24/05/2026
■ INJILI MITAANI, JUMAMOSI 23.5.2026 - KANISA LA FGBF DAR-ES-SALAAM
■ KUHUBIRI INJILI MITAANI, KATIKA MITAA NA VICHOCHORO VYA JIJI LA DAR-ES-SALAAM, TANZANIA
■ NI INJILI YA MTU KWA MTU, NYUMBA KWA NYUMBA, NA VICHOCHORO VYAKE; NA KWA KILA KUNDI LA WATU (MATENDO YA MITUME 20:20, 26-27)
■ JUMLA YA IDADI YA WATU WAZIMA WALIOOKOKA SIKU HIYO: 1385
■ NI KAZI YA MUNGU, ILIYOFANYWA NA WASHIRIKA WA KANISA LA FGBF DAR-ES-SALAAM, JUMAMOSI YA UINJILISTI; 23.5.2026
■ Mahali lilipo Kanisa katika Jiji la Dar-Es-Salaam, Tanzania:
BARABARA YA SAM NUJOMA, MWENGE; MKABALA NA MLIMANI CITY
Hizi, ni picha zinazowaonyesha baadhi ya Washirika; ambao ni miongoni mwa mamia ya Washirika wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Dar-Es-Salaam; lililoko Barabara ya Sam Nujoma, Mwenge; waliokuwa wakihubiri Injili Mitaani; mtu kwa mtu, nyumba kwa nyumba, na vichochoro vyake; na kwa kila kundi la watu; katika pembe zote za Jiji la Dar-Es-Salaam, na viunga vyake; Siku ya Jumamosi, tarehe 23.5.2026. Wakati unapozitazama picha hizi, ZINGATIA PIA, UJUMBE UFUATAO, KUTOKA KWA ASKOFU MKUU ZACHARY KAKOBE:
"Ndugu yangu mpendwa, jambo la kuzingatia, ni kwamba; picha hizi, siyo picha za tukio spesheli au mahususi, lililopangwa na kuandaliwa maalum, linalotokea kwa nadra; bali ni shughuli au hali ya utendaji wa kawaida, katika maisha ya Washirika wengi wa Kanisa la FGBF Dar-Es-Salaam. Kwa miaka mingi sasa, kuhubiri Injili mitaani, imekuwa ni sehemu ya maisha ya Washirika wengi wa Kanisa la FGBF Dar-Es-Salaam. Ukiacha Jumamosi kadhaa kila mwezi, zinazoitwa "JUMAMOSI ZA UINJILISTI"; ambapo Washirika wote huingia mitaani kushuhudia au kuhubiri Injili, katika maeneo mbalimbali ya Zoni zao; vilevile, Washirika katika Seksheni, na Makanisa ya Nyumbani, kadha wa kadha; hupanga mikakati yao wenyewe, na kuwa na siku tofauti tofauti, katika wiki, za kufanya kazi hii; achilia mbali makundi ya Washirika wachache wachache, ambao huhubiri Injili, takriban kila siku. Na zaidi sana, Washirika wengi binafsi hutumia kila fursa wanayoipata kila siku, kuhubiri Injili; iwe ni katika daladala, au mahali pengine popote. Kila Mshirika katika Kanisa hili, ni wajibu wake kuihubiri kila mahali; Habari Njema ya MWOKOZI WA ULIMWENGU, YESU KRISTO (1 YOHANA 4:14; YOHANA 4:42)."
"Kazi hii ya Kuhubiri Injili, siyo kazi ya Askofu au Mchungaji fulani, PEKE YAKE; wala siyo kazi ya Mwinjilisti au Mhubiri fulani "Mkubwa" wa Kimataifa, peke yake! NI KAZI INAYOPASWA KUFANYWA NA KILA MTU ALIYEOKOKA, awe ni mwanamume au mwanamke (MATENDO YA MITUME 2:18, 21); au ameokoka zamani, au ameokoka hivi karibuni (YOHANA 1:40-42; 4:5-30, 39-42). Hivi ndivyo ilivyokuwa Nyakati za Kanisa la Kwanza. Sauli aliposababisha adha kuu ya Kanisa la Kwanza, WASHIRIKA WOTE (wanaume pamoja na wanawake); walitawanyika na kwenda huko na huko, KULIHUBIRI NENO. Biblia inatupa simulizi hii, katika MATENDO YA MITUME 8:1, 3-4, "Siku ile kukatukia adha kuu ya Kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; WOTE WAKATAWANYIKA katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume. Sauli akaliharibu Kanisa, akaingia kila nyumba, na kuwaburuta WANAUME NA WANAWAKE na kuwatupa gerezani. Lakini WALE WALIOTAWANYIKA (wangapi? Wote!) WAKAENDA HUKO NA HUKO WAKILIHUBIRI NENO." Unaweza kuona! Mitume, wao hawakwenda; bali WASHIRIKA WOTE, WANAUME KWA WANAWAKE walikwenda; kwa kuogopa kuburutwa na Sauli, na kupelekwa gerezani. Na kule walikokwenda, WOTE wakalihubiri Neno, wote wakaihubiri Injili."
