11/08/2026
HUKUCHAGULIWA KWA BAHATI MBAYA UKAE KWENYE NAFASI ULIYONAYO LEO
Mdo 6:3-4 SUV
[3] Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; [4] na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.
Napenda niongee na wale ambao wamechaguliwa katika nafasi mbalimbali katika kundi la Mungu, au kanisa la Mungu, au kusanyiko la ki-Mungu.
Tunaweza kufikiri nafasi tuliyopewa ni nafasi k**a zingine za kawaida, tunaweza kuchukulia kwa uzito mdogo zile nafasi tulizopewa au kuchaguliwa.
Hatujui au hatujiulizi kuwa kuchaguliwa kwetu ilitokea nini mpaka watumishi wa Mungu wakaa na kuona vyema fulani na fulani wakae katika nafasi fulani.
Hupaswi kujichukulia kawaida na kujiona mnyonge, waliokuweka hapo hawakulala Leo na kuamka kesho yake wakakuweka. Ulikuwepo mchakato mrefu wa kukupata wewe.
Lipo jukumu kubwa ambalo waliokuweka waliona unaweza kulifanya na wao wakafanya majukumu mengine ya ki-Mungu.
Mdo 6:2 SUV
[2] Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani.
Unamwona mchungaji, Askofu, au yeyote yule aliyekaa kwenye nafasi fulani kuliongoza kundi la BWANA kuona vyema kukuchagua wewe au mtu fulani akae kwenye nafasi fulani, kwa akili ya kawaida utaona ni matakwa yake, bila kujua MUNGU amesema nini naye.
Sio hivyo tu, kwenye huduma/madhehebu mbalimbali wameweka miongozo ya idara, watu huchaguliwa kila baada ya kipindi fulani, wengine huchaguliwa kuwa shemasi, wazee wa kanisa, katibu na waratibu wa idara mbalimbali kanisani.
Kufanya hivyo ni kurahisisha utendaji wa Ki- Mungu kanisani, usipoelewa utatumika kwa mazoea na kwa viwango vya chini, bila kufanya unajikosesha baraka za Mungu zinazotaka na nafasi uliyowekwa.
Wakati mwingine Mungu hutupa kibali cha kukaa kwenye nafasi za chini kabisa, tukiwa waaminifu hutuweka nafasi zingine za juu zaidi.
Leo unaweza kujiona upo kwenye nafasi fulani ndogo kabisa kwenye hiyo huduma ya Mungu au kanisa, ukajua ni jambo la kawaida au watu hawajui heshima yako huko kazini kwako au kwenye jamii. Ama kwenye mipango yako unayo maono makubwa, ukaona nafasi uliyopewa hailingani na viwango vya maono yako, ukaidharau, bila kujua ulikuwa msingi wako wa majaribio wa kukupeleka kwenye eneo Mungu anataka ufike.
Napenda kukuasa jambo hili, ikiwa umechaguliwa na kuwekewa mikono utumike kwenye nafasi fulani, usije ukaipuuza na kuifanya kwa viwango vya chini. Watu waliomba na kukuona unafaa, unachokifanya kwa uzembe halikuwa kusudi la Mungu, upo nje ya mapenzi ya Mungu.
Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia na kutafakari
Mungu akubariki sana
Samson Ernest