Mkatoliki Imara

Mkatoliki Imara Tumsifu Yesu Kristo. Mpendwa Mkristo Mkatoliki,Karibu Sana Katika Page Hii Ya MKATOLIKI IMARA.

🙏🙏

23/05/2026

MASOMO YA MISA, MEI 23, 2026

JUMAMOSI, JUMA LA 7 LA PASAKA

SOMO 1
Mdo. 28 :16-20, 30-31

Tulipoingia Rumi Paulo alipewa ruhusa kukaa kwake mwenyewe pamoja na askari aliyemlinda.
Ikawa baada ya siku tatu akawaita wakuu wa Wayahudi wakutane; hata walipokutanika akawaambia, Ndugu zangu, ingawa sikufanya neno kinyume cha watu wetu wala neno lililopingamana na desturi za baba zetu, nalitiwa katika mikono ya Warumi, hali nimefungwa, tokea Yerusalemu. Na hao walipokwisha kuniuliza-uliza walitaka kunifungua, kwa maana hapakuwa na sababu yo yote kwangu ya kuuawa. Lakini Wayahudi walipotoa hoja juu ya shauri hili nalishurutishwa kutaka rufani kwa Kaisari. Si kwamba nalikuwa na neno la kuwash*taki watu wa taifa langu. Basi kwa ajili ya hayo, nimewaita mje kunitazama na kusema nami; kwa maana nimefungwa kwa mnyororo huu kwa ajili ya tumaini la Israeli.

Akakaa muda wa miaka miwlli mizima katika nyumba yake aliyokuwa ameipanga, akawakaribi sha watu wote waliokuwa wakimwendea, akihubiri habari za ufalme wa Mungu, na kuyafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri mwingi, asikatazwe na mtu.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 11 :4-5, 7 (K) 7

(K) Wanyofu wa moyo wauona uso wake, Ee Bwana. au: Aleluya.

Bwana yu katika hekalu lake takatifu.
Bwana ambaye kiti chake kiko mbinguni,
Macho yake yanaangalia;
Kope zake zinawajaribu wanadamu. (K)

Bwana humjaribu mwenye haki;
Bali nafsi yake humchukia asiye haki,
Na mwenye kupenda udhalimu. (K)

Kwa kuwa Bwana ndiye mwenye haki,
Apenda matendo ya haki,
Wanyofu wa moyo watamwona uso wake. (K)

SHANGILIO
Mt. 28 :19-20

Aleluya, aleluya,
Enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi. Mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, Hata ukamilifu wa dahari.
Aleluya.

INJILI
Yn. 21:20-25

Petro aligeuka akamwona yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu anafuata; (ndiye huyo aliyeegama kifuani pake wakati wa kula chakula cha jioni, akasema, Bwana, ni nani akusalitiye?). Basi Petro akamwona huyo, akamwambia Yesu, Bwana, na huyu je? Yesu akamwambia, Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe? Wewe unifuate mimi.

Basi neno hilo lilienea katikati ya ndugu ya kwamba mwanafunzi yule hafi. Walakini Yesu hakumwambia ya kwamba hafi; bali, Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe? Huyu ndiye yule mwanafunzi ayashuhudiaye haya, na aliyeyaandika haya; nasi twajua ya kuwa ushuhuda wake ni kweli. Kuna na mambo mengine mengi aliyoyafanya Yesu; ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa.

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.

