29/08/2026
◄ UNA NEEMA ALIYONAYO YESU ►
- Warumi 4:16 16
Kwa sababu hiyo, ahadi hiyo inatokana na imani ili iwe kwa njia ya neema, ili ahadi hiyo iwe na hakika kwa uzao wote; si kwa wale tu walio wa sheria, bali pia kwa wale walio na imani ya Ibrahimu, ambaye ni baba yetu sote...
Unayo thamani kubwa sana mbele za Mungu, fikiria Mungu kumtoa mwanaye pekee kufa kwa ajili ya mtu k**a wewe.
- HII NI THAMANI YA NAMNA GANI?
- JE! NI UPENDO MKUU NAMNA GANI?
Mungu ni pendo na anadhihirisha kwa vitendo. Na tunapoyajua haya, tunaona kuwa Neema ya Mungu ni kibali ambacho hatukustahili, hatukukitolea jasho, wala hatukukipata kwa sababu ya matendo yetu.
Na kwa kuwa hatukustahili wala kukitolea jasho, sote tunastahilishwa kukipokea kwa neema tu.
# Lakini tunaiishije neema hiyo?
K**a unavyoweza kutumia password _(nenosiri)_ likakupa ruhusa ya kutumia programu ya kompyuta, imani nayo ni password inayotuwezesha kuishi katika neema ya Mungu ambayo hatukustahili.
Imani haina uhusiano wowote na yale tunayofanya au tunayoweza kufanya, bali Imani ni kuamini tu na kutangaza yale ambayo Mungu amefanya na atakayofanya kwa ajili yetu.
Tunapoamini kuwa kibali cha Mungu kiko juu yetu kwa sababu ya kazi aliyoimaliza Kristo, ahadi Zake zote zinakuwa na hakika kwetu, maana sisi ni uzao wake Ibrahimu. Hivyo tunayo "imani ya Ibrahimu".
Muangalie Ruthu alikuwa mjane wa Mataifa ambaye aliweka imani yake katika neema ya Mungu. Aliamini kwamba kibali cha Mungu kingemwongoza kwenye shamba sahihi la kuokota masazo ya mavuno, ambapo angepata kibali machoni pa mwenye shamba. (Ruthu 2:2)
Kwa sababu Ruthu alimtegemea Mungu, hakumweka tu katika shamba la Boazi tajiri, bali pia alimuingiza katika ukoo wa Yesu! (Mathayo 1:5)
Imani ya Ruthu ilimfungulia ulimwengu mpya kabisa. Alitoka katika umaskini kwenda kwenye utajiri, kutoka katika ujane kwenda kwenye ndoa, na kutoka kutokuwa na watoto hadi kuwa na familia kamili. Pia alikuja kuwa mtu anayeheshimika katika jamii. (Ruthu 4:13-15)
Ikiwa Ruthu, mtu wa Mataifa aliyekuwa chini ya agano la kale, alimtegemea Mungu, na kwa imani akapokea kibali, je! Sisi tulio chini ya agano jipya la neema tutafurahia zaidi kiasi gani baraka zinazoletwa na neema ya Mungu ambayo hatukustahili!
Mungu anatuona ndani ya Yule Apendwaye (Yesu) leo, tunafurahia kibali kilekile ambacho Yesu anacho!
- Waefeso 1:5-6
> Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake. Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa.>
Rafiki yangu, unapoamini kuwa una kibali kilekile alicho nacho Yesu, ulimwengu mpya utafunguka mbele yako, ulimwengu ambamo ahadi zote za Mungu ni " Ndiyo" na "Amina" ndani ya Kristo!
Unapoamini kuwa kibali cha Mungu kiko juu yako kwa sababu ya kazi aliyoikamilisha Kristo, ahadi Zake zote zinakuwa hakika kwako.