Kibabii University Catholic Community

Kibabii University Catholic Community Arise and evangelise

27/09/2025

*MASOMO YA MISA, SEPTEMBA 27 2025.*

*JUMAMOSI YA JUMA LA ISHIRINI NA TANO KATIKA KIPINDI CHA KAWAIDA MWAKA C(I).*

*KUMBUKUMBU YA MTAKATIFU VINSENTI WA PAULO, PADRE NA MWANZILISHI WA IMANI.*

*RANGI YA KILITURJIA: NYEUPE 🤍*

*ROZARI: MATENDO YA FURAHA.*

*SOMO LA KWANZA*

*Somo katika kitabu cha Nabii Zakaria (ZAKARIA 2: 5 - 9, 14 - 15a)*

Niliyainua macho yangu, nikaangalia. Tazama, alionekana mtu mwenye kamba ya kupimia mkononi. Nikamwuliza, “Una kwenda wapi?” Akanijibu, “Nakwenda kuupima Yerusalemu, ili nione una upana na urefu gani." Tazama, yule malaika aliyesimama nami akasimama kimya, lakini malaika mwingine akamwendea, akamwambia: "Nenda mbio, ukamwambie kijana yule: Yerusalemu utakuwa k**a mji usio na boma, kwa sababu ya wingi wa watu na wanyama waliomo ndani yake. Mimi mwenyewe, asema Bwana, nitauzunguka k**a ukuta wa moto; nitakuwa utukufu wake ndani yake." “Imba na furahi,ee binti Sioni, maana, tazama, ninakuja ili nikae kati yako, asema Bwana. Na katika siku ile, mataifa mengi watajiunga na Bwana, nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa kati yako."

*Neno Ia Bwana......*
*Tumshukuru Mungu.*

*ZABURI YA KUITIKIZANA*
Yeremia 31: 10, 11 - 12ab, 13 (K.) 10d

*K/. Bwana atatulinda k**a mchungaji alilindavyo kundi lake.*

Enyi mataifa, lisikieni neno la Bwana,
litangazeni katika pwani za mbali;
semeni: “Aliyemtawanya Israeli atamkusanya;
atamlinda k**a mchungaji alindavyo kundi lake. *K/.*

Kwa maana Bwana atamwokoa Yakobo,
atamwopoa katika mkono wa mtu
mwenye nguvu kumpita yeye.
Watakuja na kupaza sauti kwa shangwe juu ya Mlima Sioni,
wataukimbilia wema wa Bwana. *K/.*

Hapo binti watafurahi kwa kucheza ngoma,
na vijana na wazee vilevile.
Nitageuza huzuni yao kuwa changamko,
nitawatuliza na kuwafurahisha baada ya mateso yao. *K/.*

*SHANGILIO LA INJILI*
2 Timotheo 1: 10

*K. Aleluya. W. Aleluya.*
Mwokozi wetu Kristo Yesu ameyashinda mauti na ametangaza uzima wa milele kwa Injili.
*W. Aleluya.*

*INJILI*

*Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Luka (LUKA 9: 43b - 45)*

Wakati ule: Watu wote walipokuwa wanastaajabia mambo yote aliyoyafanya,Yesu aliwaambia wafuasi wake, "Tunzeni masikioni mwenu maneno haya. Mwana wa Mtu anakwenda kutiwa mikononi mwa watu." Lakini hawakulifahamu neno hilo; lilifichwa kwao wasilitambue, nao wakaogopa kumwuliza maana ya neno hilo.

*Injili ya Bwana......*
*Sifa Kwako Ee Kristo.*

25/09/2025

*MASOMO YA MISA, SEPTEMBA 25 2025.*

*ALHAMISI YA JUMA LA ISHIRINI NA TANO, KIPINDI CHA KAWAIDA, MWAKA C(I)*

*RANGI YA KILITURJIA: KIJANI KIBICHI💚*

*ROZARI: MATENDO YA MWANGA.*

*SOMO LA KWANZA*
Ijengeni nyumba itakayonipendeza.

