09/01/2026
Baba Mtakatifu Leo XIV, ameligawa jimbo Katoliki Shinyanga na kuanzisha jimbo jipya la Bariadi. Jimbo Katoliki Shinyanga lililokuwa na waumini 880,000 kwa sasa litabaki na waumini 514,000 huku waumini 366,000 wakiangukia jimbo jipya la Bariadi.
Parokia 24 zitabaki Shinyanga na parokia 19 zitakuwa sehemu ya jimbo jipya la Bariadi. Mapadre 63 watabaki Shinyanga na 43 wataenda Bariadi. Shule 12 zitabaki Shinyanga na shule 9 zitakuwa jimbo la Bariadi. Hospitali na vituo vya afya 9 vitabaki Shinyanga na 7 vitakua Bariadi.
Baba Mtakatifu amemteua Askofu Rev.Dr.Prosper Baltazar Lyimo (PhD) kuwa Askofu wa kwanza wa jimbo jipya la Bariadi. Kabla ya uteuzi huo alikuwa Askofu Msaidizi wa jimbo kuu katoliki Arusha.
Askofu Prosper Lyimo alizaliwa kijiji cha Kyou, Kilema, wilayani Moshi, Agosti 20, 1964. Alisoma shule ya msingi Ngurdoto, Arusha, na sekondari ya Thomas Aquinas kidato cha kwanza hadi cha sita na kufaulu vizuri (division 1 form four, division 1 form six).
Alijiunga na Seminari ya Kibosho kwa Shahada ya Kwanza ya Falsafa (Bachelor Degree in Philosophy) na baadae Seminari Kuu ya St.Paul kwa Shahada ya Utaalimungu (Bachelor Degree in Theology) na kuhitimu mwaka 1996. Alipata daraja la Upadri tarehe 4 Julai 1997.
Amekua mlezi wa kiroho (Chaplain) seminari ndogo ya Mtakatifu Thomas Aquinas, Arusha (1997-1999) kisha akateuliwa kuwa Kansela wa jimbo kuu Arusha (2000-2004).
Baadaye alitumwa masomoni Chuo Kikuu cha Kipapa (University of Urbaniana) mjini Roma, Italia kwa Shahada ya Uzamili katika Sheria za Kanisa (Masterโs Degree in Canon Law) mwaka 2004 hadi 2007.
Baada ya kuhitimu alirudi na kutumika k**a Padre jimbo kuu Arsha, kabla ya kutumwa tena masomoni Chuo Kikuu cha St.Paul, kilichopo Ottawa, Canada kusomea Shahada ya Uzamivu ya Sheria (Juris Canonici Doctor, JCD) na kuhitimu mwaka 2011. Aliporudi alihudumu k**a Kansela na Mwanasheria wa jimbo kuu Katoliki Arusha (2011-2014).
Novemba 11, 2014 aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francis kuwa Askofu msaidizi wa jimbo kuu Arusha, na askofu wa heshima wa Vanariona (Algeria) nafasi alizohudumu hadi leo alipoteuliwa kuwa Askofu wa jimbo jipya la Bariadi. Tumtakie heri katika Utume wake huu mpya.!