02/03/2023
KUTOKA MEZANI KWA MKURUGENZI MKUU
Hatimaye juma la maadhimisho ya utumishi wa wanawake katika kanisa la T.A.G limewadia. Mwaka huu wa 2023 juma hili linaanza tar 27 Feb 2023 na kufika kilele chake siku ya jumapili ya tar 5 Machi 2023. Juma hili linajulikana k**a juma la WWK. Hili ni juma la furaha sana na juma la huduma maalumu za wanawake katika kanisa.
Tunamshukuru MUNGU kwamba Kanisa la T.A.G linatambua utumishi wa wanawake na linatoa nafasi kwa wanawake kumtumikia MUNGU katika kipindi chote cha mwaka. Juma hili ni juma maalum la kusherehekea utumishi huo wa wanawake mwaka mzima.
Idara inayosimamia huduma za wanawake katika kanisa la T.A.G inaitwa idara ya wanawake watumishi wa Kristo WWK. Idara hii huwaunganisha wanawake makanisani ili kuwaelekeza kuliishi NENO la MUNGU na kuwa baraka majumbani kwao, makanisani kwao, kwa mchungaji wao na kwenye jamii wanayoishi na hata ulimwenguni kote. Himizo kubwa ni kumtumikia MUNGU na kuhakikisha kuwa mahali popote mwanamke wa WWK alipo ufalme wa MUNGU unajengwa.
Katika juma hili maalumu wanawake tunatumika katika madhabahu za makanisa yetu tukimshukuru BWANA kwa vipawa mbalimbali alivyotupa na huduma alizotujalia kuwa nazo ili kulibariki kanisa. Baadhi ya huduma zinazofanywa na wanawake wakati huu ni pamoja na ; kuendesha semina za NENO la MUNGU, semina za ndoa na familia, au semina za mabinti. Maeneo mengine wanawake hufanya mikutano ya injili, ushuhudiaji wa nyumba kwa nyumba, au kupeleka Upendo wa KRISTO kwa wagonjwa na watu wenye mahitaji maalum. Siku ya jumapili ndio sikukuu yenyewe haswa.
Siku hiyo ya jumapili ya tar 5 Machi ndio kilele cha sherehe hizi na katika siku hiyo huduma zote kanisa zinakuwa chini ya idara ya WWK. Furaha hii inakamilishwa kwa kumtegemeza na kumbariki mchungaji na familia yake kwa zawadi kubwa kuliko zote alizopewa katika mwaka mzima. Zawadi hii ni ishara ya kusema kwake wanawake tunakupenda na tunamshukuru MUNGU Kwa ajili ya huduma Yako; Ni namna ya kumtia moyo mchungaji na kuonyesha kwa matendo kusimama naye katika huduma.
Katika juma hili pia tunaleta hamasa kwa wanawake wote katika makanisa ya T.A.G kutilia mkazo utumishi wao kwa BWANA wakiwa katika umoja na wanawake wengine. Kumtumikia MUNGU Kwa pamoja kuna matokeo makubwa zaidi kuliko kumtumikia MUNGU ukiwa peke yako. K**a wewe ni mwanamke katika T.A.G na bado hushiriki katika huduma za WWK huu ni wakati wa kujiunga na WWK na kudhamiria kudumu katika utumishi huu wa pamoja kwa wanawake katika kanisa. NENO la MUNGU linafunua kwamba ni katika umoja MUNGU huamuru baraka (Zab 133).
Jambo la muhimu kukumbuka mwaka huu tunaposherehekea sikukuu yetu ni kwamba bado k**a kanisa Tunaendelea kumtaka BWANA na nguvu zake. Huu sasa ni mwaka wa nne wa utekelezaji wa mpango mkakakti wa kanisa wa miaka 13 ya moto wa uamsho. Tunapaswa kuendelea kuomba na kujitoa na kutumiwa na MUNGU kusababisha uamsho mkuu kutokea. Andiko letu mwaka huu linatoka katika kitabu cha Hosea 6:3. Himizo ni kukaa katika hali ya kutarajia kwani BWANA hakika atatujilia k**a mvua za vuli.
Tudumu kuomba sana na kumtumikia MUNGU sana ili kuona madhihirisho ya nguvu za MUNGU katika maisha na huduma zetu.
Ninapohitimisha nawatakia wanawake wote katika kanisa la T.A.G ushindi, furaha na amani katika kuadhimisha juma letu hili mpka kufikia siku ya kilele chake yaani sikukuu ya WWK. MUNGU azidi kuwapa wanawake wa WWK nguvu mpya ya kumtumikia kwa viwango vya juu zaidi katika mwaka huu 2023.
NAWATAKIA HERI NA BARAKA KATIKA JUMA LA WWK NA SIKUKUU YA WWK
MCH: FARAJA HAMULI
MKURUGENZI MKUU WA WWK T.A.G