21/03/2026
*MASOMO YA MISA TAKATIFU YA JUMAPILI, MACHI 22, 2026*
*DOMINIKA YA TANO YA KWARESIMA, MWAKA A*
*RANGI YA LITURUJIA: URUJUANI 💜*
*ROZARI 📿: MATENDO YA UTUKUFU*
*MADA YA DOMINIKA:*
``` YESU: BWANA WA UZIMA.```
*_Masomo yote matatu leo yanahimiza maisha ambayo Mungu hutoa kwa watu wote. Somo la kwanza linatuambulishia mada hiyo kupitia unabii wa Ezekieli uliowapa Waisraeli tumaini la ufufuko. Injili inawasilisha ujumbe mpya ulioletwa na Yesu. Sio tena suala la ufufuko siku ya mwisho, lakini zawadi ya maisha mapya ambayo inazuia mtu kufa. Katika somo la pili Paulo anasema juu ya Roho, wakala wa ufufuko wa Kristo na wetu pia._*
*ANTIFONA YA KUINGIA: _Zaburi 43:1-2_*
_Ee Bwana, unihukumu, unitetee mbele ya taifa lisilo na huruma. Uniopoe, ee Mungu, na mtu wa hila na mwovu, kwa kuwa wewe ndiwe ngome yangu._
*KOLEKTA*
```Ee Bwana Mungu wetu, tunaomba msaada wako, ili na sisi ,,,tuenende kwa ari katika upendo ule ambao kwao Mwanao aliupenda ulimwengu hata akajitoa afe. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao...```
*SOMO LA KWANZA*
*EZEKIELI 37:12-14*
_Nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi_
_*Somo katika kitabu cha Nabii Ezekieli*_
Bwana Mungu asema hivi: Tazameni! Nitayafunua makaburi yenu, na kuwapandisha ninyi kutoka makaburi yenu, enyi watu wa taifa langu; nitawarudisha katika nchi ya Israeli. Nanyi mtatambua ya kuwa ndimi Bwana, nitakapofunua makaburi yenu, na kuwapandisha ninyi kutoka makaburi yenu, enyi watu wa taifa langu! Nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi, nitawaweka ninyi katika nchi yenu. Nanyi mtatambua ya kuwa Mimi, Bwana, nimenena; na nitatenda, asema Bwana.
_*Neno la Bwana*_
*ZABURI YA KUITIKIZANA*
*ZABURI 130:1-2, 3-4, 5-6, 7-8 (K. 7b)*
*KIITIKIO: _Kwa Bwana kuna fadhili, kwake kuna wokovu mwingi_*
Toka shimoni nakulilia, ee Bwana.
Ee Bwana, uisikie sauti yangu!
Masikio yako na yasikilize
sauti ya maombi yangu.
*KIITIKIO: _Kwa Bwana kuna fadhili, kwake kuna wokovu mwingi_*
K**a wewe, ee Bwana ungeweka kumbukumbu ya dhambi zetu,
ee Bwana, nani angesimama?
Lakini kwako kuna msamaha,
ili wakutumikie kwa uchaji.
*KIITIKIO: _Kwa Bwana kuna fadhili, kwake kuna wokovu mwingi_*
Ninamngoja Bwana, roho yangu inamngoja,
na ninalitumainia neno lake.
Roho yangu inamngoja Bwana
kuliko walinzi waingojavyo asubuhi.
*KIITIKIO: _Kwa Bwana kuna fadhili, kwake kuna wokovu mwingi_*
Ee Israeli, umngoje Bwana.
Kwa maana kwa Bwana kuna fadhili,
kwake kuna wokovu mwingi.
Yeye ataiokoa Israeli na maovu yake yote.
*KIITIKIO: _Kwa Bwana kuna fadhili, kwake kuna wokovu mwingi_*
*SOMO LA PILI*
*WARUMI 8:8-11*
_Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu_
_*Somo katika barua ya Mtakatifu Paulo kwa Warumi*_
Ndugu zangu: Wote walio wafuasi wa mwili hawawezi kumpendeza Mungu. Ninyi, lakini, si wafuasi wa mwili, bali wa roho, ikiwa Roho wa Mungu amekaa kweli ndani yenu. K**a mtu hana Roho wa Kristo, basi si mtu wake. Lakini k**a Kristo akiwa ndani yenu, ingawa miili yenu imekufa kwa sababu ya dhambi, roho zenu ni hai kwa sababu ya uadilifu. Ikiwa Roho wake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, basi yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataiokoa pia miili yenu katika hali ya kufa na kuitilia uzima kwa nguvu ya Roho anayekaa ndani yenu.
_*Neno la Bwana*_
*SHANGILIO LA INJILI*
*YOHANE 11:25a, 26*
_*Sifa na utukufu kwako, ee Kristo*_
Mimi ni ufufuo na uzima, asema Bwana; anisadikiye hatakufa milele.