"Hapo awali, Yesu Kristo alikuwa amewapa Washirika hao, Agizo Kuu, ambalo linatuhusu sisi pia; la kwenda kuhubiri Injili kwa kila kiumbe (MARKO 16:15); na baadaye Yesu akawaambia wakawe mashahidi wake Uyahudi wote na Samaria (MATENDO YA MITUME 1:8); lakini hawakutii maagizo hayo, bali waliendelea tu kujibariki na kujiburudisha wenyewe Kanisani, kwa mapambio; k**a wengi wetu tunavyofanya; mpaka pale Sauli alipoanza kuingia nyumba kwa nyumba, na kuwaburuta gerezani; NDIPO wakalazimika kwenda kuhubiri Injili Uyahudi na Samaria!! Je, na ninyi katika Kanisa lenu, au na wewe binafsi, unasubiri mpaka Mungu amwachie Sauli awaletee, au akuletee adha kuu, ndipo ulazimike kwenda kuhubiri huko na huko? SAA YA KUAMKA KATIKA USINGIZI IMEKWISHA KUWADIA! (WARUMI 13:11-12). Habari Njema ya Ufalme wa Mungu, itahubiriwa katika Ulimwengu wote, KUWA USHUHUDA KWA MATAIFA YOTE; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja (MATHAYO 24:14)."
"Ndugu yangu, uliyeokoka; bila kujali kwamba, WEWE ni Mshirika wa Kanisa gani; kumbuka kwamba, NI OLE WAKO USIPOIHUBIRI INJILI (1 WAKORINTHO 9:16-17). Usingojee mpaka Mungu amlete Sauli kukushurutisha, kufanya hivyo! Wala usitoe udhuru kwamba, wewe bado mchanga kiroho; hujajua sana Neno la Mungu. KILA AMWAMINIYE YESU, MWANA WA MUNGU; ANAO HUO USHUHUDA NDANI YAKE (1 YOHANA 5:10). Ndani yako kuna ushuhuda, utumie ushuhuda huo, katika kuwashuhudia au kuwahubiria Injili, watu wengine. Ushuhuda wako ni upi? Ni Neno lile ulilolipokea, ambalo lilikufanya ukate shauri kuokoka. Nenda mitaani, ukalitumie Neno hilohilo kuwahubiria watu wengine. Anzia hapo!! (YOHANA 1:35-46)."
"Aidha, wako watu wengine wanaosema kwamba wamejazwa Nguvu ya Roho Mtakatifu, na wananena kwa lugha (MATENDO YA MITUME 1:8; 2:4). Ni vema, na ni vizuri sana! Hata hivyo, kinachoshangaza, ni kwamba; baadhi ya watu hawa, wanaosema wamejazwa Nguvu ya Roho Mtakatifu; tangu "wajazwe Nguvu hiyo", siyo tu kwamba, hawajamleta hata mtu mmoja kwa Yesu; bali pia, hawana ujasiri wowote kabisa wa kumhubiria Injili, mtu hata mmoja! Wamejaa aibu na woga! K**a wewe ni mtu wa jinsi hii, niruhusu kukuuliza, "Wewe kweli umempokea Roho Mtakatifu, VILEVILE k**a Mitume wa Kanisa la Kwanza (MATENDO YA MITUME 10:44-47)? Kimsingi, Nguvu ya Roho Mtakatifu, au Uwezo utokao juu; ni Uwezo unaomwezesha mtu kuwahubiria watu juu ya makosa na dhambi zao; na toba na ondoleo la dhambi hizo; kwa ufanisi na tija kubwa (LUKA 24:47,49). Biblia inasema katika MIKA 3:8, "Bali mimi NIMEJAA NGUVU KWA ROHO YA BWANA; NIMEJAA hukumu na UWEZO; NIMHUBIRI YAKOBO KOSA LAKE; NA ISRAELI DHAMBI YAKE."
"Nguvu ya Roho Mtakatifu, inamfanya mtu, kulinena Neno la Mungu, kwa ujasiri wa kipekee (MATENDO 4:31). Wanafunzi wa Yesu waliokuwa waoga kuishindania Imani (MATHAYO 26:56; 69-75); baada ya kujaa Nguvu ya Roho Mtakatifu, walibadilishwa, na kuwa na ujasiri wa ajabu (MATENDO YA MITUME 4:13; 18-20). Walisema, "MAANA SISI HATUWEZI KUACHA KUYANENA MAMBO TULIYOYAONA NA KUYASIKIA (MATENDO YA MITUME 4:20). Ni kwa nini walikuwa hawawezi kuacha kumhubiri Yesu? Kujazwa Nguvu ya Roho Mtakatifu, kunaitwa pia, kubatizwa kwa Roho Mtakatifu na KWA MOTO (MATHAYO 3:11). Mtu akibatizwa kwa moto huo wa Roho Mtakatifu, moto huo uwakao ndani yake; unamfanya mtu huyo kushindwa kujizuia kumhubiri Yesu! (YEREMIA 20:9)."
