31/05/2019
KIPI CHANZO CHA UTOFAUTI KATI YA BIBLIA YA KIKATOLIKI NA ILE YA KILOKOLE / KIPROTESTANTI.
Na Didas Tumaini
UTANGULIZI
Biblia ya Kikatoliki ina jumla ya vitabu 73 wakati ile ya kilokole ina jumla ya vitabu 66.Biblia zote zina idadi sawa ya vitabu vya agano jipya ambavyo ni 27.
Tofauti inakuja kwenye vitabu vya agano la kale ambapo katoliki ina vitabu 7 zaidi ya vile vya kiprotestanti/walokole.Ambapo wakatoliki tuna vitabu vya agano la kale 46 wakati walokole wana vitabu 39 vya agano la kale.
Vitabu 7 zaidi kwa wakatoliki ni Judith,Joshua bin Sira,Hekima ya suleimani,Baruku,Makabayo I&II na Tobit.
KWANINI UTOFAUTI HUU WA VITABU SABA UMEJITOKEZA KATI YA WAKATOLIKI NA WAPROTESTANT/WALOKOLE?
Ni kwasababu sisi wakatokili tunatumia ile tafsiri ya kale ya Kigiriki ya Orodha ya Vitabu vya Biblia (Older Greek / Alexandrian list of authorized books) inayoitwa Greek Canon.
Mnamo mwaka 250BC kabla ya kristo,wanazuoni wapatao sabini wa kiyahudi walipewa kazi ya kuitafsiri Biblia ya agano la kale kwa wakati ule kutoka kwenye lugha yake ya asili ya Kiebrania kwenda kwenye lugha ya Kigiriki. Ikumbukwe miaka hiyo ya 250BC hakukuwa na Agano jipya,kristo alikuwa bado hajazaliwa na waisraeli walikuwa mateka chini ya utawala wa Babiloni.Kuhusu Waisraeli kupelekwa mateka Babuloni rejea (Daniel 1:1-7; 2Mambo ya Nyakati 36:5-7;Isaya 39:5-8)
Orodha ya vitabu vya Biblia ya wakati huo ilikuwa na vitabu 39 tofauti na hii tunayotumia hivi sasa kwa sisi wakatoliki.Katika kipindi hiki hakukuwa na agano jipya kwasababu masiha hakuwa bado amekuja ulimwenguni.Kwahiyo biblia inayozungumziwa ilikuwa na Agano moja tu,agano la kale.Kwahiyo Wanazuoni wale walipotafsiri walijumuisha vitabu vingine 7 vilivyoitwa Deuterocanonical ambavyo viliandikwa na wayahudi waliokuwa uhamishoni lakini kwa lugha ya kigiriki.
Mpaka karne ya tatu kabla ya Kristo,theluthi mbili (⅔) ya waisraeli walikuwa uhamishoni Babuloni hawakuwa tena kwenye nchi yao ya ahadi,Kanaani.Wakuu wa kibabiloni walichagua wale waisraeli wenye akili,hekima na maarifa makubwa na kuondoka nao utumwani/uhamishoni.Ni theluthi moja (⅓) tu ya watoto,wazee na wasiojiweza ndio waliobaki Kanaami.Kundi hili dogo lililobaki waliliita Palestina lakini baada ya vuguvugu la Zionist kwa ulimwengu wa sasa wanajulikana k**a Waisraeli (Hii nayo ni historia ndefu),hawa hawakwenda utumwani babiloni,walibaki kwenye nchi ya Ahadi.Hawa waliongea na kuandika kwa Kiebrania.
Wale waliokwenda utumwani walikatazwa kutumia lugha yao ya asili ya kiebrania,walikatazwa wasiwafundishe watoto wao kwa lugha ya kiebrania badala yake watumie lugha ya Babiloni ambayo ni Kigiriki,kwa kuwa hii ndio iiyokuwa lugha rasmi ya taifa la wababuloni.Watoto waliozaliwa utumwani walilelewa na kufundishwa kwa lugha ya Kigiriki.Hapa kilikuja kizazi kipya cha waisraeli ndani ya nchi ya Babiloni kilichokuwa kinaongea lugha ya kigiriki.
Kizazi hiki ndio miongoni mwa wale sabini waliochaguliwa kuitafsiri biblia yenye vitabu 39 iliyokuwa kwa lugha ya kiebrania kwenda kwenye lugha ya kigiriki.Wanazuoni hao walipewa siku sabini tu kuhakikisha kazi hiyo imekamilika.Kazi ilipokamilika walikuja na Biblia yenye tafsiri ya kigiriki yenye vitabu 46 wakijumuisha vile vitabu saba ambavyo asili yake vilikuwa ni lugha ya kigiriki.Vitabu hivi saba viliandikwa kipindi kile cha uhamisho na kipindi wakiishi uhamishoni (500-100BC) ambapo waandishi wa vitabu hivi saba walitumia lugha ya taifa la kibabiloni kuviandika.
Tafsiri hii mpya kwa lugha ya kigiriki yenye vitabu 46 inajulikana kwa kilatini k**a Septuaginta au kwa namba za kirumi k**a LXX.