*TAFAKARI*

Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Bado tupo katika kipindi cha novena na leo ni siku ya mwisho, siku ya tisa, siku ya neema. Siku ya kujiandaa kwa kumpokea Roho Mtakatifu kwa siku ya Pentekoste. Na leo tafakari ya neno la Mungu tukianza kwa kuiangalia injili yetu, injili yetu inatuongoza tutakayosoma leo inafunga sehemu ya injili ya kitabu cha Yohane kuashiria kwamba kipindi cha pasaka, na habari za Kristo baada ya kufufuka basi ndio zinafikia ukingoni. Hata kwenye somo letu la kwanza leo, sehemu ya kitabu cha matendo ya mitume tutakayosoma ni sehemu inayofunga hiki kitabu; yote haya ni kuonesha kwamba kipindi cha pasaka ndio tunakifunga kifunga. Habari za Kristo mfufuka zimeweza kuenea kwa watu hao wote kwa nguvu na uwezo wa Roho Mtakatifu. Wengi wameamini na mitume wamekazana kwa namna ya ajabu na hivyo ni juu yetu kuiga mfano wao hasa katika suala la kukazana kuipenda kazi ya Bwana. Hili ndilo lililo la muhimu.

Sasa katika injili yetu ya leo, Petro anaulizia hatma ya yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu. Yeye jana aliambiwa hatma yake kwamba watatokea watu watakaomfunga na kumpeleka asikopenda akimaanisha atakufa kifo gani na kweli Petro alikufa kifo dini. Petro aliposikia kwamba Yesu amemtabiria hatma yenye ugumu namna hiyo, basi alitaka kujua hatma ya yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu. Sababu za kufanya hivi labda yawezekana kwamba Petro aliona kwamba Yesu amemtabiria mwisho mgumu sana-hivyo yawezekana kwamba Petro alijiona kana kwamba Yesu anampatia adhabu kutokana na lile kosa lake la kumsaliti; hivyo alitaka kuulizia na mwisho wa yule anayempenda ili aweze kupima mwisho wake na yeye ili mwishowe alinganishe. Lakini Yesu anamwambia Petro hiyo sio juu yako; ni juu yangu mimi.

Ndugu zangu, Petro alikuwa miongoni mwa wanafunzi wenye umri mkubwa kuliko wale wengine. Pia alichaguliwa kuwa kiongozi wa wengine. Uongozi ni utumishi na majitoleo na sio ubosi. Hivyo k**a kiongozi ilimbidi awe wa kwanza kuwaonesha wenzake njia, afuate ile njia ya Bwana wake. Hii haikuwa adhabu bali ulikuwa ni upendo mkubwa kwa Petro na kwa njia ya uhodari wake, aliweza kuwatia moyo mitume wengine. Somo hili ndugu zangu litupatie matumaini hasa kwa baadhi yetu tulio viongozi, wazazi au wenye wadogo wanaotegemea uongozi toka kwao. Lazima tuwe mstari wa mbele katika kuliongoza hili kundi na tusiwe wa kukata tamaa kwani tutaliangusha kundi lote. Mara nyingi mtoto wa kwanza ndiye anayepataga shida kuliko wenzake. Mtoto huyu anapofaulu kuwa hodari na kuwaongoza wenzake, mwishowe huiletea familia maendeleo makubwa.
Hivyo basi kila mmoja wetu anaalikwa kuwa Petro mahali pale anapoishi. Tuoneshe mfano, tuwe sababu za kuwatia moyo wenzetu ili wasirudi nyuma au kukata tamaa.

Paulo katika somo la kwanza anatupatia mfano wa askari bora aliyepambana hadi mwisho bila kuogopa ugumu wowote. Huku kupambana kwake kuliwasaidia sana wale wakristo wa makanisa aliyoanzisha waweze kusonga mbele. Wao walipomuona Paulo akivumilia yote hayo, nao walikuwa na moyo wa kupambana hivi hivi, nao hawakuogopa kifungo wakawa mstari wa mbele kuihubiri injili. Nasi tuepukane na ile hali ya kuwa watu wakata tamaa; mkata tamaa huwarudisha wenzake nyuma na kuifanya jamii yote ianguke. Tuepukane na hali hii.

Usisahau KU-LIKE na KU-SHARE page hii ya Mkatoliki Imara
©️ Pd. Prosper Kessy OFMCap.