"Siyo hilo tu, bali pia, mtu aliyebatizwa kwa moto wa Roho Mtakatifu, anapohubiri, maneno yake yanakuwa moto! (YEREMIA 5:14; 23:29). Mtu huyu, anapomshuhudia mtu, au kumhubiri Injili; Roho Mtakatifu, ambaye ni Mungu, Aliye Moto Ulao (WAEBRANIA 12:29); Yeye naye, wakati huohuo; humshuhudia mtu huyo. Mhubiri huyo hushuhudia, na vilevile; Roho Mtakatifu, Naye; hushuhudia PAMOJA NA MHUBIRI HUYO (YOHANA 15:26-27). Roho Mtakatifu humwongoza mtu anayehubiriwa, na kumtia katika Kweli yote; kwa kumhakikishia kwamba, yeye ni mwenye dhambi, na kwamba, hukumu nzito ya milele itamkabili, asipoyatilia maanani, maneno ya haki; anayoambiwa na Mhubiri huyo (YOHANA 16:8, 13). Ni kwa ajili hii sasa, ndiyo maana; mahubiri ya mtu aliyejaa Nguvu ya Roho Mtakatifu, huwa na tija kubwa. Sasa nikuulize tena, Je, umempokea Roho Mtakatifu VILEVILE walivyompokea Mitume? K**a, Jibu lako ni Ndiyo; basi amka, Ewe Shujaa uliyelala usingizi (YONA 1:6); nenda mitaani, ukamhubiri Yesu Kristo; ya kwamba, Anakuja upesi, wala hatakawia!! (WAEBRANIA 10:37; UFUNUO WA YOHANA 22:12)."
"Ndugu yangu mpendwa; ninakuambia tena kwa msisitizo! Uwe na huruma kwa wenye dhambi, walioko mitaani, ambao wanaangamia; au siyo ni OLE WAKO; damu ya watu hao itatakwa mkononi mwako; hukumu itakukabili (EZEKIELI 3:18-19). HUKUMU HAINA HURUMA KWAKE YEYE ASIYEONA HURUMA (YAKOBO 2:13). Kila mtu anayekwenda kuwahubiria Injili, watu walioko huko mitaani; katika ulimwengu wa roho, huko mitaani; anakwenda kuwaokoa watu hao, kwa KUWANYAKUA KATIKA MOTO. Katika YUDA 1:22-23, tunasoma, "WAHURUMIENI .... WAOKOENI KWA KUWANYAKUA KATIKA MOTO ...." Ni kwa nini, wenye dhambi hao wanatajwa wako katika moto? Sababu ni kwamba, Neno la Yesu Kristo mwenyewe, linasema katika YOHANA 3:18, ".... ASIYEAMINI AMEKWISHA KUHUKUMIWA ..." Unaweza kuona! Kimsingi, wasioamini, wamekwisha kupewa hukumu ya kutupwa katika moto wa milele! (UFUNUO WA YOHANA 21:8; MATHAYO 25:41). Hivyo, ukiwapelekea Injili, Mwokozi Yesu Kristo anayefanya kazi pamoja na sisi wahubiri katika kuokoa (1 WAKORINTHO 3:9; WARUMI 10:13-14); anakutumia WEWE, kuwanyakua wenye dhambi hao, katika hukumu ya moto wa milele! Uwe na huruma! Yeye asiyewahurumia wenye dhambi hao, na kuchukua hatua ya kwenda kuwanyakua katika moto, kwa kwenda kuwahubiria Injili; tunaweza kumfananisha na dereva wa gari la zimamoto lenye vifaa vyote vya uokoaji; anayejistarehesha kwa kunywa soda, na kula nyama choma, mahali fulani; bila huruma wala kujali, huku akiwa ameliegesha gari hilo, hapo alipo; ambapo siyo mbali na nyumba inayoungua moto, ambamo ndani ya nyumba hiyo, kuna watu wa familia kadha, walioshindwa kutoka kwenye nyumba hiyo!! WEWE SASA, NDIYE DEREVA HUYO!! Mwenye masikio, na asikie (MATHAYO 11:15)."
"Nimalize kwa kusema kuwa, inakupasa kufahamu pia kwamba, ziko nchi kadha duniani, ambazo, kumhubiria Injili mtu yeyote aliyeko mahali popote; ni kosa la jinai, ambalo hukumu yake ni kutoweshwa duniani. Hata hivyo, wako watu wachache wanaothubutu kuwahubiria Injili watu kadhaa, katika nchi hizo, na kuwa tayari kwa lolote; baada ya kuk**atwa. Ikiwa tumezungukwa na mashahidi wa Yesu, wa viwango hivi (WAEBRANIA 12:1); sisi tulioko Tanzania, au katika nchi nyingine; zilizo na uhuru wa kuhubiri Injili hii, kwa mtu yeyote; tutapataje kupona? (WAEBRANIA 2:1-3). TAFAKARI!!! Ni maombi yangu, kwamba, wewe uliyeokoka unapoangalia picha hizi; wewe pia utaumbiwa mzigo wa kwenda mitaani kuhubiri Injili. Umepewa vingi, hivyo BWANA atavitaka vingi kwako! (LUKA 12:47-48). Neema ya Bwana Yesu Kristo na iwe pamoja na roho yako (FILEMONI 1:25)."