23/02/2019
AINA TATU(3) YA WATU WANAOKUZUNGUKA.
Bwana Yesu asifiwe.
Nakusalimu katika jina lipitalo majina yote mtu wa Mungu. Leo nataka niongee nawe aina tatu ya watu wanaokuzunguka katika ulimwengu huu.
Linapokuja swala la mafanikio ya kiroho ama kimwili hapa duniani, watu wanaokuzunguka wana mchango mkubwa mno. Mara nyingi tumekuwa tukirudi nyuma kimaendeleo ama hatufikii hatima ya mafanikio kwa sababu ya watu tulionao/wanaotuzunguka. Abrahamu alichelewa kupokea nchi ya ahadi kwa sababu ya kuambatana na Lutu (Mwanzo 12 na 13). Kwa hiyo katika maisha yako kuwa makini na nani unamwambia ndoto ama siri zako, ama nani unaambatana naye.
Sasa nataka tuone kwa undani aina hizi tatu za watu wanaokuzunguka;
1. WASIRI: Hawa ni aina ya watu ambao wapo kwa ajili yako, ni aina ya watu wanaokupenda bila kutegemea jambo lolote kutoka kwako. Uwe juu ama chini kimaisha, uwe sahihi ama umekosa bado watakuwa na wewe muda wote. Ni aina ya watu ambao wamejiunganisha na maisha yako haijalishi ni ya namna gani. Watakusifia utakapofanya vizuri na ukikosea watakukosoa, watakukaripia pale utakapofanya mambo ya kipuuzi, siku zote watakushauri mambo ya mafanikio. Ukiumia wataumia na wewe, ukifurahi watafurahi na wewe, ukiwa na uzuni watakupa faraja, wapo tayari kuingia gharama ama kwenye matatizo kwa ajili yako. Mara nyingi watu wa namna hii huwa wanakuombea ufanikiwe ata kuwazidi wao. Watu wa namna hii ni wachache sana na k**a unao wawili ama watatu katika maisha yako, basi wewe umebarikiwa. Unamkumbuka Ruthu kwa Naomi katika kitabu cha Ruthu??? Ngoja nikupe maandiko machache uone, Ruthu 1:16-17 "16 Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu;
17 Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; BWANA anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami." Hayo ni maneno ya Ruthu kwa mama mkwe wake Naomi.
2.WASHIRIKA: Hii ni aina ya watu ambao hawapo kwa ajili yako, bali kwa ajili ya kile ulichonacho chenye faida kwao. Ilimladi una kile wanachokitaka basi watakuwa na wewe kwa hali na mali, watafanya kazi na wewe yamkini wanajua kuna kitu watafaidika. Watu wa namna hii wakikutana na mtu ambaye anaweza kuwapatika kile wanachokitaka kwako kwa ubora ama ukubwa zaidi yako uwe na uhakika wataachana na wewe. La msingi ni kutambua watu wa namna hii hawapo kwa ajili yako bali ulichonacho/wanachokipata kwako, na usipokuwa makini unaweza kuwachanganya na wasiri. Ukikwama kiuchumi ama kimaisha utawatambua vizuri, hata mmoja hautamuona na wataishia kukuumiza moyo wako. Unawakumbuka wale makutano waliokula mikate na samaki mpaka wakavimbiwa??? Baada ya siku kadhaa walimsaka tena Yesu, unajua kilichowafanya wamsake?? Ebu ona kilichowafanya wamsake tena Yesu, Yohana 6:24-26 "24 Basi mkutano, walipoona ya kuwa Yesu hayuko huko wala wanafunzi wake, waliingia mashuani wenyewe, wakaenda Kapernaumu wakimtafuta Yesu.
25 Hata walipomwona ng’ambo ya bahari, walimwambia, Rabi, wewe umekuja lini hapa?
26 Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba." Sasa hawa ndo aina ya waumini wengi walioko makanisani, wanamtafuta Yesu kwa sababu wameskia anaweza kutatua shida zao, wakifanikiwa huwaoni tena makanisani. Wakristo wengi wapo kanisani si kwa sababu wanampenda Mungu, bali wapo kanisani kwa sababu Mungu anaweza kujibu maitaji yao, hawapo kwa ajili ya Mungu bali wanachoweza kupata kutoka kwa Mungu.
3. WAPINZANI WENZA: Watu wa namna hii hawapo kwa ajili yako wala kwa ajili ya wanachoweza kufaidika kutoka kwako, bali watu wa namna hii wapo kwa ajili ya kile ambacho upo kinyume nacho. K**a upo kinyume na jambo fulani, basi ata wao watakuunga mkono kwa sababu wapo kinyume na jambo hilo pia, ikiwezekana ata kifedha watakuwezesha ili ushindi upatikane. Mara nyingi watu wa namna hii uwa hawapendi wajulikane wapo upande gani, ujificha nyuma ya kivuli chako ili wasionekane. Wakati mwingine wataungana na wewe kwa hali na mali ili wakusaidie umpige adui yako. Sasa usichanganyikiwe na muungano wao, watakuwa na wewe mpaka ushindi upatikane, wapo kwa ajili ya kutimiza kusudi na likitimia hutawaona tena. Usivunjike moyo wakiondoka maana kusudi lao litakuwa limetimia. Urafiki wa namna hii mara nyingi unafanyika kati ya mtu na mtu, nchi na nchi, kabila na kabila, ukanda na ukanda, nk. Mwanamke huyu na mwanamke huyu wanaungana kwa ajili ya kumchamba mwanamke fulani kisa wote hawampendi. Unaikumbuka vita kati ya Shinari, Elasari, Elamu, Goimu na Sodoma, Gomora, Adma, Seboimu, Soari??? Wafalme wa hizo nchi waliungana kulingana na ukanda wao kupigana kwa sababu tu ukanda mmoja hauelewani na mwingine (Mwanzo 14:1-12). Unamkumbuka Mfalme Sauli na Daudi walipoungana kwa sababu tu ya adui Goliati?? Baada ya hapo kilichoendelea ni nini? Uhasama baina yao wawili, mifano ipo mingi kwenye biblia ila kwa leo ngoja niishie hapo.
Ni maombi yangu kwa Mungu somo hii lizae matunda ndani yako, uweze kuwatambua aina ya watu waliokuzunguka.
Mungu akubariki.