*Somo katika kitabu cha Nabii Hagai (HAGAI 1: 1 — 8)*

Katika mwaka wa pili wa utawala wake mfalme Dariusi, siku ya kwanza ya mwezi wa sita, neno la Bwana liliwafikia Zerubabeli, liwali wa Yuda, na Yeshua kuhani mkuu, kwa kinywa cha nabii Hagai. Alisema: Bwana wa ulimwengu amesema hivi: Watu hawa wanasema: "Wakati wa kujengwa tena nyumba ya Bwana haujafika." Ndipo Neno la Bwana lilipokuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema: Je, huu ndio wakati kwenu ninyi kukaa katika nyumba zenu zenye mapambo ya mbao, hali nyumba hii inabaki kuwa magofu? Basi sasa Bwana wa majeshi asema hivi: Zitafakarini njia zenu. Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula, lakini hamshibi; mnakunywa, lakini hamkati kiu; mnavaa nguo, lakini hampati joto; na mtu wa mshahara apatapo mshahara, huutia katika mfuko uliotoboka. Basi Bwana wa majeshi asema hivi: "Zitafakarini njia zenu. Nendeni kwenye nchi ya milima; mlete mbao na mjenge nyumba itakayonipendeza, nami nitatukuzwa, asema Bwana."

*Neno la Bwana....*
*Tumshukuru Mungu.*

*ZABURI YA KUITIKIZANA*
Zaburi 149: 1b — 2, 3 — 4, 5 — 6a na 9bc (K. 4a)

*K. Bwana anapendezwa na watu wake.*
au:
*Aleluya.*

Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
sifa yake ivume katika mkutano wa waaminifu.
Israeli na amfurahie mwumbaji wake;
wana wa Sioni na wamshangilie mfalme wao. *K.*

Walisifu jina lake kwa kucheza,
wamwimbie kwa matari na kinubi.
Kwa kuwa Bwana apendezwa na watu wake;
huwapamba wanyonge kwa wokovu. *K.*

Waaminifu na wamshangilie kwa utukufu,
waimbe kwa sauti kubwa ya furaha vitandani mwao.
Sifa za Mungu na ziwe vinywani mwao,
ndiyo heshima ya waaminifu wake wote. *K.*

*SHANGILIO LA INJILI*
Yohane 14: 7

*K. Aleluya. W. Aleluya.*
K. Mimi ndimi njia, ukweli, na uzima, asema Bwana; hakuna ajaye kwa Baba, ila kwa njia yangu mimi.
*W. Aleluya.*

*INJILI*
Yohane nilimkata kichwa; ni nani basi huyu ambaye ninasikia habari zake?

*† Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Luka (LUKA 9: 7 — 9)*

Wakati ule: Mfalme Herode alisikia yote yaliyotendeka, akahangaika kwa sababu watu wengi walisema ya kwamba "Yohane amefufuka katika wafu"; wengine walisema kwamba "Eliya ametokea," tena wengine kwamba "Mmojawapo wa manabii wa kale amefufuka." Lakini Herode akasema, "Yohane nilimkata kichwa. Basi, ni nani huyu ambaye ninasikia mambo k**a haya juu yake?" Akatafuta nafasi ya kumwona.

*Injili ya Bwana.....*
*Sifa Kwako Ee Kristo.*

03/12/2022

For the laity, this is the appropriate posture.

18/11/2022
MASOMO YA MISA JUMAPILI, OKTOBA 2, 2022DOMINIKA YA 27 YA MWAKASOMO 1Hab. 1:2 – 3; 2:2 – 4Ee Bwana, nilie hata lini, wewe...
02/10/2022

MASOMO YA MISA
JUMAPILI, OKTOBA 2, 2022
DOMINIKA YA 27 YA MWAKA

SOMO 1
Hab. 1:2 – 3; 2:2 – 4

Ee Bwana, nilie hata lini, wewe usitake kusikia? Nakulilia kwa sababu ya udhalimu, ila hutaki kuokoa. Mbona wanionyesha uovu, na kunitazamisha ukaidi? Maana uharibifu na udhalimu u mbele yangu; kuna ugomvi, na mashindano yatokea. Bwana akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi asana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma k**a maji. Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia; ingojee; kwa kuwa haina bidi kuja, haitakawia. Tazama, roho yake hujivunia, haina unyofu ndani yake; lakini mwenye haki ataishi kwa Imani yake.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 95:1 – 2, 6 – 9, (K) 7 – 8

(K) Ingekuwa heri leo tusikie sauti yake! Tusifanye migumu mioyo yetu.

