06/23/2026
SOMO LA LEO: MOYO WENYE SHUKRANI HUMPENDEZA MUNGU
1 Wathesalonike 5:18"Shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu."
NENO KUU: Shukrani kwa Mungu.
WAZO KUU: Mungu hufurahishwa na watu wanaojua kutambua wema wake na kumshukuru katika kila hali ya maisha.
SHABAHA: Kukuhimiza wewe muumini kuwa na moyo wa shukrani kila siku, ukitambua kwamba kila jambo jema hutoka kwa Mungu.
UTANGULIZI
Ni rahisi kumshukuru Mungu wakati mambo yanakwenda vizuri. Tunapopata kazi, tunapopona ugonjwa, tunapofanikiwa katika biashara au tunapopokea baraka tulizoziomba, shukrani hutoka kwa urahisi. Lakini mtume Paulo anasema:"Shukuruni kwa kila jambo." Hakusema shukuruni kwa mambo mazuri pekee. Alisema kwa kila jambo. Hii haimaanishi kufurahia mateso au majaribu, bali kutambua kwamba hata katikati ya hali ngumu, Mungu bado anatawala na ana kusudi jema kwa maisha yetu.
1. SHUKRANI HUONYESHA KWAMBA TUNAMTAMBUA MUNGU
Yakobo 1:17"Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga." Watu wengi hupokea baraka lakini husahau chanzo chake. Mtu anapata afya nzuri, lakini hasemi asante. Anapata kazi, lakini hamkumbuki Mungu. Anapata familia nzuri, lakini hana muda wa kumshukuru Mungu. Moyo wenye shukrani hutambua kwamba kila tulicho nacho ni zawadi kutoka kwa Mungu.
Fundisho:
Kadiri tunavyotambua wema wa Mungu, ndivyo shukrani zetu zinavyoongezeka.
2. SHUKRANI HUFUKUZA MANUN'UNIKO
Wafilipi 2:14 "Yatendeni yote pasipo manung'uniko."
Waisraeli waliona miujiza mingi jangwani, lakini mara nyingi walilalamika.
Badala ya kuhesabu baraka walizopokea, walikazia macho matatizo yao.
Matokeo yake, walikosa furaha na amani. Mtu mwenye moyo wa shukrani huona kile Mungu amefanya badala ya kuangalia tu kile ambacho bado hajapata.
FundishoManung'uniko humfanya mtu asione baraka zake, lakini shukrani humfanya azione hata zilizo ndogo.
3. SHUKRANI HULETA AMANI MOYONI
Wafilipi 4:6-7"Katika kila neno kwa kusali na kuomba pamoja na kushukuru..."
Paulo anaunganisha maombi na shukrani. Tunapomshukuru Mungu, mioyo yetu hujazwa amani.
Badala ya kuishi katika wasiwasi, tunaanza kukumbuka jinsi Mungu alivyotutunza zamani. Na k**a alitusaidia jana, atatusaidia tena leo.
Fundisho: Moyo wa shukrani hujenga imani na kuondoa hofu.
4. YESU ALITUACHIA MFANO WA SHUKRANI
Luka 22:19. Kabla ya kula mkate katika karamu ya mwisho, Yesu alishukuru. Hata kabla ya kumfufua Lazaro, Yesu alimshukuru Baba. Yesu alionyesha kwamba shukrani si jambo la kufanya baada ya kupata kila kitu tunachotaka, bali ni mtindo wa maisha.
Fundisho: Ikiwa Yesu mwenyewe alikuwa na moyo wa shukrani, sisi pia tunapaswa kuishi kwa shukrani.
5. MUNGU HUFURAHISHWA NA WATU WENYE SHUKRANI
Luka 17:15-18 Yesu aliwaponya watu kumi wenye ukoma. Lakini mmoja tu alirudi kumshukuru. Yesu akauliza: "Je! hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wako wapi?"Mungu anathamini moyo unaorudi kutoa shukrani.
Fundisho: Usiwe mtu anayepokea baraka na kuondoka kimya kimya. Jifunze kurudi na kusema, "Asante Bwana."
HITIMISHO
Leo ukiangalia maisha yako, utagundua kwamba Mungu amekufanyia mengi. Amekupa pumzi ya uhai. Amekulinda katika hatari nyingi usizoziona. Amekupa nguvu za kuendelea. Amekupa neema ya kufika leo. Huenda bado kuna maombi ambayo yanasubiri majibu. Lakini bado unayo sababu nyingi za kumshukuru Mungu.Kwa hiyo, usisubiri mpaka kila tatizo liishe ndipo umshukuru Mungu.Mshukuru sasa. Mshukuru kila siku.Mshukuru katika furaha na katika majaribu. Kwa sababu moyo wenye shukrani humpendeza Mungu.
TUOMBE:
Baba yetu wa mbinguni, ninakushukuru kwa wema wako, rehema zako na upendo wako usio na mwisho. Asante kwa pumzi ya uhai, kwa ulinzi wako, kwa chakula, kwa familia, na kwa neema zako ambazo naziona na hata nisizoziona. Nisamehe pale ambapo nimekuwa nikilalamika badala ya kushukuru. Nifundishe kuwa na moyo wa shukrani katika kila hali ya maisha. Nijalie kuona wema wako kila siku na nikutumike kwa furaha na unyenyekevu. Na maisha yangu yawe sadaka ya shukrani mbele zako siku zote. Naomba haya kwa Jina la Yesu Kristo. Amina.
Comments, shares na likes ni mojawapo ya njia ya kushirikiana nasi katika kuwafikia wengi iwezekanavyo. MUNGU akubarik