15/05/2026

Masomo ya Misa jumamosi

(Jumamosi, Mei 16, 2026)

Somo la kwanza
Mdo 18:23-28

Paulo, akiisha kukaa Antiokia siku kadha wa kadha aliondoka, akapita kati ya nchi ya Galatia na Frigia, mji kwa mji, akiwathibitisha wanafunzi. Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzaliwa wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohane tu. Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi. Na alipotaka kuvuka bahari aende mpaka Akaya, ndugu wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe; naye alipofika akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu. Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.

Wimbo wa Katikati
Zab 47: 1-2, 7-9

Enyi watu wote, pigeni makofi,
Mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe,
Kwa kuwa Bwana Aliye juu, mwenye kuogofya,
Ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote.
(K) Mungu ndiye mfalme wa dunia yote.
Au: Aleluya.

Maana Mungu ndiye mfalme wa dunia yote,
Imbeni kwa akili.
Mungu awamiliki mataifa,
Mungu ameketi katika kiti chake kitakatifu.
(K) Mungu ndiye mfalme wa dunia yote.
Au: Aleluya.

Wakuu wa watu wamekusanyika,
Wawe watu wa Mungu wa Ibrahimu.
Maana ngao za dunia zina Mungu,
Ametukuka sana.
(K) Mungu ndiye mfalme wa dunia yote.
Au: Aleluya.

Shangilio
Yn 10:27

Aleluya, aleluya,
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya.

Injili
Yn 16:23-28

Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu. Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu. Hayo nimesema nanyi kwa mithali; saa yaja ambayo sitasema nanyi tena kwa mithali; lakini nitawapa waziwazi habari ya Baba. Na siku ile mtaomba kwa jina langu; wala siwaambii ya kwamba mimi nitawaombea kwa Baba; kwa maana Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na kusadiki ya kwamba mimi nalitoka kwa Baba. Nalitoka kwa Baba, nami nimekuja hapa ulimwenguni; tena nauacha ulimwengu; na kwenda kwa Baba.

***********************************

TAFAKARI

KUELEWA NENO LA MUNGU.

Katika somo la kwanza kutoka katika kitabu cha matendo ya Mitume, kina muongelea mtu mmoja ambaye anaitwa Apollo ambaye ni mfano kwa wakristo wote. Alifahamu maandiko na alikuwa na ujasiri wa kuhubiri habari njema. Alifanya watu wengi wabadilishe maisha yao na kuongoka, kwa kutangaza Neno la Mungu. Sio wote walio na uweze wa kufafanua Neno la Mungu. Tunahitaji msaada wa Mungu na uongozi wa Roho Mtakatifu. Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo umefungua milango ya neema. Tunaweza kuomba kwa Mungu kwa jina la Kristo na nguvu ya Roho Mtakatifu.

Maandiko Matakatifu, na hasa mafundisho ya Kristo yapo katika lugha ambayo imefunikwa kiasi kikubwa, ambayo sio wote waweza kuelewa. Kwahiyo kwanini Yesu anaongea katika lugha ambayo imefunikwa au kufichwa na asiongee kwa wazi wazi moja kwa moja? Jibu linahusika na sisi ukosefu wetu wa kutokuwa wazi katika ukweli. K**a tunakuwa wazi katika ukweli, na kuwa tayari kukumbatia ukweli bila kujali ni namna ghani, Yesu angeongea nasi na sisi kuitika mara moja. Lakini sivyo ilivyo. Ufunguo wa kuelewa haya ni kuelewa na kutambua elimu ya mapenzi ya Mungu na utayari wa kutimiza mapenzi hayo. Mara nyingi sisi tunataka Yesu atuambie mapenzi yake, tufikirie juu yake, na kuangalia, alafu sisi tunakuja na majibu yetu wenyewe. Lakini k**a tunataka Yesu aongee nasi wazi wazi, tunapaswa kusema ndio kwa Yesu hata bila kutambua anataka tufanye nini. Utayari wa kukubali mapenzi yake ni mwanzo wa kuelewa mapenzi yake.