Njoni tumwimbie Bwana,
Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
Tuje mbele yake kwa shukrani,
Tumfanyie shangwe kwa zaburi. (K)

Njoni, tuabudu tusujudu,
Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
Kwa maana ndiye Mungu wetu,
Na sisi, tu watu wa malisho yake,
Na kondoo za mkono wake. (K)

Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu;
K**a huko Meriba;
K**a siku ile ya Musa jangwani,
Hapo waliponijaribu baba zenu,
Wakanipima, wakayaona matendo yangu. (K)

SOMO 2
2Tim. 1:6 – 8; 13 – 14

Ndugu yangu, nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu. Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu nay a upendo nay a moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wal ausinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu. Shika kielelezo cha maneno yenye uzima uliyoyasikia kwangu, katika Imani na upendo ulio katika Kristo Yesu. Ilinde ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

SHANGILIO
Yn. 15:15

Aleluya, aleluya,
Ninyi nimewaita rafika,
kwa kuwa yote niliyoyasikia
kwa baba yangu nimewaarifuni.
Aleluya!

INJILI
Lk. 17:5 – 10

Mitume walimwambia Bwana, Tuongezee Imani. Bwana akasema, K**a mngekuwa na Imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng’oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii.
Lakini, ni nani kwenu mwenye mtumwa alimaye au achungaye ng’ombe, atakayemwambia mara arudipo kutoka shambani, Njoo upesi, keti, ule chakula? Je! Hatamwambia, Nifanyie tayari chakula, nile; jifunge unitumikie, hata niishe kula na kunywa, ndipo nawe utakapokula na kunywa? Je! Atampa asante yule mtumwa; kwa sababu ameyafanya aliyoagizwa? Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya.

Injili ya Bwana...Sifa kwako, ee Kristo

01/10/2022

“MBEGU ZA UZIMA”
Jumapili, Oktoba 2, 2022
Dominika ya 27 ya Mwaka

Hab 1:2-3; 2:2-4
Zab 95: 1-2, 6-9
2 Tim 1: 6-8, 13-14
Lk 17: 5-10

KUSALI KWA IMANI!

Biblia haijasema k**a Abrahamu alienda kwenye mapango kusali lakini anachukuliwa Baba wa imani: baba wa imani na mfano wa sala. Maisha Yake yanatawaliwa na sala na imani; alifanya vitu tu baada ya kusikia sauti ya Mungu; alichukua jukumu na kutekeleza na kushika njia mara baada ya kusikia neno la Bwana. Maisha Yake yanatawaliwa na mazungumzo baina Yake na Mungu. Mungu alimwambia Abram: nenda....Abram akaondoka... (Mwa 12:1,4)... " Neno la Mungu lilimjia Abram katika ndoto ..... na Abram akasema: Bwana utanipa nini Mimi?”… (Mwa 15:1,2). Bwana alimtokea katika Mamre na hapo akainamisha kichwa chake ardhini" Mwa 18:1-3). “Bwana alimjaribu Abram... Abram akajibu nipo hapa!”(Mwa 22:1) mazungumzo haya yaliijaza imani ya Abraham, yalimwandaa kupokea mapenzi ya Mungu.

Nabii Habakuki aliishi na changamato nyingi sana katika imani Yake. Ukosefu wa Haki, maovu katika jamii yanaonesha Mungu hapendezwi na haingilii kati. Habakkuki ana jaribu Kuelewa yanayotea na haogopi kuanza masungumzo na Mungu. Anathubutu kumuuliza Mungu kwa ujasiri kwamba anapingana naye, kwamba haelewi kukaa kwake kimya bila kutenda kitu dhidi ya maovu, anamkumbusha juu ya ukimya wake na kutokufanya kitu; anathubutu kumwambia atoe hesabu ya njia zake juu ya kuutawala ulimwengu na matukio ya kihistoria. Baada ya kutoa malalamiko yake, na juu ya uovu wa watu, nabii anakaa kimya. Ni wakati wa Mungu kujibu. Mungu anajibu, hatoi maelezo yeyote, anadai juu ya uaminifu usio na masharti. Anajua juu ya mapungufu ya nabii na ya watu; alijua kwamba hawawezi kuelewa sababu ya ukimya wake wakutokufanya kitu. Badala yake anatoa uhakika kwamba kilichosemwa leo siku moja kitaeleweka kwa wote.

