08/05/2026
SIKU YA NANE YA KUFUNGA NA KUOMBA
SOMO: MAMBO YA ROHONI HUTAMBULIKANA KWA JINSI YA ROHONI NA KWA IMANI
MCH HERENA MWAKISININI
Waebrania 11:1-3 “Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Maana kwa hiyo wazee wetu walishuhudiwa. Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo Dhahiri”.
Mungu ni wa kuaminiwa, tunapomwamini ni kwa sababu tumezisikia habari zake. Tumezisikia habari zake kuwa yeye ndiye muumbaji wetu na kwa njia hiyo tumeamini kwa kusikia.
Mwezi wa tano ni mwezi tunaomwendea Mungu kwa imani juu ya mambo tunayoyatarajia.
Neno la Kristo ndilo linalotufanya tumwamini Mungu na kwa kuamini kunasababisha jambo kutokea. Pasipo kuamini hakuna matokeo ya jambo lolote kutokea, lakini unapoomba kwa kuamini ndipo unasababisha jambo kutokea.
Kuamini kunapoambatana na matokeo kunasababisha wale wanaokuzunguka kuvutwa na kile ulichonacho, kuwafanya waone kuna umuhimu wa kuambatana nawe
Marko 11:22-26 “Yesu akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu. Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu. Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. Lakini k**a ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu”.
Ili uweze kuona matunda ya kile unachokiamini na matokeo ya kile unachokitafuta lazima ujifunze kuachilia na kusamehe, ndipo Mungu atayasikia maombi yako na kusababisha matunda ya imani yako yakujilie.
K**a una kitu chochote ndani ya mwezi huu lazima ukiachilie ili Mungu aweze kusababisha matendo makuu yatokee kwako na ndipo utayaona matokeo ya kuamini kwako.
MAOMBI
Omba Mungu katika mfungo huu, Mungu akafufue vipawa ndani yetu na kila aliyelala akaamke.
Omba nguvu ya Roho Mtakatifu ije ikujaze kwa upya pale ulipopungua.
Omba Mungu akuachilie hekima na kutambua sauti yake
Kutoka 35:10-11 “Na kila mtu kati yenu aliye na moyo wa hekima na aje, na kuyafanya hayo yote ambayo Bwana ameyaagiza”.
Omba Mungu akufanye kwa upya na akufinyange vile apendavyo ili ufae kwa kazi yake.
Omba Mungu akatupe nguvu ya kushinda majaribu.
Yakobo 1:12 Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao.
Ng’oa kila mbegu mbaya inayotokana na kuzaliwa, elimu na mazingira.
Vunja laana yoyote iliyoingia kwako na kwa kanisa na ondoa mzigo mzito kwenye maisha yako.
- Ondoa mzigo wa maradhi, magonjwa.
- Ondoa kudharauliwa
- Ondoa kunyanyaswa
- Ondo kukandamizwa
- Ondoa kukataliwa.
Nenda ukakatae kila roho za visasi na malipizi juu yako