25/10/2022
Somo: FUNGA NA KUOMBA UNAPOTAKA KUANZA KITU
Ukisoma katika Biblia yako utauona watumishi wengi wa Mungu walivyokuwa wanafanya kabla ya kuanzisha kitu chochote.
Mfano:
a) YESU
Tunamuona Yesu kabla ya kuanza kazi ya Mungu hapa duniani alifunga kwa siku 40 mchana na usiku.
"Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa."
Mathayo 4:2
Alifanya hivi ili kupata muda wa kutosha wa faragha na Baba kabla ya kuanza kazi yake hapa duniani.
Hii ilikuwa kwa ajili ya safari yake yote ya huduma. Kwa hiyo huduma yake yote alimkabidhi Baba kabla ya kuanza. Na hii ilimsaidia kumaliza salama kazi yake hapa duniani.
Hapa kuna kitu cha kujifunza. Kabla ya kuanza kitu chochote katika maisha yako chukua muda anza na Bwana kwanza.
Kabla hujaanza biashara, chukua muda wako funga na kuomba. Kabla hujaanza kazi, chukua muda funga na kuomba. Kabla hujaanza mwaka au mwezi chukua muda wako funga na kuomba. Mkabidhi Bwana kila kitu chako na utaona mkono wa Bwana katika maisha yako.
"Umkabidhi Bwana njia yako, Pia umtumaini, naye atafanya."
Zaburi 37:5
b) ESTA
Huyu Esta kabla ya kwenda kwa Mfalme kinyume cha utaratibu alihitaji maombi ya kufunga na kuomba ili aweze kupata mpenyo na kibali kwa Mfalme.
"Basi Esta akawatuma ili wamjibu Mordekai, Uende ukawakusanye Wayahudi wote waliopo hapa Shushani, MKAFUNGE KWA AJILI YANGU; msile wala kunywa muda wa siku tatu, usiku wala mchana, nami na wajakazi wangu TUTAFUNGA VILE VILE; kisha nitaingia kwa mfalme, kinyume cha sheria; nami nikiangamia, na niangamie."
Esta 4:15-16
Baada ya maombi haya waliyoomba, Esta alipata kibali na mpenyo(Esta 5) kwa Mfalme. Ooonh! Tazama nguvu ya maombi ya kufunga na kuomba.
Esta alifahamu nguvu ya maombi ya kufunga. Ndio maana aliita watu wafunge na kuomba kwa ajili yake na yeye mwenyewe akafunga.
Kabla hujaenda kwenye interview yako, funga na kuomba. Kabla hujaingia kwenye ndoa, funga na kuomba. Kabla hujaenda kupambania tenda ya biashara, funga na kuomba. Kuna nguvu katika kuomba.
Ubarikiwe sana.
Innocent Morris
+255652796450 (WhatsApp)
Usikose maombi ya kufunga na kuomba kuanzia tarehe 1 mpaka 7 mwezi wa 11 na kila siku ya mfungo tutakuwa live katika YouTube channel yetu ya Holy Spirit Conneo