Moravian Sabasaba Singida

Moravian Sabasaba Singida Preaching and proclaiming good news of Jesus Christ through social media

29/08/2026
MUNGU NI MKUU KULIKO TATIZO UNALOLIONA                      KUTOKA 15:3–7"“BWANA ni mtu wa vita, BWANA ndilo jina lake. ...
22/08/2026

MUNGU NI MKUU KULIKO TATIZO UNALOLIONA

KUTOKA 15:3–7
"“BWANA ni mtu wa vita, BWANA ndilo jina lake. Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini; maofisa wake wateule wamezama katika Bahari ya Shamu. Vilindi vimewafunikiza; walizama vilindini k**a jiwe.

BWANA, mkono wako wa kuume umepata fahari kwa uwezo; BWANA, mkono wako wa kuume wawasetaseta adui. Kwa wingi wa ukuu wako wawaangusha wanaokupinga; waituma hasira yako, nayo huwateketeza k**a mabua makavu.”

TAFAKARI

Mungu ni mkuu kuliko jambo lolote tunaloliwaza au kuliona. Wana wa Israeli walitambua ukuu wake baada ya kuvuka Bahari ya Shamu na kuliona jeshi la Farao likizama baharini.

Ingawa walikuwa wameshuhudia mapigo kumi yaliyompata Farao na jinsi Mungu alivyowatoa Misri, walipoona jeshi la Farao likiwakaribia, walijawa na hofu kana kwamba Mungu hakuwahi kuwaokoa. Walisahau kwamba Mungu aliyewatoa Misri ndiye aliyekuwa pamoja nao mbele ya Bahari ya Shamu.

Nasi wakati mwingine hutazama ukubwa wa tatizo na kusahau ukuu wa Mungu. Tunauona mlima ulio mbele yetu lakini tunasahau njia ndefu ambazo tayari Mungu ametuvusha. Hakuna mlima unaofika angani, wala hakuna bahari iliyo kubwa kuliko Muumba wake.

Mungu wetu ni mkuu kuliko vyote vilivyo duniani na mbinguni. Kabla hajaviumba, “nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi.” Lakini Mungu alisema nuru iwepo, nayo ikawa. Hata giza linapoingia katika maisha yetu, Mungu anaweza kuliamuru na kulitoa nuru.

✍🏼Changamoto ni sehemu ya safari ya maisha. Usitazame tu mlima ulio mbele yako; kumbuka pia mabonde, dhoruba na njia ngumu ambazo tayari umezipita. Mungu aliyekuvusha wakati ule hajabadilika. Bado yupo pamoja nawe; hasinzii wala halali usingizi.

✍🏼Mungu ni mkuu kuliko njia unayopita, tatizo linalokusumbua na hofu inayotaka kuutawala moyo wako. Usipime uwezo wa Mungu kwa ukubwa wa tatizo lako; pima tatizo lako kwa ukuu wa Mungu wako.

✍🏼Kwa kuwa umeamka salama na umejaliwa uhai, mtie moyo aliyevunjika moyo, mwombee anayepitia njia ngumu, mshike mkono aliyeanguka, msaidie mwenye uhitaji na mpe tumaini aliyekata tamaa. Huenda unayolalamikia ni mambo ambayo mwingine anamwomba Mungu ayapate.

MUHIMU KUFAHAMU.,Usitazame ukubwa wa tatizo lako; mtazame Mungu aliye mkuu kuliko tatizo hilo. Mungu aliyekuvusha jana bado anaweza kukuvusha leo.

UTII HUFUNGUA MLANGO WA BARAKA ZA MUNGU"Na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata, usikiapo sauti ya BWANA, Mungu wako...
17/08/2026

UTII HUFUNGUA MLANGO WA BARAKA ZA MUNGU

"Na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata, usikiapo sauti ya BWANA, Mungu wako.”— Kumbukumbu la Torati 28:2

TAFAKARI

Mungu aliwaahidi wana wa Israeli baraka nyingi ikiwa wangesikiliza sauti yake, kushika maagizo yake na kutembea katika njia zake. Hata leo, Mungu anatuita katika maisha ya imani, utii na uaminifu.

🎚️Maneno “zitakujilia na kukupata” yanaonesha kuwa baraka za Mungu humfuata mtu anayeishi kwa kumtegemea na kumtii. Mungu hubariki maisha yetu katika namna mbalimbali:

●Hutubariki mjini na mashambani.
●Hubariki familia, watoto na kazi za mikono yetu.
●Hutupatia mahitaji yetu na kutufundisha kuwa baraka kwa wengine.
●Hutulinda tunapoingia na tunapotoka.
●Hutupa ushindi dhidi ya mipango ya adui.
●Hutufanya kuwa kichwa wala si mkia—kuwa juu wala si chini.

🎚️Utii si njia ya kumnunua Mungu, bali ni ushahidi wa upendo na imani yetu kwake. Baraka zake si mali pekee; zinajumuisha amani, afya, hekima, ulinzi, neema, mahusiano mema na uwezo wa kuvumilia nyakati ngumu.

MUHIMU KUFAHAMU KUWA 👉Usikengeuke kwenda kulia wala kushoto. Sikiliza sauti ya Mungu na utekeleze Neno lake. Iwe wewe ni mfanyakazi, mfanyabiashara, mkulima au mwanafunzi, mweke Mungu mbele katika yote unayofanya. Atakuongoza na kuibariki kazi ya mikono yako kwa kusudi lake.

Address

Singida

Website

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when Moravian Sabasaba Singida posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Shortcuts

Share

Category