Baada ya karne kadhaa kupita na baada ya kristo kuzaliwa,jamii ya waisraeli ilikuwa na dini kuu mbili ila ya kiyahudi,Judaism na ile ya kikristo yaani walioamini katika kristo.
Judaism walivipokea vitabu hivi 46 vya septuaginta na kuvitumia kwa mafundisho yao.Baadae nao Wakristo walivipokea vitabu vyote 46 vya septuaginta na kuvitumia kwa mafundisho yao.
NB:msomaji wangu,kumbuka hapa nazungumzia tu agano la kale ambalo ndio lenye utofauti kati ya biblia yetu ya kikatoliki na ile ya walokole (protestanti).Agano jipya halitofautiani wote tuna idadi sawa ya vitabu na mpangilio wa sura,aya ni mmoja.Yaani wote wakatoliki na walokole tunaanza na injili ya mathayo na kumalizia na ufunuo wa yohane.Labda tu matamshi yanaweza kutofautiana ila mantiki ni ile ile.
Tuendelee;
Ilipofika mwaka wa 90AD, baada ya kristo kuzaliwa viongozi wa dini ya kiyahudi/Judaism waliamua kupitia upya orodha ya vitabu vya septuaginta,Mwaka 70 AD katika kipindi ambacho hekalu la Yerusalem lilibomolewa wa Warumi,Dini ya Kiyahudi ilijitenga na ile ya kikristo na wote waliamua kutumia bilblia tofauti.,ilikuwaje? Ilikuwa hivi.
Miaka 20 baadae wanazuoni wa kiyahudi walianza kuondoka maandiko yenye asili ya kigiriki kwenye biblia yao,ambapo vile vitabu saba (Deuterocanonical) vilivyokuwa vimeandikwa kwa lugha ya kigiriki tokea mwanzo vikaondolewa.Vitabu hivi kiasili havikuwa vimeandikwa kwa lugha mama ya wayahudi yaani Kiebrania,vilikuwa vimeandikwa na wayahudi walioishi uhamishini Babuloni waliokuwa wakizungumza kigiriki k**a kima Sira,Baruku n.k
Baada ya kuondoa vitabu hivyo saba,ndipo ilipopatikana Agano la kale lenye vitabu 39 vyenye asili ya lugha ya Kiebrania tu na waandishi wake waliviandika wakiwa kwenye nchi ya ahadi,Kanaani au Palestina.Orodha hii mpya ya vitabu vya agano la kale inajulikana k**a Palestinian Canon jina hili ni kwa mujibu wan chi yao takatifu kwa wakati ule.Lakini kwa kizazi hiki cha sasa kuna baadhi ya wapalestina wanaendelea kutumia ile orodha yenye vitabu 46 lakini Wayahudi wa sasa ama waisraeli wao bado wanatumia orodha yenye vitabu 39 tu.
Mpaka hapo wakristo wote walikuwa na agano la kale yenye vitabu 46 wakati wayahudi walikuwa na agano la kale lenye vitabu 39.
NINI KILITOKEA HADI WAKRISTO KWA WAKRISTO WAKAANZA KUTOFAUTINA KWA IDADI YA VITABU VYA AGANO LA KALE?
Mnamo mwaka wa 400AD baada ya kristo,Baba Mtakatifu Damasus I alimwambia Mtakatifu Jerome atafsiri biblia yote yaani Agano la kale lililokuwa limeandikwa kwa Kigiriki na Agano Jipya lililokuwa kwa kiebrania na kigiriki kwenda kwenye lugha moja,lugha iliyokuwa rasmi kwa Waroma,lugha ya Kilatini.Lugha hii pia ndio iliyokua lugha ya kufundishia wa wakristo wakatoliki.
Mtakatifu Jerome alitumia tafsiri ya Septuaginta na alitafsiri vitabu vyote pamoja na agano jipya kwa lugha ya kilatini na kuunda Biblia ya Kwanza yenye jumla ya vitabu 73.Ikumbukwe kwa miaka ya nyuma kabla ya Mtakatifu Jerome kutafsiri,hakukuwahi kuwa na biblia yenye mjumuisho wa agano la kale na agano jipya.Ilikuwa kazi kubwa sana na iliyotukuka aliyoifanya Mungu kupitia mt.Jerome
Biblia hii ilitumika kwa muda mrefu sana kwa wakristo wote,haikubadilika kwa muda wa karne 15 sawa na miaka 1500,yaani kwa kipindi chote hichi cha karne 15 wakristo wote walikuwa wanatumia biblia yenye vitabu 73.
Ikumbukwe kuwa Judaism au Wayahudi ile sio dini ya kikristo wale wanaamini katika Torati ya Musa na Manabii tu.Hawaamini katika Yesu Kristo kwa kifupi biblia yao haina Agano Jipya.
Hivyo kwa karne zote hizo 15 wale wote waliokuwa wanaamini katika kristo walitumia biblia moja yenye vitabu 73,iliyotafsiriwa na Makatifu Jerome kwa kibali cha Papa Damasus wa kwanza.
