15/08/2026
*MASOMO YA MISA YA JUMAPILI*
*DOMINIKA YA ISHIRINI KATIKA KIPINDI CHA KAWAIDA MWAKA A*
*AGOSTI 16 2026*
*RANGI YA LITURUJIA: KIJANIπ*
*ANTIFONA YA KUINGIA*
Ee Mungu uliye ngao yetu, uangalie, utazame uso wa mpakwa wako. Kweli, siku moja katika nyua zako ni bora kuliko zingine elfu.
*KOLEKTA*
```Ee Mungu, umewaandalia wakupendao mema yasiyoonekana; uwashe mioyoni mwetu moto wa upendo wako, ili, kwa kukupenda wewe katika yote na kuliko yote, tuzifikie ahadi zako zinazopita hamu zote. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao....```
*MADA YA DOMINIKA*
```"KANISA KATOLIKI" LINAMAANISHA NINI?``
*SOMO LA KWANZA*
Isaya 56: 1, 6-7
_Nao wageni nitawaongoza mpaka mlima wangu mtakatifu_
*Somo katika kitabu cha Nabii Isaya*
Bwana asema hivi: "Shikeni sheria, tendeni haki, kwani wokovu wangu uko karibu kuja, na haki yangu iko karibu kufunuliwa. Nao wageni wanaoandamana na Bwana ili kumtumikia, na kulipenda jina la Bwana, -- kusudi wawe watumishi wake -- nao wote wanaotunza Sabato bila kuivunja, na kulishika agano langu, hao nitawaongoza mpaka mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala. Sadaka zao na matoleo yao vitakubaliwa juu ya altare yangu, kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote."
*Neno la Bwana*
*ZABURI YA KUITIKIZANA*
Zaburi 67: 2 - 3, 5, 6 na 8 (K. 4 )
*K. Watu na wakutukuze ee Mungu, watu wote na wakutukuze.*
Mungu na aturehemu na kutubariki;
Atuangazie uso wake. /Njia yake itambulike duniani,
Na wokovu wake katika mataifa yote..
*K*
Mataifa na wafurahi na kushangilia;
Kwa kuwa unawatawala kwa haki,
Na kuwaongoza mataifa ya dunia.
*K*
Watu na wakutukuze, ee Mungu;
Watu wote na wakutukuze!/ Mungu atatubariki sisi;
Na miisho yote ya dunia itamcha Mungu wetu.
*K*
*SOMO LA PILI*
Warumi 11: 13 -15, 29 - 32
_Kwa maana Mungu akiwajalia watu neema zake na kuwaita, hajuti tena._
*Somo katika barua ya Mtakatifu Paulo kwa Warumi*
Ndugu zangu: Ninyi watu wa mataifa, nawaambieni: Mimi niliye mtume wa watu wa mataifa, nakuza huduma yangu nikitumaini kuchochea wivu wa wenzangu wa damu moja, na hivyo kuwaokoa walau baadhi yao. Kwa kuwa kukataliwa kwao kumeiletea dunia upatanisho, kupokewa kwao kutazidi kuwa uzima baada ya kufa. Kwa maana Mungu akiwajalia watu neema zake na kuwaita,hajuti tena. K**a vile ninyi zamani mlivyomkaidi Mungu, sasa lakini mmesamehewa kutokana na ukaidi wao. Vivyo hivyo wale wamekaidi kwa ajili ya msamaha mliyojaliwa ninyi, ili sasa wao pia wasamehewe. Kwa maana Mungu amewatia wote katika ukaidi wao, ili awasamehe wote.
*Neno la Bwana*
*SHANGILIO LA INJILI*
Mathayo 4: 23
*Aleluya. Aleluya.*
Yesu alitangaza Injili ya ufalme akiponya kila namna ya magonjwa na maradhi kati ya watu.
*Aleluya*
*INJILI*
Mathayo 15: 21 - 28
_Mama, imani yako ni kubwa!_
βοΈ *Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo*
Wakati ule: Yesu aliondoka huko akaenda sehemu za Tiro na Sidoni. Hapo Mwanamke Mkananayo alikuja kutoka eneo lile akaita kwa sauti kubwa, " unihurumie, Bwana, Mwana wa Daudi. Binti yangu anasumbuliwa sana na pepo mbaya." Lakini hakumjibu neno, wafuasi wake Wakamwendea, wakamwomba wakisema, "Mwache aende zake, kwa maana anatufuata kwa kelele. " Akajibu, " Nimetumwa kwa kondoo wapotevu wa nyumba ya Israeli tu." Naye akaja,akamsujudia, akasema, " Bwana, unisaidie, " Akamjibu, " Si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. " Naye akasema, "Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo katika meza za Bwana wao." Hapo Yesu akajibu, akamwambia, "Mama, imani yako ni kubwa! Utendewe k**a utakavyo. " Tangu saa ile binti yake akawa mzima.
*Injili ya Bwana*