27/01/2026
HERITAGE FOUNDATION Yapendekeza JUMAPILI Iwe “SIKU YA MAPUMZIKO ”; KANISA LA WAADVENTISTA QA SABATO LATOA ONYO
Stanton Witherspoon
Januari 21, 2026
Mnamo Januari 8, Heritage Foundation ilitoa waraka unaowataka watunga sheria kuanzisha “siku ya pamoja ya mapumziko” siku ya Jumapili, jambo ambalo limesababisha Kanisa la Waadventista wa Sabato ya Saba Amerika Kaskazini kutoa taarifa ya onyo.
Heritage Foundation, inayojitambulisha k**a “kikundi cha utetezi wa sera za kihafidhina,” pia ilichapisha Project 2025, ambayo iliainisha malengo mengi ya sera yaliyounda msingi wa vipaumbele vya kisheria vya serikali ya sasa ya Marekani. Katika utangulizi wa Project 2025 yenye kurasa 900, ilisema kwenye ukurasa wa xiv:
“Lengo letu ni kukusanya jeshi la wahafidhina waliounganishwa, waliopitiwa (kuchunguzwa), waliopata mafunzo, na waliokuwa tayari kuanza kazi Siku ya Kwanza ili kuubomoa Mfumo wa Utawala wa Serikali.”
Katika taarifa iliyotolewa Januari 18, Idara ya Amerika Kaskazini (NAD) ilisema kuwa waraka mpya wa Heritage Foundation unaoitwa “Saving America by Saving the Family: A Foundation for the Next 250 Years” unaonesha “kupuuza kwa kutia wasiwasi uhuru wa dini wa Wamarekani wote.”
Hasa, NAD ilipinga vikali wito wa waraka huo kwa watunga sheria “kurejesha siku ya pamoja ya mapumziko kwa wafanyakazi wa Marekani” na “kulinda Jumapili k**a siku ya mapumziko, tafakari, na muda wa familia.” Heritage Foundation imedai kuwa kuwa na siku moja ya pamoja ya mapumziko kungeimarisha familia na kuboresha ustawi wa kijamii.
Ingawa pendekezo la Heritage Foundation linaonekana k**a hatua ya kuunga mkono familia na kujenga jamii, viongozi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato ya siku ya Saba wamesema kuwa mapendekezo ya kulinda Jumapili kupitia hatua za serikali yanafanana sana na sheria za Jumapili ambazo kanisa hilo limekuwa likizipinga kwa muda mrefu.
“Tunaamini kuwa watu wote wameumbwa kwa mfano wa Mungu na wana uhuru wa kuabudu kulingana na dhamiri zao,” ilisema taarifa ya NAD. “Kwa zaidi ya miaka 160, Kanisa limekuwa likipinga kwa nguvu aina yoyote ya sheria ya Jumapili.”
Upinzani huo umekuwa sehemu muhimu ya utambulisho wa umma wa dhehebu hilo tangu mwanzo wake.
Mwaka 1888, viongozi wa Waadventista walipinga hadharani mapendekezo ya sheria za shirikisho kuhusu Jumapili, zikiwemo sheria zilizodhaminiwa na Seneta wa Marekani Henry W. Blair ambazo zingehimiza utunzaji wa Jumapili kote nchini. Miongoni mwa sauti mashuhuri alikuwa Alonzo T. Jones, mhariri wa Kiadventista na mtetezi wa uhuru wa dini, ambaye alitoa ushahidi mbele ya Kamati ya Seneti ya Marekani ya Elimu na Kazi akisema, “Serikali haina haki ya kutunga sheria za ibada za kidini.”
Wanahistoria wa kanisa na kumbukumbu za uhuru wa dini za Waadventista zinaeleza ushahidi wa Jones k**a tukio muhimu lililochangia msimamo wa kanisa katika kutetea uhuru wa dhamiri na kutenganisha masuala ya ibada ya dini na sheria za serikali.
Maafisa wa NAD walisema mapendekezo ya Heritage Foundation yanafufua wasiwasi uleule wa zamani.
“Pendekezo hili jipya la ‘siku ya pamoja ya mapumziko’ haliendani kabisa na urithi tajiri wa Marekani wa kulinda uhuru wa dini wa raia wote,” iliendelea taarifa hiyo. “Linaonesha nia hatari ya kutumia mamlaka ya serikali kuendeleza malengo ya kidini.”