Mfano kamili wa hili ni Mama yetu Bikira Maria. Kabala ya Malaika kuja kwake yeye alikuwa akiyashika mapenzi ya Mungu. na Malaika alipofika na kumwelezea nini kitacho tokea, yeye aliuliza uelewa zaidi. Na kweli alipata kuelewa zaidi kwa kupata jibu kwa swali lake. Lakini sababu moja ya malaika, k**a mjumbe wa Mungu, aliongea wazi wazi kwasababu alishafahamu wazi moyo wa Maria kuwa unamtegemea Mungu bila kujali kutatokea nini.

Je, unataka Mungu aongee nawe katika hali ya uwazi? Je, unataka kuelewa Neno la Mungu? k**a ndivyo, sema ndio kwa kile ambacho Mungu anapenda wewe utende daima. Kwa kujenga hali hii ya kusema ndio kwa mapenzi ya Mungu, itamfanya Mungu kukufungulia mlango mara moja kuelewa yale yote anayotaka uyatende katika kutimiza mapenzi yake.

Sala:
Bwana, ninachagua mapenzi yako leo na daima. Sichagui kitu kingine ni mapenzi yako tu. Ninavyosema ndio kwako, nisaidie niweze kukuwa katika hali ya uwazi wako unaopenda. Yesu, ninakuamini wewe.
Amina.

10/05/2026

DOMINIKA 6 YA PASAKA MWAKA A WA KANISA

MASOMO, INJILI & MAOMBI

ANTIFONA YA KUINGIA: Isa.48:20
Hubirini kwa sauti ya kuimba, tangazeni haya, yatamkeni mpaka mwisho wa dunia, semeni, Bwana amewakomboa watu wake, aleluya!

Utukufu husemwa.

KOLEKTA
Ee Mungu mwenyezi, utufanye tuzisherehekee kwa upendo motomoto siku hizi za furaha tunazoadhimisha kwa heshima ya Bwana mfufuka. Utujalie, ili hayo tunayoyakumbuka katika liturujia tuyazingatie daima kwa matendo. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Mdo.8:5-8,14-17

Filipo alitelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule. Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohane; ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu; kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.66:1-7,16,20 (K)1

1. Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote,
Imbeni utukufu wa jina lake,
Tukuzeni sifa zake.
Mwambieni Mungu,
Matendo yako yatisha k**a nini!

(K) Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote,
Au:
Aleluya!

2. Nchi yote itakusujudia na kukuimbia,
Naam, italiimbia jina lako.
Njoni yatazameni matendo ya Mungu;
Hutisha kwa mambo awatendayo wanadamu. (K)

3. Aligeuza bahari ikawa nchi kavu;
Katika mto walivuka kwa miguu;
Huko ndiko tulikomfurahia.
Atawala kwa uweza wake milele. (K)

4. Njoni, sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu,
Nami nitayatangaza aliyonitendea roho yangu.
Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu,
Wala kuniondolea fadhili zake. (K)

SOMO 2: 1Pet.3:15-18
Ndugu zangu, mwe tayari sikuzote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu. Nanyi mwe na dhamiri njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika Kristo. Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya. Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa.

SHANGILIO: Yn.14:23
Aleluya, aleluya!
Yesu alisema:
Mtu akinipenda, atalishika neno langu;
na Baba yangu atampenda;
nasi tutakuja kwake.
Aleluya!

INJILI: Yn.14:15-21
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu. Bado kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena; bali ninyi mnaniona. Na kwa sababu mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai. Siku ile ninyi mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu. Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.

Tafakari

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Ndugu wapenzi, Yesu alijua kwamba atatutangulia kwenda katika utukufu wa milele. Lakini hakuwa na nia ya kutuacha yatima duniani. Alituahidia msaada.

Tumuendee Bwana Yesu,
1. Bwana Yesu, ulituahidia msaidizi baada ya kuondoka kwako: Utusaidie tumtambue na kumpokea katika Roho Mtakatifu ili atuongoze katika maisha ya kila siku.

