31/01/2021
Mhe. Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo ameongoza ibada ya Jumapili Usharika wa Sawe iliyokuwa na matendo mbalimbali leo tarehe 31.01.2021.
Kwanza alizindua shamba la miparachichi ambalo kwa mujibu wa risala iliyosomwa na Kiongozi wa Usharika Mch. Joseph Loti Shango lina ekari 3 na miti ya miparachichi zaidi ya 300.
Pili alifanya sala ya kuhamisha madhahabu ya kanisa la zamani ili kupisha ujenzi wa kanisa jipya.
Tatu aliweka wakfu kiti cha madhabahuni akaliacho kiongozi wa ibada.
Nne alihubiri Neno la Mungu toka Efe. 2:8-10 akisisitiza mambo yafuatayo:
Kwamba, neema ni kitu ambacho mtu anapewa bure bila kukitumikia, bila kukilipia na kinachompa nguvu ili asihangaike kujitafutia wokovu.
"Uhai tulionao, hewa tunayovuta, familia tuliyo nayo, na maendeleo tuliyo nayo tunawezeshwa na Mungu kwa neema yake tu sio kwa nguvu ama akili zetu. Hivyo, tuone umuhimu wa kumshukuru Mungu." Alisisitiza.
Wapo wanaoanza kazi lakini wasione matunda, wasifurahie matunda ya kazi yao. Yote inakuwa ubatili tu.
Tunapoanza kazi, kuona matunda, na kuyafurahia ni kwa Neema ya Mungu tu.
Neno linaeleza kuhusu wokovu tuliopata toka dhambi, mauti, laana, ufalme wa giza ama shetani, na toka hukumu ya milele ni kwa nguvu ya Mungu tu.
Tunapokea wokovu kwa njia ya imani kwa Yesu Kristo tu katika kumwendea kwa toba na kuamini kuwa kazi yake msalabani tunapokea wokovu.
Na hata kumwamini Yesu tunajaliwa na Mungu mwenyewe. Hatuna cho chote tunachoweza kuweka ili kupata wokovu.
Ni kweli kwamba hakuna wokovu kwa mwingine wala kingine ila kwa Yesu tu. Hivyo, asije mtu akajiisifu. Tunajenga kanisa, tunapiga tarambeta, na mambo mbalimbali, asije mtu akajisifu. Tunachotoa ni kumrudishia Mungu shukrani.
Waliopata wokovu, Wakristo, wanajua kumtegemea na kumtumikia Mungu kwa furaha.
Na hatupaswi kuwahukumu wengine bali tuwaombee na kumzalia Mungu matunda mema kwa kutumia vipawa tulivyojaliwa kufanya kazi ya Mungu, kutenda mema kwa jirani, shughuli za maendeleo ya jamii na kutunza uumbaji wa Mungu.
Tumeokolewa ili kutenda matendo mema, bali hatuokolewi kwa matendo hayo mema.
Alihitimisha kwa kupongeza washarika wa Sawe kwa kazi kubwa ya ujenzi wa kanisa jipya unaoendelea. Kazi hiyo ikiwa ni itikio lao la wokovu walioupata kwa neema tu. Ni kibali cha pekee ambacho sio vizazi vyote vinapata bahati hiyo.
Aliwaasa watu wote kuwa tunapita nyakati ambazo ni ngumu. Tusihofu kuendelea na kazi zetu, bali tuendelee kuomba na kuchukua tahadhari dhidi ya COVID-19.
Tano aliongoza harambee ya ujenzi wa kanisa jipya ambapo zilipatikana zaidi ya Tzs 62Milioni.
Mbali ya harambee hiyo ilitolewa shukrani maalumu ya kumshukuru Mungu kwa ajili ya harambee iliyopita hadi kufikia harambee hii nyingine ya ujenzi wa kanisa jipya.
Mwenyekiti wa jengo alitoa taarifa kuwa awali makisio ya ujenzi yalikuwa Tzs 300Milioni bali kwa kupanda kwa gharama mpaka sasa zimeshatumika Tzs 700M. Aidha, lengo la harambee hii leo ni kupata Tzs 100M kuendeleza kazi ya ujenzi huo.
Ibada ilihudhuriwa na Wana Sawe toka maeneo mbalimbali nchini na ilianza saa 4:00 asubuhi na kumalizika saa 11:45 jioni. Hizi ni baadhi ya picha za matukio hayo.