Zaidi ya masuala ya kikatiba, NAD ilionyesha pia athari za kivitendo kwa wachache wa kidini. Viongozi wa kanisa walisema kuwa utekelezaji wa vikwazo vya Jumapili unaweza kuwaweka waumini wa dini zinazofanya ibada siku nyingine, wakiwemo Waadventista na Wayahudi wa Kiorthodoksi, katika hali ya hasara ya kiuchumi.
“Kuzuia shughuli za kibiashara siku ya Jumapili pia kunaleta changamoto kubwa za kivitendo kwa waumini wa dini ambazo haziabudu Jumapili,” ilisema taarifa hiyo.
Kanisa liliweka msingi wa pingamizi lake katika Marekebisho ya Kwanza ya Katiba ya Marekani, ambayo yanakataza serikali kuanzisha dini na kulinda uhuru wa kutekeleza imani. NAD ilisema sheria za Jumapili zinakiuka kanuni ya kikatiba kwamba serikali inapaswa kubaki bila upendeleo kati ya mila na imani tofauti za kidini.
“Sheria za Jumapili zinakwenda kinyume na Marekebisho ya Kwanza ya Katiba ya Marekani, ambayo yanalinda uhuru wa dini kwa Wamarekani wote kwa kuitaka serikali kubaki bila upendeleo kati ya imani tofauti za kidini.”
Historia ya Heritage Foundation
Heritage Foundation ilianzishwa mwaka 1973 na inajieleza k**a taasisi ya utafiti na elimu yenye dhamira ya “kuunda na kukuza sera za umma zinazozingatia kanuni za biashara huria, serikali yenye mipaka, uhuru wa mtu binafsi, maadili ya jadi ya Marekani, na ulinzi imara wa taifa.”
Ikiwa na makao yake makuu Washington, DC, taasisi hiyo inasema inafanya kazi ya kuandaa mapendekezo ya sera na kuyawasilisha kwa watunga sheria, serikali kuu, na umma.
Ingawa pendekezo la mapumziko ya Jumapili bado halijawa muswada wa sheria, viongozi wa Waadventista walisema kuwa kujumuishwa kwake katika ripoti ya sera ya familia kunaonesha mwelekeo unaohitaji kuchunguzwa kwa makini.
Pendekezo hilo tayari limeingia katika mjadala mpana wa kitaifa kuhusu dini, sera za familia, na nafasi ya imani katika maisha ya umma. Gazeti la Washington Post hivi karibuni liliripoti juu ya mapendekezo mbalimbali yaliyomo katika ripoti ya Heritage, likieleza jinsi ilivyochochea mjadala miongoni mwa watunga sera na wachambuzi kutoka pande mbalimbali za kisiasa.
Sabato ya Uhuru wa Dini
NAD ilitoa taarifa yake wakati muhimu katika kalenda ya Waadventista. Kila mwaka, Sabato ya tatu ya Januari, Waadventista duniani kote huadhimisha Sabato ya Uhuru wa Dini, wakihimizwa kutafakari juu ya uhuru wa dhamiri na kuunga mkono kazi za kanisa katika eneo hili. Siku hiyo kwa kawaida huambatana na mahubiri maalum yanayozungumzia uhuru wa dini k**a haki ya kikatiba na pia k**a kanuni ya kiroho inayotokana na tabia ya Mungu. Sadaka maalum zinazokusanywa siku hiyo hutumika kusaidia idara ya Mahusiano ya Umma na Uhuru wa Dini ya kanisa, ambayo hutoa msaada wa kisheria kwa watu wanaokumbana na ubaguzi wa kidini na kuchapisha jarida la Liberty kwa ajili ya watunga sheria, majaji, na viongozi wa kiraia.
Maafisa wa NAD walisema wataendelea kushirikiana na watunga sera, mashirika ya uhuru wa dini, na washirika wa madhehebu mbalimbali.
“Viongozi wa kanisa letu katika Idara ya Amerika Kaskazini na katika makongamano ya muungano wataendelea kuinua bendera ya ukweli na uhuru wa dini,” ilisema taarifa hiyo, “wakipinga kwa uthabiti pendekezo hili na hatua zozote zinazofanana nalo.”