_*Sifa na utukufu kwako, ee Kristo*_
✝️ *INJILI* 📖
*YOHANE 11:1-45*
_Mimi ni ufufuo na uzima_
_*Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Yohane*_
Wakati ule: Kulikuwa na mgonjwa mmoja, jina lake Lazaro wa Bethania, katika kijiji cha Maria na dada yake Martha. Ndiye Maria yule aliyempaka Bwana manukato, akamfuta miguu kwa nywele zake. ☆Basi, Lazaro, kaka yake, alikuwa mgonjwa. Dada hao wakampasha habari hii, "Bwana, umpendaye ni mgonjwa. Yesu aliposikia hayo, alisema, "Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo." Yesu alimpenda Martha na dada yake na Lazaro. Basi, aliposikia ya kuwa Lazaro ni mgonjwa, alishinda bado siku mbili mahali pale alipokaa. Kisha akawaambia wafuasi wake, "Twendeni Yudea tena." ☆ Wafuasi wake wakamwambia, "Rabbi, hivi karibuni tu Wayahudi walitaka kukupiga kwa mawe, nawe unataka kurudi huko?" Yesu akajibu, "Je, saa za mchana si kumi na mbili? Mtu akienda mchana, hajikwai, kwa maana anaona mwanga wa ulimwengu kuu. Lakini akienda usiku, hujikwaa, kwa sababu mwanga haumo ndani yake." Baada ya maneno hayo, akawaambia, "Rafiki yetu Lazaro analala, lakini ninakwenda kumwamsha. Wafuasi wakamwambia, "Bwana, akilala atapona." Yesu alikuwa anamaanisha mauti yake, lakini wale walidhani anamaanisha usingizi wa kawaida. Hapo Yesu akawaambia wazi wazi, "Lazaro amekufa. Nami nafurahi kwa ajili yenu ya kuwa sikuwako, mpate kusadiki. Lakini sasa twendeni kwake." Tomaso, aitwaye Pacha, akawaambia wafuasi wenziwe, "Twendeni nasi, ili tufe pamoja naye." ☆Yesu alipofika, alimkuta Lazaro amekaa kaburini kwa siku nne. Mji wa Bethania uko karibu na Yerusalemu, kadiri ya maili mbili hivi. Wayahudi wengi walikuwa wamefika kwa Martha na Maria kuwapa pole kwa sababu ya ndugu yao. ☆ Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alikwenda kumlaki; lakini Maria akaendelea kukaa nyumbani. Martha akamwambia Yesu, "Bwana, k**a ungalikuwapo, kaka yangu hangalikufa. Lakini hata sasa najua ya kuwa Mungu atakupa chochote utakachomwomba." Yesu akamwambia, "Kaka yako atafufuka." Martha akamjibu, "Najua atafufuka siku ya mwisho," Yesu akamwambia, "Mimi ni ufufuo na uzima; anisadikiye mimi hata k**a atakufa, ataishi, na kila anayeishi na kunisadiki hatakufa milele. Je, wasadiki hayo?" Naye akamjibu, "Ndiyo, Bwana, nasadiki ya kuwa wewe u Kristo, Mwana wa Mungu, atakayekuja ulimwenguni humu." Baada ya maneno hayo, Martha alikwenda kumwita Maria, dada yake, akimnong'onezea, "Mwalimu yupo, anakuita." Naye aliposikia hayo, alisimama upesi, akaenda kumlaki. Maana Yesu alikuwa hajaingia bado kijijini bali alibaki mahali alipokutana na Martha. Wayahudi waliokaa nyumbani pamoja na Maria ili kumfariji, walipomwona anasimama upesi na kuondoka, walimfuata wakidhani anakwenda kaburini kuomboleza huko. Basi, Maria akafika kwa Yesu. Mara alipomwona, alimwangukia miguuni pake, akamwambia, "Bwana, k**a ungalikuwapo hapa, kaka yangu asingalikufa." Tazama, Yesu alipomwona analia, na Wayahudi waliofuatana naye wanalia, ☆ "aliona uchungu rohoni, akafadhaika, na akasema, "Mmemzika wapi?" Wakamwambia, "Bwana, njoo uone." Yesu akalia machozi. Wayahudi wakasema, "Tazameni jinsi alivyompenda." Wengine wao wakasema, "Je, huyu aliyemfumbua kipofu macho hakuweza kumfanya na huyu asife?" Njiani, Yesu aliona uchungu tena moyoni mwake, kisha akafika kwenye kaburi. Lilikuwa ni pango, limefungwa kwa jiwe. Yesu akasema, "Liondoeni jiwe." Martha, dada ya aliyekufa, akamwambia, Bwana, sasa ni siku ya nne; ameanza kunuka." Yesu akamjibu, "Sikukuambia kwamba ukisadiki utaona utukufu wa Mungu?" Basi, wakaliondoa jiwe. Yesu akainua macho, akasema, "Baba, nakushukuru kwa sababu umenisikiliza. Nalijua ya kuwa wewe wanisikiliza siku zote; lakini kwa ajili ya watu hawa wanaohudhuria nilisema hayo, wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma." Baada ya maneno hayo, akaita kwa sauti kubwa, "Lazaro, njoo nje!" Maiti akatoka, miguu na mikono yake imefungwa sanda, na uso wake umefungwa kitambaa. Yesu akawaambia watu, "Mfungueni, apate kutembea." Wengi wa Wayahudi waliokuja kumtazama Maria, wakaona aliyoyafanya, wakamsadiki Yesu.☆
_*Injili ya Bwana*_
_Au somo fupi: Yohane l1:3-7.17.20-27.33b-45. Soma kati ya ☆_