2. Roho Mtakatifu anajitokeza kwa namna mbalimbali: Utufungue masikio ya mioyo yetu ili yatambue mvuto Mtakatifu.

3. Roho Mtakatifu anasema kwa kupitia mioyo yetu, utusaidie kwa njia ya Roho huyo kuonesha huruma, upendo na wema kwa wenzetu tunaoishi nao.

4. Roho Mtakatifu anasema katika shida na taabu za wenzetu: Utuamshe kwa Roho wako Mtakatifu tuwasaidie wenye shida mbalimbali.

5. Roho Mtakatifu anadai ushuhuda wetu wa imani: Utuhimize tusiepuke wajibu wetu katika kuishuhudia imani yetu katika maisha yetu ya kila siku.

6. Roho Mtakatifu atatumia wajumbe wa kueneza habari ya Ufalme wako: Uwaimarishe wote walioitwa kutimiza wito wa pekee katika kanisa lako.

Ee Mungu Baba, tunatambua nia yako thabiti ya kutusaidia tusipotee katika njia ya wokovu. Upokee maombi yetu kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU
Ee Bwana, zipae kwako sala zetu pamoja na dhabihu tunayokutolea, ili, tukiisha kutakaswa kwa upendo wako, tuwe tunastahili kuzipokea sakramenti za huruma yako kuu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Yn.14:15-16
Bwana asema: Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele.

SALA BAADA YA KOMUNYO
Ee Mungu mwenyezi wa milele, unayetutengeneza upya kwa uzima wa milele katika ufufuko wa Kristo, uzidishe kwetu tunda la sakramenti ya kipasaka, na ututilie moyoni nguvu ya chakula hiki cha wokovu. Kwa njia ya Kristo bwana wetu.

Usisahau KU-LIKE na KU-SHARE page hii ya Mkatoliki Imara

02/05/2026

DOMINIKA 5 YA PASAKA MWAKA A WA KANISA.

MASOMO, INJILI & MAOMBI

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.98:1-2
Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana Bwana ametenda mambo ya ajabu; machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake, aleluya.

Utukufu husemwa.

KOLEKTA
Ee Mungu mwenyezi wa milele, ulitimize daima fumbo la Pasaka ndani yetu. Na hao uliopenda kuwafanya upya kwa njia ya Ubatizo mtakatifu, uwajalie wazae matunda mengi kwa msaada wa ulinzi wako, na kuzifikia furaha za uzima wa milele. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Krsito Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Mdo.6:1-7
Siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung'uniko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku. Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani. Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno. Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia; ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao. Neno la Mungu likaenea; na hesabu ya wanafunzi ikazidi sana katika Yerusalemu; jamii kubwa ya makuhani wakaitii ile Imani.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.33:1-2,4-5,18-19 (K)22
1. Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki,
Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.
Mshukuruni Bwana kwa kinubi,
Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.

(K) Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi,
K**a vile tulivyokungoja wewe.
au:
Aleluya!

2. Kwa kuwa neno la Bwana lina adili,
Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
Huzipenda haki na hukumu,
Nchi imejaa fadhili za Bwana. (K)

3. Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao,
Wazingojeao fadhili zake.
Yeye huwaponya nafsi zao na mauti,
Na kuwahuisha wakati wa njaa. (K)

SOMO 2: 1Pet.2:4-9
Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima. Ninyi nanyi, k**a mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo. Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko, Tazama, naweka katika Sayuni Jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika. Basi, heshima hii ni kwenu ninyi mnaoamini. Bali kwao wasioamini, Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni. Tena, Jiwe la kujikwaza mguu, na mwamba wa kuangusha. Kwa maana hujikwaza kwa neno lile, wasiliamini, nao waliwekwa kusudi wapate hayo. Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu.

SHANGILIO: Yn.14:6
Aleluya, aleluya!
Yesu alimwambia,
Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima;
mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya!

