihaka, kuhuzunisha, kutia uchungu,vita ya wazi na hata kutumia manabii wa Uongo.

Ukiona watu wanasema uongo juu yako, wanakudharau, wanakudhihaki, kusababisha uchungu, kupambana nawe wazi wazi na kutumia hata manabii wa uongo ujue kuwa wameona maendeleo yako na wamejua umoja ndio unaokuwezesha kufanya hivyo. Wanatumia mbinu mbalimbali ili kuhakikisha wanakuchafua wewe na kuvunja usikivu wa watu wasikuamini kuwe na mafarakano, wewe usiogope endelea kutunza tabia yako njema na Mungu atakupigania.

HITIMISHO
Mungu atusaidie katika changamoto yoyote tusikubali kupoteza umoja wetu na ikibidi tugharamie kuutunza umoja.

AMEN.

KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI JIMBO LA KILIMANJARO MASHARIKI USHARIKA WA HIMO  SIKU YA BABA DUNIANI 16/06/2024  Historia ya...
16/06/2024

KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI JIMBO LA KILIMANJARO MASHARIKI
USHARIKA WA HIMO

SIKU YA BABA DUNIANI 16/06/2024

Historia ya Waisraeli yafichua kwamba baba alistahili kuwa wa hekima katika kuwapa maagizo watoto wake katika njia za Mungu na neno lake kwa minajili ya ukuaji wao kiroho na maisha yao. (Kumb 6:5, Mith 22:6, Efe 6:4)

Sehemu ya manufaa ya Waefeso 6:4 imefafanuliwa kwa mwelekeo wa ndani sana- waelimishe, welee, kuza tabia yao katika maisha yao kwa kuwaelekeza na kuwafunza neno la Mungu. Baba Mkristo ni chombo katika mikono ya Mungu.

Martin Luther alisema, “Liweke tunda kando ya kiboko ili umpe akifanya vyema.” Nidhamu lazima itekelezwe kwa umakini sana na mafundisho kila siku kwa maombi mengi.

“Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katka haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema” (2 Timotheo 3:16-17). Jukumu la baba la kwanza ni kumzoesha mtoto na maandiko.

Sikukuu ya akina baba ni sikukuu ya kidini. Aliyeianzisha (Sonora Smart Dodd) ambaye mtoto wa k**e wa William Jackson Smart alikuwa kanisani mwaka 1909 akisikiliza mahubiri siku ya mama duniani na jinsi ilivyokuwa ikielezewa kwa bashasha zote na kwa bahati yeye alikuwa amelelewa na baba peke yake kwa sababu mama yake alifariki akiwa mdogo kabisa pamoja na wadogo zake watano.

Sikukuu hii ya wababa duniani iliadhimishwa mara ya kwanza siku ya kukumbuka kuzaliwa kwa William Jackson Smart tarehe 19/06/1910 na iliungwa mkono na viongozi wa dini na hata sasa kanisa katoliki la Roma limeendelea kuadhimisha siku kuu ya Mtakatifu Joseph, tarehe 19 mwezi wa tatu ikiwa ni heshima kwa akina baba.

Raisi wa Marekani Calvin Coolidge aliunga mkono maadhimisho haya. Alikuwa raisi wa thelathini wa Marekani (1923 – 1929)

Rais Lyndon B. Johnson rais wa thelathini na sita (36) wa Marekania (1963 – 1969) alitangaza kuitambua siku ya wababa duniani.

Na rais wa thelathini na saba (37) wa marekani (1969 – 1974) alitia saini sheria inayotaja Jumapili ya tatu ya Juni k**a siku ya baba duniani. Na tangu wakati huo imeendelea kuadhimishwa maeneo mbalimbali duniani.

Sikukuu ya baba imekuwa ni sherehe iliyobeba umaarufu duniani kwa ajili ya kuwaenzi na kuwaheshimu kina baba na kusherehekea ubaba, vifungo vya baba, na ushawishi wa baba katika jamii.

K*tokana na chimbuko la siku hii tunaweza kusema kwamba ni siku ya kuwaenzi kina baba wote wanaojitolea kutekeleza majukumu yao ya ubaba katika kuwalea watoto wao na kuwakumbusha wanaume waliojisahau kutimiza wajibu wao kuanza utekelezaji.


Katika maadhimisho hayo, wababa wameonesha kwa vitendo baadhi ya shughuli zinazofanywa na wanawake ili kuonesha namna baba bora anavyoshirikiana na mke wake katika majukumu ya matunzo, malezi na makuzi ya familia na watoto.

Baada ya miaka miamoja na kumi na moja (111) tangu kuanzishwa kwa siku hii, nchini Tanzania waliadhimisha kwa mara ya kwanza huko Shinyanga jumapili ya tarehe 20/06/2021 katika viwanja vya Zimamoto na yaliongozwa na kauli mbiu isemayo “Tembea katika viatu vyake, thamini mapambano yake”

Katika maadhimisho hayo yaliyoongozwa na Naibu waziri ofisi ya waziri mkuu (Kazi, vijana na ajira) Mhe Patrobas Katambi alikaza kuwa “Lengo la siku hii ni kuwafanya wanaume kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia,maadhimisho haya yamekusudia kutambua mchango wa wababa k**a viongozi wa familia kwa kuwa wana wajibu mkubwa wa kulinda, kutunza,kuongoza na kustawisha familia katika Nyanja za kijamii, kielimu, kiuchumi na kiroho”.

Na pia aliongeza kwa kusema “Maadhimisho haya yawe sehemu ya mabadiliko makubwa katika jamii yetu na kuondoa dhana potofu ya mfumo dume unaokandamiza makundi mengine wakiwemo wanawake na watoto. Sisi wababa ni walinzi na wafariji wakuu wa wanawake hivyo ni vyema tuwatunze, tuwapende na tuwaendeleze wake wake zetu”,

Kwa mwaka huu wa 2024 siku hii ya wababa itaadhimishwa tarehe 16/06/2024 ni siku ya kuwapongeza wababa wote wanaopambana kuhakikisha maisha yanaendelea na wanaotunza familia zao.

Una baba? Umepanga kumfanyia nini baba siku ya leo? Na wewe baba umejiandaaje kusheherekea sikukuu hii?

Ingawa kwa kiasi kikubwa ilikuwa sikukuu ya kidini, Siku ya Akina Baba imefanywa kibiashara kwa kutuma kadi za salamu na utoaji wa zawadi. Wengine huzingatia desturi ya kuvaa waridi jekundu ili kuonyesha kwamba baba ya mtu yu hai au waridi jeupe kuonyesha kwamba amekufa. Wanaume wengine - kwa mfano, babu au wajomba ambao wamechukua majukumu ya uzazi - mara nyingi pia wanaheshimiwa siku hiyo.

Hongera kwa siku ya wababa duniani.

Mch George Mamuya
KKKT - Usharika wa Himo.

Address

67
Marangu

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when Rev. George Mamuya posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Contact The Place Of Worship

Send a message to Rev. George Mamuya:

Share