07/09/2026
MASOMO YA MISA, SIKUKUU YA KUZALIWA BIKIRA MARIA MTAKATIFU,
SEPTEMBER 8, 2025
RANGI YA KILITURJIA: NYEUPE 🤍
SOMO LA KWANZA
MIKA 5:1—4a
Bwana atawatoa ninyi kwa maadui, mpaka yule mama mwenye mimba awe amejifungua.
Somo katika kitabu cha Nabii Mika
Bwana asema hivi: Lakini wewe, ee Bethlehemu ya Efratha, uliye mdogo kati ya koo za Yuda, kwako wewe atatokea kwa ajili yangu Yule atakayetawala juu ya Israeli; asili yake ni tangu zamani, tangu siku za kale na kale. Ndiyo maana Bwana atawatoa ninyi kwa maadui, mpaka yule mama mwenye mimba awe amejifungua; ndugu zake waliobaki salama watawarudia wana wa Israeli. Hapo Yeye atasimama imara, atachunga kundi lake kwa nguvu ya Bwana, na kwa utukufu wa jina la Bwana Mungu wake. Nao watarudi salama, maana atakuwa mkubwa hata mipaka ya dunia. Yeye atakuwa amani.
NENO LA BWANA... TUMSHUKURU MUNGU
au somo lifuatalo:
SOMO LA KWANZA
WARUMI 8:28—30
"Maana wale aliowajua toka mwanzo, aliwachagua."
Somo katika barua ya Mtakatifu Paulo kwa Warumi
Ndugu: Twajua ya kuwa wale wampendao Mungu hufanikiwa katika yote, ndio wale walioitwa toka mwanzo katika azimio lake. Maana wale aliowajua toka mwanzo, aliwachagua toka mwanzo ili kuwalinganisha na sura ya Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua toka mwanzo aliwaita; nao aliowaita aliwapa uadilifu; nao walioadilishwa aliwapa utukufu wa mbinguni.
NENO LA BWANA... TUMSHUKURU MUNGU
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 13:6ab, 6cd (K. Isaya 61:10)
K. Ninafurahi sana katika Bwana.
Nami, ee Bwana, nimeitumainia huruma yako,
ujalie moyo wangu furaha wokovu wako. K.
Nitamwimbia Bwana,
kwa maana amekuwa mkarimu kwangu. K.
SHANGILIO LA INJILI
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Umebarikiwa, ewe Bikira Maria, na unastahili sifa zote, kwa maana uliiletea dunia jua la haki, yaani Kristo Mungu wetu.
W. Aleluya.
SOMO LA INJILI
MATHAYO 1:1—16, 18—23
"Amepata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu."
† Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo
Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa Daudi, mwana wa Abrahamu. Abrahamu alimzaa Isaka; Isaka akamzaa Yakobo; Yakobo alimzaa Yuda na ndugu zake; Yuda alimzaa Peresi na Zera kwa Tamari; Peresi alimzaa Esromu; Esromu alimzaa Aramu; Aramu alimzaa Aminadabu; Aminadabu alimzaa Nashoni; Nashoni alimzaa Salmoni; Salmoni alimzaa Boazi kwa Rahabu; Boazi alimzaa Obedi kwa Ruthu; Obedi alimzaa Yese; Yese alimzaa mfalme Daudi. Sulemani alimzaa Rehoboamu; Rehoboamu alimzaa Abiya; Abiya alimzaa Asa; Asa alimzaa Yehoshafati; Yehoshafati alimzaa Yoramu; Yoramu alimzaa Uzia; Uzia alimzaa Yothamu; Yothamu alimzaa Ahazi; Ahazi alimzaa Hezekia; Hezekia alimzaa Manase; Manase alimzaa Amoni; Amoni alimzaa Yosia; Yosia alimzaa Yekonia na ndugu zake, wakati wa ule uhamisho wa Babeli. Na baada ya ule uhamisho wa Babeli, Yekonia alimzaa Shealtieli; Shealtieli alimzaa Zerubabeli; Zerubabeli alimzaa Abihudi; Abihudi alimzaa Eliakimu; Eliakimu alimzaa Azori; Azori alimzaa Sadoki; Sadoki alimzaa Akimu; Akimu alimzaa Eliudi; Eliudi alimzaa Eleazari; Eleazari alimzaa Mathani; Mathani alimzaa Yakobo; Yakobo alimzaa Yosefu mumewe Maria aliyemzaa YESU aitwaye Kristo.
*Kuzaliwa kwa Yesu Kristo kulikuwa hivi. Maria, mama yake, alipokuwa ameposwa na Yosefu, kabla hawajakaa pamoja alionekana ana mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Mumewe Yosefu akiwa mtu mwadilifu, hakupenda kumwaibisha hadharani. Basi, akanuia kumwacha kwa Siri. Alipokuwa akifikiria hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea ghafla katika ndoto, akasema, "Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumpokea Maria kuwa mke wako, maana mimba yake ameipata kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Atamzaa mwana, naye utampa jina lake "Yesu." Maana yeye atawaokoa watu wake katika dhambi zao." Hayo yote yametendeka, ili neno alilonena Bwana kwa njia ya nabii litimie, kwamba: "Tazama, bikira atachukua mimba na kumzaa mwana, naye watamwita Emanueli maana yake, "Mungu pamoja nasi."
INJILI YA BWANA... SIFA KWAKO EE KRISTO