01/02/2026
UTARATIBU WA KUJIUNGA NA MAUA SEMINARY
Seminari ni taasisi za malezi na elimu zinazomilikiwa na Kanisa Katoliki au Mashirika ya Kitawa ya Kikatoliki. Zimeanzishwa mahususi kwa ajili ya kuwaandaa vijana wa kiume katika malezi ya jumla na endelevu ya kiroho, kitaaluma, kimaadili na kibinadamu, kwa lengo la kuwasaidia kutambua, kukuza na kuthibitisha wito wao wa kuwa mapadre au watawa katika Kanisa Katoliki.
Kwa msingi huo, wito wa kipadre au kitawa ndio kigezo cha kwanza na cha msingi katika mchakato wa kujiunga na Maua Seminary. Mwombaji anatakiwa kuonesha dalili za wazi za wito huo kupitia mwenendo wake wa maisha, ushiriki wake katika shughuli za Kanisa, maadili mema, pamoja na nia ya dhati ya kujitoa kwa huduma ya Kanisa na kwa wokovu wa watu.
Baada ya kuthibitishwa kwa wito, uwezo wa kitaaluma huangaliwa kulingana na ngazi ya seminari husika. Mwombaji anatakiwa kuwa na kiwango cha elimu kinachokubalika kwa mujibu wa sera ya elimu ya shirika, miongozo na kanuni za seminari, pamoja na uwezo wa kuendelea kielimu na kimalezi.
Aidha, vigezo vingine muhimu vinavyozingatiwa katika mchakato wa udahili wa Kujiunga na Kidato cha Kwanza (Form I) ni pamoja na:
1. Mwombaji wa kujiunga na Kidato cha Kwanza anatakiwa:
• Awe katika umri unaokubalika kwa mujibu wa miongozo ya Seminari Ndogo.
• Aonyeshe dalili za wito, nidhamu na tabia njema.
• Awe na afya njema ya mwili na akili.
• Awe amepokea sakramenti za Ubatizo na Ekaristi, na awe
anaendelea vizuri katika maisha ya sakramenti.
• Awe na idhini na ushirikiano wa wazazi au walezi.
• Aandike barua ya maombi kwa Mkurugenzi wa Miito wa Shirika
kuanzia Januari anapoingia darasa la saba. Ahakikishe barua yake
imepita kwa Paroko.
• Awe na barua ya mapendekezo (ushuhuda) kutoka kwa Paroko.
• Awe amemaliza elimu ya msingi na kufaulu Mtihani wa Taifa wa
Darasa la Saba.
• Kufaulu mtihani wa taifa haitoshi, hii ni hatua ya kwanza tu.
• Apitie usaili wa awali unaofanywa na uongozi wa seminari (k**a
ni Jimbo la Moshi)
• Mwombaji anapaswa kufanya mtihani ulioandaliwa na seminari na
kufaulu kwa kiwango tarajiwa (inategemea na ufaulu wa jumla).
• Usahihishaji wa mitihani na kuchagua wanafunzi (selection)
utafanywa na k**ati ya elimu.
2. Mwombaji wa Kujiunga na Kidato cha Tano (Form V)
Mwombaji wa kujiunga na Kidato cha Tano anatakiwa:
• Mwombaji aandike barua ya kuomba kujiunga na seminari kwa
Mkurugenzi wa Miito wa Shirika.
• Baada ya kuandika barua mwombaji atapaswa ahudhurie semina
ya kufahamiana itakayoandaliwa na Mkurugenzi wa Miito wa
Shirika.
• Awe amemaliza elimu ya sekondari ya chini na kufaulu Mtihani wa
Taifa wa Kidato cha Nne kwa kiwango cha daraja la kwanza
(Division I) au daraja la pili (Division II)
• Aonyeshe ukomavu wa awali wa kiroho, kimaadili na kibinadamu,
unaolingana na ngazi ya Seminari Ndogo
• Awe na ushiriki mzuri katika maisha ya Kanisa, hasa katika
sakramenti na huduma za parokia
• Awe na afya njema ya mwili na akili
• Awe na barua ya mapendekezo kutoka kwa Paroko au kiongozi
halali wa Kanisa.
• Awe tayari kufuata kanuni na mtindo wa maisha ya seminari
• Apitie usaili wa kina unaofanywa na viongozi wa seminari
• Awe na idhini na msaada wa wazazi au walezi
• Awe na uwezo wa kuchangia ada na mahitaji ya seminari
kulingana na taratibu zilizowekwa.
3. Masharti ya Jumla
Kwa waombaji wote wa Seminari Ndogo:
• Nidhamu, utii na maadili mema ni nguzo kuu za maisha ya
seminari.
• Udahili hufanyika kwa kuzingatia mapendekezo ya Parokia,
tathmini ya k**ati ya elimu ya shirika kutokana na ripoti ya
Mkurugenzi wa Miito na nafasi zilizopo.
• Udahili wa mwisho ni haki ya k**ati ya elimu, kwa mujibu wa sera
ya elimu ya shirika na miongozo ya seminari.
• Kukubaliwa kujiunga na seminari hakumaanishi moja kwa moja
kukubaliwa kuwa padre au mtawa, bali ni kuanza safari ya malezi
ya wito
Kwa ujumla, Seminari Ndogo ni kitalu cha malezi ya awali ya wito, hivyo mchakato wa kujiunga unaongozwa zaidi na kutambua na kukuza wito kuliko ufaulu wa kitaaluma pekee, kwa ajili ya ustawi wa Kanisa na huduma ya baadaye kwa Watu wa Mungu.