16/05/2024
KUHUSU IMANI
"Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo." Warumi 10:17
Somo la imani bado linaonekana gumu na tata sana kwa wengi, ingawa ni rahisi. Utata wake umefichwa katika urahisi wake. Wengi husema hawana imani au wana imani ndogo; hata hivyo, unawakuta watu hao hao wanaamini mambo mengi sana isipokuwa Neno la Mungu.
Leo, nimeongozwa kuzungumzia suala linalohusu imani.
Baada ya wengi kusikia wahubiri wakizungumzia imani na umuhimu wake; walihisi hitaji la imani, na hivyo walitaka kuwa nayo. Walitaka kuitengeneza imani ndani yao, na wengine kuiongeza. Lakini, wengi hawafahamu wafanye nini ili wawe na imani, hivyo hitaji lao la 'imani kubwa' limewafanya kupoteza hata imani ile ndogo waliyokuwa nayo.
Fahamu hili kuhusu imani. Hakuna imani inayojiumba yenyewe. Imani yote hutolewa na hupokelewa; rahisi namna hiyo. Neno linapopokelewa, ndani yake imani inapokelewa. Neno la madaktari kwa mgonjwa hubeba imani katika dawa; mwongozo wa watengenezaji gari hubeba imani katika gari yao. Unaweza hata kumwamini rubani na maisha yako kwa kumwona tu akiwa amevalia sare. Vipi kuhusu Neno la muumba wako?
Mioyo yetu ni udongo mzuri ya kupandia imani, lakini tunachagua mbegu tunazoruhusu kukua k**a imani ndani yetu. Wengine wamewaamini wazazi wao kuwapatia msaada, zaidi ya wanavyoweza kumwamini Mungu; wengine wana imani na ripoti ya daktari na maagizo yake, kuliko Neno linavyosema (ripoti ya Mungu).
Changamoto ya mtu yeyote anayehangaika na imani ni kwamba, bado hajamjua Mungu katika kweli, wala Neno lake.
Usihangaike kujitengenezea imani yako, pokea tu neno la Mungu zaidi; ndani yake ni imani. Imani imefungwa ndani ya Neno. Kadiri unavyopokea Neno, ndivyo imani inavyoongezeka ndani yako. Baada ya kuwa na imani yote unayohitaji, ifanyie kazi ili kuifanya iwe na imara zaidi.
- Harufu ya Uzima
Na D. K. Davis
0713816586