INJILI: Yn.14:1-12
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; k**a sivyo, ningaliwaambia, maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo. Nami niendako mwaijua njia. Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia? Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. K**a mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba, tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. Filipo akamwambia, Bwana, utuoneshe Baba, yatutosha. Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuoneshe Baba? Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake. Mnisadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! Hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe. Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba.

Tafakari

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Ndugu wapendwa, Yesu aliwaeleza wafuasi wake kwamba atawatangulia kwenda mbinguni ili kuwatayarishia mahali pa kukaa kwa daima katika heri ya kimungu.

Tumuendee Bwana wetu Yesu Kristu,
1. Ee Bwana Yesu, tunakushukuru kwa kufika kwetu ili kutupokea kwenye heri yako. Usichoke kutuangalia tusipotee katika njia ya kukufuata ili kufikia unapokaa wewe.

2. Mtume Tomas alikuuliza habari ya njia hiyo ya kufikia heri. Utusaidie kukutambua wewe k**a njia yetu ya heri ya hapa duniani na huko mbinguni.

3. Wewe una umoja na Baba wa mbinguni. Utusaidie kupokea mafundisho yako na kuyafuata katika maisha yetu ya kila siku.

4. Tukifuata nyayo zako utuangaze kutambua shida za wenzetu na kuwasaidia.

5. Ulitoa ahadi kwamba, wafuasi wataweza kwa neema yako, kutenda makubwa. Utupe ujasiri wa kuendeleza ujumbe wako mbele ya watu na kuwaongoza katika njia yako.

Ee Mungu Baba, Mwana wako alianza kukusanya watu na kuwaongoza katika njia inayowapeleka kwako. Upokee bidii zetu za kushiriki uongozi wake anayeishi na kutawala pamoja nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, daima na milele. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU
Ee Mungu, kwa njia ya mabadilishano matakatifu ya sadaka hii, umetufanya washirika wa umungu wako mkuu na wa pekee. Tunakuomba, utujalie ili, k**a tulivyoujua ukweli wako, hali kadhalika tuweze kuufikia kwa mwenendo stahiki. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Yn.15:1,5
Mimi ndimi mzabibu wa kweli, nanyi ni matawi, asema Bwana; akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana, aleluya.

SALA BAADA YA KOMUNYO
Ee Bwana, tunakuomba kwa wema wako uwe nasi taifa lako. Na sisi ulitulisha mafumbo ya mbinguni, utufanye tuondokane na maisha ya zamani, tuingie katika upya wa uzima. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

Usisahau KU-LIKE na KU-SHARE page hii ya Mkatoliki Imara

26/04/2026

MASOMO YA MISA NA TAFAKARI, APRILI 26, 2026
DOMINIKA YA 4 YA PASAKA

JUMAPILI YA KRISTO MCHUNGAJI MWEMA

MWANZO:
Zab. 33:5 – 6
Nchi imejaa fadhili za Bwana. Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika, aleluya.

SOMO 1
Mdo 2:14a, 36 – 41

Siku ya Pentekoste Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia,
Basi nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyesulibisha kuwa Bwana na Kristo.
Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Krito, mpate kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie. Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi. Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 23:1 – 6 (K) 1

(K) Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu.

Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu huniongoza. (K)

Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza
Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
Sitaogopa mabaya;
Kwa maana Wewe upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (K)

Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe changu kinafurika. (K)

Hakika wema na fadhili zitanifuata
Siku zote za maisha yangu;
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)

SOMO 2
1Pet. 2:20b – 25

Kustahimili, mtendapo mema na kupata mateso, huu ndio wema hasa mbele za Mungu. Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake.
Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake. Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogopfya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki. Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti; ili, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa. Kwa maana mlikuwa mnapotea k**a kondoo; lakini sasa mmemrudia Mchungaji na Mwangalizi war oho zenu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

SHANGILIO
Yn. 10:14

Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi.
Aleluya.

