03/04/2026
*Mambo 12 muhimu ya kutafakari leo katika mashtaka, mateso na hukumu ya kifo cha Yesu*"
1. *Mwamtafuta nani? Yesu Mnazareti- Ni Mimi*". Ujasiri wa kukiri na kujitambulisha wazi wazi hata kwa gharama ya maisha yetu. Je tuko tayari kukubali kuwa sisi ni Wakristo hata ikiwa tunatafutwa kuuawa au pengine tungekana k**a Petro, simjui mtu huyo, mimi si mkristo kabisa wala sijui kinachoendelea. "*Mkristo tambua cheo chako*
2. *"K**a mwanitafuta mimi waachieni hao waende zao*. Ujasiri wa kubeba msalaba peke yako bila kudai wengine au kutaka kufa na wengi wasio na hatia.
3. *"Rudisha Upanga alani kikombe alichonipa Baba sitokinywa*. Kukubali kuwajibika na kujitoa kwa ajili ya wengine bila kutafuta udhuru au kujihurumia. Mpokee mwenzio wa ndoa, watoto, wazazi, majirani na hata marafiki k**a dai la msingi la uwajibikaji na kujitoa sadaka kwa ajili yao.
4. *"Nimesema na watu waziwazi wala sikusema neno lolote kwa siri*. Je kuna tunayo yasema dhidi ya wenzetu kwa siri, masengenyo, fitina, majungu n.k
5. *"K**a nimesema vibaya, shuhudia ule ubaya, la sivyo kwanini wanipiga?* Wakati fulani kudai haki na uhuru wa kujitetea, usikubali kukaa kimya pale haki inapokurupushwa kwa kudhani ndiyo msamaha. Dunia huharabika pale watu wema wanapotambua kuwa ubaya unatendeka kisha wakakaa kimya na kuruhusu ubaya utamalaki
6. *"Wewe wasema kwa nafsi yako, au wengine wamekuambia habari zangu?* Tutoe nafasi ya kuwasikiliza watu na hata kuwafahamu kwa ukaribu na si kukurupuka na kutoa hukumu za mchongo.
7. "*Mimi nimekuja ili nishuhudie kweli na kila aliye wa kweli husikia sauti yangu*. Isivyo bahati dunia ya leo haitoi kabisa nafasi ya kutafuta, na kuujua ukweli na hata kushuhudia ukweli bali uongo na fitina vimechukua nafasi kubwa. Je unaamini katika kweli na kushuhudia kweli?
8. *"Wewe ungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu ungepewa toka juu,lakini ana dhambi kubwa zaidi aliyenitia mikononi mwako*. Je tunatumia vyeo, nafasi na vipato vyetu kuwanyanyasa wengine au ninakubali kitumiwa na wakubwa na matajiri kufanikisha uovu wao dhidi ya wengine?
9. "*Mama tazama mwanao, Mwana tazama mama yako*. Kumbuka hakuna mtu aishie kwa nafsi yake mwenyewe. Tunawajibika kwa wenzetu, tutambue utu wao, heshima yao, na mahitaji yao na tuwe tayari kuwasadia pale inapobidi
10. "*Naona Kiu*: Kiu ni dai au hamu ya jambo fulani muhimu au la lazima katika maisha. Nini kiu yako katika safari yako na hatima yake? Kukutana na Mungu au kuupata ulimwengu na fahari zake? Nafsi yangu inamuonea kiu Mungu, Mungu wangu aliye hai, k**a Ayala aoneavyao kiu nyua za maji, lini nitakapomuona Mungu? (Zab 42)
11."*Baba wasamehe kwa kuwa hawajui watendalo:* Msamaha ni tiba, kuachilia huponya maumivu, Upendo huvumilia yote, Upendo hauhesabu maovu, haulipi kisasi.
12. *"Yametimia*: Je natambua kuwa maisha ya hapa duniani yana mwisho, ninamalizaje safari hii? Mwisho wangu unanipa kibali cha kuishi na Mungu au yametimia katika upotofu na nimepoteza kila kitu. Itamfaidia nini mtu akiupata ulimwengu wote na kupata hasara ya nafsi yake?
Ndugu yenu
Padre Benedict Muk**a Luzangi