Mambo yalikuja kubadilika pale yalipotokea mageuzi yaliyozaa Uprotestanti (Protestanti Reformation). Ilikuwaje,ilikuwa hivi!
Padri mkatoliki wa Shirika la Waagustino,Msomi na mwanatheologia Martin Luther aliona kwamba wayahudi wana idadi ndogo ya vitabu vya agano la kale 39,kuliko vile 46 vya wakatoliki.
Na kwa kuzingatia kwamba baadhi ya makosa na kashfa zilizokuwa zikiliandama kanisa mwishoni mwa zama za kati za kanisa (Late Medieval Church) zilitokana na baadhi ya mafundisho ambayo msingi wake ulikuwa ni baadhi ya vitabu vya Deuterocanonical hususan kitabu cha WAMAKABAYO kuhusu fundisho la kikatoliki la TOHARANI na KUOMBEA WAFU (Pugatory) ambapo fundisho hili msingi wake ni 2Wamakabayo 12:38-45.
Pia kutokana na kashfa ya uuzaji wa vibali vya msamaha wa dhambi na toharani (indulgences),mambo haya yalimfanya Luther ashindwe kuvumilia na aliondoka vitabu vyote vilivyokuwa vina unga mkono fundisho kuhusu kuombea wafu na toharani.
Martin Luther alipendezwa zaidi ya na vitabu vya kiyahudi (Palestinian Canon) vilivyokuwa na idadi ya vitabu 39 vya agano la kale.Hivyo alitafsiri biblia nyingine kwa kijerumani yenya jumla ya vitabu 66 pamoja na vile vya agano jipya.Tafsiri hii haikuwa na vile vitabu 7 vyenye asili ya kigiriki yaani Deuterocanonical. Biblia hii haikujumuisha vitabu vya Makabayo,Judith, Tobiti, Baruku,Hekima ya Suleimani na Sira.
Martin Luther baada ya kuondoa kitabu cha Makabayo kilichokuwa na fundisho kuhusu kuombea wafu alitumaini kuwa zile kashfa na makosa yangeondoka.Kanisa lilifanyia kazi baadhi ya madai yake yaliyokuwa na tija,lakini luther aliendela kuleta msuguano ndani ya kanisa,Kanisa halikuweza kumvumilia,likamtenga mwishowe aliamua kuanzisha dhehebu lake la Ulutheri ambalo wanatumia biblia hiyo ya mwanzilishi wao.
Kwa upande wa wakatoliki,baada ya mtaguso wa Trent,1546 waliamua kuendelea kutumia vitabu saba vya Deuterocanonical yaani Makabayo,Judith,Tobiti,Baruku,Hekima ya Suleimani na Sira.
Kwanini waliamua kuendelea kuvitumia?
Kwa sababu kwa kipindi chote hicho cha karne 15 zilizopita kuanzia wakristo wa kwanza kabisa chini ya Mitume wa Yesu walivitambua vitabu hivi na kuvitumia.Hata wale waliokuwa kabla ya Kristo na wakati wa kristo walikuwa wakivitumia vitabu hivi.
Na ndio orodha ile ile ya vitabu iliyokuwa ikitumika kabla ya kristo,wakati wa kristo na baada ya kristo na ndio iliyokuja kutafsiriwa na Mtakatifu Jerome na kutenganeza biblia ya kwanza iliyoendelea kutumika hadi pale Martin Luther alipokuja kufanya mabadiliko ambayo hayatambuliwi na kanisa Katoliki.
HITIMISHO
Tokea Karne ya 16 katika kipindi cha Mageuzi,kumekuwa na aina mbili za biblia
•Biblia ya Wakatoliki
•Biblia ya Waprotestanti (Walokole)
Ambazo kwa Asilimia 99 zinafanana kwa mpangilio na maneno isipokuwa kwa vile vitabu saba tu ambavyo vipo kwenye biblia za wakatoliki tu.
Baadhi ya madhehebu mengine wanavitambua hivyo vitabu na wanaviweka kwenye orodha ya Vitabu wanavyoviita Apocrypha ambapo vinakuwa mwishoni kabisa mwa Agano la kale.
Kwa sisi wakatoliki vitabu hivi vipo kwenye orodha inayoitwa Deuterocanonical.
Biblia zote za wakatoliki na waprotestani,walokole,wasabato n.k zinaanzia na kitabu cha Mwanzo (Genesis) na kumalizia kitabu cha Ufunuo (Revelation).Vyote vina injili nne,Mathayo,Marko,Luka na Yohane.
Tofauti ipo tu kwenye vile vitabu saba vya deuterocanonical vya agano la kale,ambapo wakatoliki ndio tunavyo tu na walokole hawana.
USHAURI KWA MKATOLIKI WAKATI UNAPOTAKA NUNUA BIBLIA
Mkatoliki unapoenda kununua biblia hakikisha biblia hiyo ina jumla ya vitabu 73 yaani Agano la kale 46 na Agano jipya 27.Kisha nenda kwa padre aibariki kabla hujaanza kuitumia
Ubarikiwe Sana
Didas Tumaini
0712778881
Like na share www.fb.com/viwawa.rulenge/