INJILI
Yn. 10:1 – 10

Yesu aliwaambia Wayahudi, Amin, amin, nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika z**i la kondoo, lakini akwea penginepo, huyo ni mwivi naye ni mnyang’anyi. Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo. Bawabu humfungulia huyo, na kondoo humsikia sauti yake; naye huwaita kondoo wake kwa majina yao, na kuwapeleka nje. Naye awatoapo kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake. Mgeni hawatamfuata kabisa, bali watamkimbia; kwa maana hawazijui sauti za wageni.
Mithali hiyo Yesu aliwaambia; lakini wao hawakuelewa na mambo hayo aliyowaambia.
Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo. Wote walionitangulia ni wevi na wanyang’anyi; lakini kondoo hawakuwasikia. Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho. Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

***************************************

TAFAKARI

Kukutana na Mchungaji Mwema

Jumapili ya nne ya Pasaka
inajulikana k**a jumapili ya Mchungaji Mwema. Yesu anatangaza kwamba yeye ni “Mchungaji mwema.” Yesu anatupa sura ya Mchungaji mwema anayewafahamu kondoo wake: anawaita, anawalisha na kuwaongoza. Ni kwa sababu ya hili Kanisa limeipendekeza Jumapili hii kuwa siku ya kuombea miito duniani ili liweze kupata wachungaji wema.

Yesu anaonesha wazi tofauti ya wachungaji. Tofauti anayotoa ni juu ya mchungaji yule anayewafahamu kondoo wake na kuwajali, na wale wanaofuata tu mkumbo bila sadaka ya upendo. Hawa ni wachungaji wenye kutafuta maslahi toka kwa kondoo, huwaumiza kondoo kwa matendo yao mapotofu na kuwaacha wazurure na kuliwa na mbwa mwitu. Yesu alitolea sadaka kamilifu k**a Mchungaji wa kimungu. Alikuwa tayari kutembea nasi katika njia zote-sisi kondoo wake. Alikuwa tayari kutoa sadaka ya kila kitu. Hakutaka mateso, kuonewa na kukataliwa vimuondoe kutoka katika lengo lake la kuwajali na kuwatunza watu wake katika njia kamili. Hili linapaswa lituguse, kutufariji na kutupatia sisi ujasiri na kutambua ni kwa jinsi gani upendo wake ulivyo mkubwa kwetu.

Upendo uliooneshwa na Yesu kwa ajili yetu ulikuwa kamili, tena wakati wa magumu makubwa. Upendo huu ulidhihirisha muunganiko wa kiroho uliopo kati yetu na Yesu Kristo-mchungaji wetu mwema. Upendo huu hutengeneza muunganiko wa kiroho ambao ni imara kuliko matatizo tunayoweza kukutana nayo. Haijalishi ni kitu gani kigumu kinachoweza kuja katika njia zetu, tunapaswa kutambua upendo na msaada usio na kikomo kutoka kwa Mchungaji wetu mwema. Na k**a tunaweza kuona upendo huo kamili kutoka kwa wengine, tunakuwa kweli tumebarikiwa mara mbili.
Katika hali nyingine, Yesu anaongea kuhusu mfano wa mtu mwingine ambaye sio mchungaji mwema, ambaye anaona mbwa mwitu wakija na yeye kukimbia.

Tunapaswa kuona ndani ya mtu huyu, vishawishi vyote ambavyo vyaweza kuja katika maisha yetu. Ni vigumu kubaki imara wakati wa nyakati ngumu. Ni vigumu kuwa karibu na wale wenye shida wanapotuhitaji sisi. Ni vigumu kuwa waminifu mpaka mwisho bila kuwa na aibu tunapokutana na vishawishi na hofu. Yesu anatupa nguvu na msaada wa upendo kamili yeye akiwa k**a Mchungaji wetu mwema, lakini pia anatuhitaji nasi turudishe upendo huu huu kwake, kwa kuwapatia wengine upendo huu mkamilifu. Pale uliposhindwa na kupungukiwa tunamuomba yeye atuchunge k**a mchungaji ili nasi tuweze kuwachunga wengine.

