22/08/2026
Na tuombe.
Ee Baba Mwenyezi Mungu, asubuhi hii tunakupa sifa na shukrani kwa neema na upendo wako. Twakushukuru kwa kutulinda usiku kucha na kutufikisha salama katika siku mpya. Ahsante kwa kutuepusha na hatari na kutulinda katika shughuli zetu.
Ee Baba wa rehema, tunakiri dhambi na makosa yetu. Utusamehe na utusafishe kwa damu ya Yesu Kristo, ututakase mioyo yetu na utujalie neema ya kuishi maisha yanayokupendeza. Tusaidie kutubu kwa kweli na kuacha yale yanayotutenga nawe.
Bwana Mweza-Yote, tunawakabidhi mikononi mwako wenye njaa, wagonjwa, waliofiwa, wenye huzuni na waliokata tamaa. Uwafariji, uwaponye na uwatie nguvu. Tunawaweka wote mikononi mwako tukiamini Wewe pekee una uwezo wa kutatua kila jambo.
Baba, tunalikabidhi taifa letu la Kenya kwako. Ulilinde na uliangalie kwa rehema zako. Wape viongozi hekima, busara na moyo wa utumishi wa kweli. Ulete amani, mshik**ano na uadilifu miongoni mwa jamii zote. Uibariki ardhi yetu, wakulima, mifugo na kazi za mikono yetu ili tuwe na chakula na ustawi.
Ee Baba, twalikabidhi Kanisa lako. Uliongoze kwa Roho Mtakatifu na ulifanye chombo cha tumaini, uponyaji na wokovu. Wabariki watumishi wako kwa nguvu, hekima na unyenyekevu wa kuongoza na kulihubiri Neno lako kwa uaminifu. Nasi utuzidishie maarifa na ufahamu ili tuwe nuru na chumvi ya dunia.
Ee Bwana, tunaziombea jamii zetu. Ulinde familia zetu, majirani na marafiki, utujalie mshik**ano, upendo na kusaidiana. Uondoe chuki, migawanyiko na uhasama, na utufundishe kuishi kwa heshima na mshik**ano. Ufanye kila kijiji na mtaa kuwa mahali pa tumaini, amani na maendeleo.
Baba yetu wa mbinguni, tunakushukuru kwa rehema zako. Tunayo mahitaji ya kibinafsi, uyasikie na uyajibu kwa mapenzi yako. Tusaidie tusiaibike bali tusubiri kwa imani na subira, tukijua wakati wako ni mkamilifu.
Tunapoanza siku hii, ukae nasi, utulinde na utuongoze katika kila hatua. Tujalie hekima, nguvu na neema ya kukutukuza katika yote tutakayofanya leo.
Tumeomba na kuamini, katika jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Amina.