Katika somo la pili mtume Paulo pia anaongelea kuhusu imani. Timoteo anaongelea kuhusu kuwa na imani, kwa njia yake kueneza matendo ya huruma. Mfuasi pia anaalikwa kuwa mkarimu katika Imani, zawadi ya Mungu ambayo ipo ndani yake na kwanjia ya kuwekea mikono, anasimikwa k**a zawadi, aliyopokea ili aweze kuchukua kazi zake za kitume k**a msaidizi wa Paulo. (2 Tim 1: 6).

“Imani” katika uhalisia ni kujikita kwa mtu, kujikabidhi kwa mtu, uaminifu, na mshikamono unaotoka katika uaminifu huo. Ndio kusema, mitume hawamuombi Yesu kuongeza uelewa wao au akili zao kuhusu mambo. Wanamuomba Yesu aongeze uaminifu wao kwake. Yesu bila kujibu moja kwa moja sala yao, anatumia njia nyingine na anatumia taswira ya picha kuelezea hali ya juu ya Imani na umuhimu wake. K**a vile Kamba yaweza kushikilia kitu kizito kuliko kamba yenyewe, ndivyo ilivyo kwa Imani kidogo, inaweza kufanya kitu kikubwa ambacho huwezi kufikiria, kitu cha hali ya juu, k**a vile kungoa mti mkubwa na kuupanda baharini. Imani, ndio kusema, kumuamini Kristo, kumkaribisha, na kumfanya atubadilishe, kumfuata mpaka mwisho kabisa, inafanya mambo ya mwanadamu yasiowezekana yawezekane katika hali zote.

Mbegu ni kwa ajli ya kupanda, ili vitu vingine vizuri zaidi vinavyopendwa viote. Tunapo otesha mbegu ya Imani yetu, inasababisha Imani zaidi iweze kukuwa, na matendo ya Imani, ambayo ni upendo wa Mungu, haki na huruma. Kwa njia hii tunaleta upendo wa Mungu kwa wasio pendwa, nakupenda, huruma ya Mungu kwa wasio na huruma na kwa wote ambao hawajaitambua huruma ya Mungu maishani mwao. Tunafanya haki ya Mungu ikuwe katika maeneo yasio na upendo, yenye vita na dhuluma, na kwa mioyo isio na haki. Tuna sababisha Imani ikuwe kwenye mioyo ya watu ambao hawakuwa na Imani, au kwa walio poteza Imani yao kwasababu ya kuboreka na kupoteza tumaini. Kwa kupanda na kupalilia mbegu ya Imani, tunakuta na Imani yetu wenyewe inakuwa, na jukumu k**a kusamehe, kila mara inamfanya mtu iwe rahisi na neema kukuwa zaidi, ni k**a sehemu za kazi katika maisha yetu, kadiri tufanyavyo kazi flani ndivyo inakuwa rahisi na nyepesi katika kuitenda: mfano pia, kucheza mpira, kucheza ala za muziki, kutengeneza picha nk. Imani yetu inatosha na ni muhimu. Tuna sehemu ya kusimamia na kuwa vyote anavyotaka Mungu.

Matukio mengi katika maisha yetu yanaweza kuonekana ya kushangaza na hayafikiriki na yanatufanya tuwe na maswali kuhusu uwepo wa Mungu. Kipindi hiki Imani yetu inawekwa kwenye majaribu makubwa, na mara nyingi tunamlilia Mungu na kumuomba msaada. “Bwana sikia sala yangu” sikiliza kilio chetu”. Mungu kila wakati anasikia sauti zetu ingawaje ni vigumu kwetu kutambua sauti yake. Sala ndio inayo fungua moyo wetu, inatusaidia kuelezea mahitaji yetu, ulinzi wetu na mipango yetu na hapo kutufanya sisi tuyakaribishe mapenzi ya Mungu katika maisha yetu. Tutafute Imani iliojitosheleza na thabiti kwa Mungu kwa njia ya sala. Imani tukiwa katika mateso yetu, Imani kuona mapenzi ya Mungu yametimia katika maisha yetu.

Sala: Bwana Yesu, ongeza Imani yetu na utufanye tuwe watumishi wako wa aminifu, ili tuendelee kufanya utume wako na kukushuhudia Wewe. Amina.

Copyright ©2013-2022 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

Address

1699
Bungoma

Telephone

+254700346337

Website

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when Kibabii University Catholic Community posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Share