Mkimbilie mchungaji mwema na amini upendo wake kwako. Yesu sio tu mchungaji bali yeye mwenyewe ni chakula-malisho yenye kutoa uzima kwa wingi.
Leo, Kanisa zima linatukumbusha hitaji letu la kuomba, k**a Yesu mwenyewe alivyo waambia wanafunzi wake "mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake" (Lk 10: 2). Tangu hapo awali Kanisa “ kwa asili yake ni la kimisionari" (Ad Gentes, 2), wito wa Ukristo unazaliwa ndani ya watu kutokana na kazi ya umisionari. Kusikia na kufuata sauti ya Kristo Mchungaji mwema, maana yake ni kuruhusu tuvutwe naye na tuongozwe naye, kujiweka wakfu kwake maana yake kumruhusu Roho Mtakatifu kututumia sisi katika mabadiliko haya ya umisionari, na kuamsha ndani yetu tamaa, furaha na ujasiri wa kutoa maisha yetu wenyewe katika utumishi wa Ufalme wa Mungu.

Katika mz**i wa kila wito wa Kikristo, tunaona harakati hii ya msingi, ya kuacha nyuma faraja yetu na mambo yote yanayotupendezesha nafsi zetu na kujikita katika maisha ya Yesu Kristo. Ina maana ya kuondoka, k**a Abrahamu, na kuacha sehemu yetu ya asili na kwenda mbele kwa uaminifu, tukijua kwamba Mungu atatuonesha njia ya nchi mpya. Hii "kwenda mbele" isitazamwe k**a ishara ya mpango tu wa maisha ya mtu binafsi, hisia ya mtu au utu wa mtu mwenyewe. Kinyume chake, wale ambao wanamfuata Kristo wanapata uzima kwa wingi kwa kujiweka wenyewe bila kujibakiza katika utumishi wa Mungu na ufalme wake. Wito wa Kikristo kwanza kabisa ni wito wa upendo, upendo ambao hutuvuta sisi na kutuelekeza nje ya sisi wenyewe. Kuitika wito wa Mungu, maana yake kumruhusu yeye atusaidie kujiacha wenyewe kwa kuondokana na usalama wetu wa uongo, na kutoka nje na kuenenda kwenye njia inayoongoza kwa Yesu Kristo, aliye asili na hatima ya maisha yetu na furaha yetu.

Katika siku hizi kwanza tunaombwa tuombee Kanisa liweze kupata wachungaji wema na waadilifu wa kufanya kazi ya Kristo ya kueneza Injili na pia liweze kupata vijana wengi wanoitwa kwenye wito wa upadre na utawa. Maadili ya dunia yamerudi nyuma kwa sababu ya kukosekana kwa wachungaji. Mitandao ya kijamii, habari potofu toka baadhi ya vyombo vya habari na wasanii waliokosa maadili wanazidi kuiteka dunia na kuporomosha maadili yake. Tunahitaji wachungaji watakaotuonesha njia ya kusonga mbele.

Sala: Baba wa huruma, uliyemtoa mwanao kwa ajili ya wokovu wetu na ambaye anatutia nguvu kila wakati kwa zawadi ya Roho wako, tujalie sisi jumuiya ya Wakristo tuliohai, upendo na furaha, vilivyo vya muhimu kwa maisha ya kidugu, na vinavyojenga ndani ya wadogo mwamko wa wito wa kujitoa wenyewe wakfu kwako na kwa ajili ya wito wa uenezaji wa neno lako. Dumisha ndani ya jumuiya hizi majitoleo ya kutoa katekesi ya kuitika wito huu wakujitoa wakfu kwako. Wajalie hekima inayohitajika katika maamuzi ya kufuata wito wako, ili katika yote ukuu wa huruma yako ya upendo iweze kungara, Amina.

©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.

Usisahau KU-LIKE na KU-SHARE page hii ya Mkatoliki Imara

Address

Dar Es Salaam

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when Mkatoliki Imara posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Share