20/12/2025
FAIDA ZA KUSIKILIZA NA KUFUATA MAELEKEZO YA MUNGU
1. Mungu ataamuru Baraka yake ikujilie au ikufuate.
Kumb 28: 1, 2
Mbaraka wa Mungu ni Zaidi ya mafanikio ya mwanadamu. Unaweza ukafanikiwa kwenye biashara yako kwa mfano lakini usiwe na mbaraka wa Bwana juu ya hiyo biashara.
Kwa nini?
Kwa sababu biashara inaweza ikakupa faida nyingi lakini isikusaidie kukutoa kimaisha. Na ndio maana watu wengi wanafanya kazi za kuajiriw lakini maisha yao ni magumu sana kana kwamba hawana kazi lakini wana kazi. Unaweza ukajiuliza hivi hizo pesa na mishahara yao wanapeleka wapi? Lakini ukweli ni kwamba kazi zao au biashara zao hazina mbaraka wa Mungu ambao ungewafanikisha kimaisha.
Kwenye mbaraka wa Mungu kun ulinzi wa Mungu, Amani ya Mungu, utoshelevu wa Kimungu, uzidisho wa Kimungu na kibali cha Mungu.
2. Unapata uhakika wa ushindi
Waamuzi 7: 1-2, - 7, - 9 –
Gidioni aliandaa jeshi kubwa sana kwa ajili ya kupigana na Wamidiani lakini Mungu alimwambia apunguze jeshi hilo hadi kufikia wat5u 300, na kuna maelekezo alimpa ya nini cha kufanya.
-Mungu akikuahidi kuwa atakupigania ni kweli kwamba atakupigania. Unachotakiwa ni kusikiliza sauti ya Mungu inayokupa maelekezo au mbinu utakayotumia kumshinda adui.
Unaweza ukawa unajua mbinu nyingi sana za kumshinda adui lakini Mungu anataka umsikilize yeye kwa sababu Mungu yeye ni Bwana wa vita, anajua ni mbinu ipi uitumie saa hiyo unapigana kwenye vita yako au kwenye hali yako.
NB: Ni muhimu sana kusikiliza maelekezo ya Mungu anayokupa hata k**a ndani mwako unajua kuwa unafahamu namna ya kutoka kwenye shida uliyo nayo.
Haiingii akilini jeshi la watu 300 kupambana na jeshi lenye watu k**a mchanga wa ufukweni halafu wategemee kushinda. Ni lazima Mungu mwenyewe ahusike. Njia za Mungu si sawa na njia za mwanadamu, na mawazo ya Mungu si sawa na mawazo ya mwanadamu.
Kwa nini Mungu anataka umsikilize kwanza? Ni kwa sababu anafanya mambo yake yote kwa utukufu wake- yaani anafanya hayo ili ajitwalie utukufu. Kwa hiyo ukifanya chochote ili ujitukuze mwenyewe, utainua vita na Mungu mwenyewe ambayo hakuna anayeweza kukusaidia. (Mungu hampi yeyote utukufu wake).
Pia unaweza ukasoma habari za kuanguka kwa ukuta wa mji wa Yeriko katika Yoshua 6: 1 – 16
3. Unapata kufahamu chanzo au asili ya tatizo unaloliombea.
2 Samweli 21: 1 – 2 – 14
Hapa tunaona habari ya Mfalme Daudi katika kipindi chake kulitukia njaa ambayo ilidumu kwa muda wa miaka mitatu, na Biblia inasema ilikuwa mwaka kwa mwaka. Ndipo Daudi akautafuta uso Bwana na Bwana akamjibu.
Biblia haijaweka wazi mfalme Daudi aliomba maombi ya namna gani lakini tunaona kile alichomjibu Bwana. Bwana alimjibu “ni kwa sababu ya Sauli alivyowaua Wagibeoni”.
- Lile neno “ni kwa sababu ya” linaonyesha kuwa Daudi aliomba kujua chanzo cha ile njaa. Ni sawa na kwamba aliomba “kwa nini njaa imekuja juu ya nchi yake”.
- Jibu la Munngu kwa Daudi halikuondoa njaa iliyokuwa juu ya nchi bali lilimpa kujua chanzo cha njaa ile au sababu ya kuwepo kwa njaa ile.
- Kulikuwa hakuna namna yoyote ile ya ile njaa kuondoka isipokuwa kushughulikia chanzo chake.
Wakati mwingine unaweza ukawa unaombea jambo Fulani lakini Mungu akakusemesha kitu tofauti na jambo unaloliombea. Halafu unashangaa.
- Kumbe Mungu anakuonyesha chanzo cha tatizo lako na halitaondoka mpaka umeshughulika na chanzo hicho.
- Tusikimbilie tu kukemea tukidhani kila tatizo tunalopitia limesababishwa na Shetani kumbe mengine ni adhabu kutokana na kosa lililofanyika huko nyuma.
Kipindi kile cha Daudi hakukuwa na damu ya Yesu ndio maana iliwabidi walipize kisasi ili kuondoa chanzo cha tatizo la njaa ile lakini sisi tunayo damu ya Yesu inayonena mema kuliko damu za watu, wanyama na hata ndege.
Hebu fikiria Daudi kaka mwaka wa kwanza anaona njaa haiondoki, mwaka wa pili bado tu, unafika mwaka wa tatu ndio anaamua kuutafuta uso wa Bwana.
- Maana yake ameacha kuomba kwamba Mungu aiondoe njaa bali anaomba kujua chanzo cha njaa ni nini.
- Usifikiri Biblia inaposema mwaka kwa mwaka kwamba Daudi alikuwa haombi, alikuwa anaomba. Lakini alipoona hakuna mabadiliko yoyote ilibidi abadilishe prayer point.
- Mwaka wa kwanza Daudi anaomba lakini hatuoni Mungu akijibu chochote na mwaka wa pili vivyo hivyo, lakini mwaka wa tatu Mungu anajibu.
NB: Hebu kaa utafakari ni kitu gani ambacho Mungu amekuwa akikuonyesha au akikusemesha lakini huelewi wala hujui?
- Kwa sababu wengi wamekwama mahali na hawajasogea mbele kwa muda mrefu wakidhani kuwa Mungu hajawajibu maombi yao kumbe ni wao hawajamsikiliza Mungu kwa makini ili kupata maelekezo ya kufanyia kazi.
Ukishindwa kusikiliza sauti ya Mungu inayosema nawe ndani yako utashindwa kuvuka mahali pa kubwa sana katika viwango vya kumjua Mungu kwenye maisha yako.