12/07/2026
KONGAMANO LA WANAWAKE - ZIWA MASHARIKI
Katika kujenga maendeleo ya kweli ulimwenguni, usawa kati ya mwanamke na mwanaume ni msingi usioweza kupuuzwa. Kadiri jamii inavyoendelea kutambua na kuthamini nafasi ya mwanamke, ndivyo uwezo wake wa kuchangia maendeleo ya familia na jamii unavyozidi kuonekana.
Kwa siku tatu, wanawake walikutana katika kongamano maalumu la kutafakari, kujifunza na kushauriana kuhusu namna wanavyoweza kuongeza mchango wao katika maendeleo ya jamii. Katika kipindi chote cha kongamano, washiriki walijifunza na Maandiko Matakatifu na jumbe za Nyumba ya Haki ya Ulimwengu kuhusu nafasi ya wanawake katika maendeleo ya familia na jamii.
Mojawapo ya uelewa uliojitokeza kwa kina ni kwamba familia ndiyo msingi wa kujenga jamii yenye maadili, umoja na maendeleo endelevu. Ilisisitizwa kuwa kila nyumba inaweza kuwa kitovu cha ibada, mazungumzo yenye kujenga, huduma kwa wengine na shughuli mbalimbali za kielimu zinazotolewa kupitia taasisi za mafunzo.
Washiriki pia walitafakari umuhimu wa makundi ya familia k**a njia madhubuti ya kupanua ushiriki wa watu binafsi na familia katika mchakato wa kujenga jumuiya amirifu. Kupitia makundi haya, familia huimarisha urafiki, hujifunza pamoja na kushiriki katika shughuli zinazokuza maendeleo ya kiroho na kijamii.
Aidha, kongamano lilisisitiza nafasi ya akina mama k**a walimu wa kwanza wa watoto. Ilibainika kuwa wanawake wana mchango wa kipekee katika kujenga msingi wa maadili mema, tabia njema na maisha ya kiroho ya watoto na vijana. Uelewa huu umeongeza dhamira ya kuendeleza programu za kielimu na kuimarisha ushiriki wa familia katika malezi ya kizazi kijacho.
Mwisho wa kongamano, washiriki waliondoka wakiwa na hamasa mpya ya kuendelea kuimarisha familia zao, kushiriki kikamilifu katika shughuli za kujenga jumuiya na kuwa chachu ya maendeleo katika maeneo wanayoishi. Ujifunzaji uliopatikana umeweka msingi imara wa kujenga jamii zenye umoja, maadili na uwezo wa kuwalea watoto na vijana katika mazingira yanayokuza utu, huduma kwa wengine na maendeleo endelevu.
Baha'i Tanzania www.bahai.or.tz