19/05/2026
JIFUNZE KUTAFSIRI MAUMIVU UNAYO YAPITIA.
Kunawakati unaweza ukapitia nyakati ngumu zakuumiza mno na ikapelekea kufanya maamuzi ambayo yanaweza kuleta madhara katika maisha yako yote, lakini nilikuwa ninatafakari na nikasema niseme na wewe ambaye unapitia maumivu makali muda huu na bado haujui namna ya kutoka kwenye hayo maumivu. Ni kweli unayopitia yanaumiza sana lakini natamani Mungu akakupe Neema ya kuyatafsiri maumivu yako kwa namna nyingine naamini hautayaona maumivu utauona ushindi mbele yako.
Si kila maumivu yanayokuja maishani mwako ni mabaya; kuna maumivu mazuri yanayolenga kukujenga, kukukomaza, na kukuvusha kwenda kiwango kingine cha baraka. Haya yanaitwa "Maumivu ya Ukuaji", hayakwepeki.
TUNAWEZA KUYATAFSIRI MAUMIVU KWA MAKUNDI K**A IFUATAVYO.
1. *Maumivu ya Kuzaa Jambo Jipya*
K**a vile mwanamke anavyopitia maumivu makali ili kuleta kiumbe kipya duniani, kuna maumivu unayoyapitia sasa kwa sababu kuna Ushuhuda Mkubwa unazaliwa ndani yako.
Yohana 16:21: "Mwanamke anapozaa huwa na huzuni kwa sababu saa yake imefika; lakini akiisha kuzaa mtoto, hakumbuki tena ule uchungu, kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtu ulimwenguni."
2. *Maumivu ya kusafishwa ili Uzae Zaidi*
Mkulima anapokata matawi ya mti, mti hupata maumivu, lakini lengo si kuuua, bali ni kuuongezea uwezo wa kuzaa matunda mengi na mazuri zaidi.
Yohana 15:2. "...na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa."
3. *Maumivu ya Kujenga Ustahimilivu na Tabia Njema*
Maumivu yanayotokana na majaribu na mapito magumu yanatengeneza misuli ya kiimani na kukupa hekima ambayo usingeweza kuipata ukiwa kwenye raha.
Warumi 5:3-4: "...tunaona fahari katika dhiki pia; tukijua ya kuwa dhiki huleta saburi; na saburi huleta uthabiti; na uthabiti huleta tumaini."
Yakobo 1:2-3: "Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu ya namna mbalimbali; mkitambua ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi."
4. *Maumivu ya Kukurejesha Kwenye Njia Sahihi*
Wakati mwingine Mungu anaruhusu upitie maumivu au kupoteza kitu ili akushtue uache njia mbaya inayoweza kukuangamiza. Haya ni maumivu ya marekebisho.
Zaburi 119:67.
"Kabla sijateswa mimi nalipotea,
Lakini sasa nimelitii neno lako."
5. *Maumivu ya Muda Mfupi Yanayotengeneza Utukufu wa Milele*
Maumivu yako ya sasa yana uzito mdogo sana ukilinganisha na uzito wa baraka, heshima, na utukufu ambao Mungu anakuandalia mbeleni.
2 Wakorintho 4:17.
"Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana;"
Kumbuka, tofauti ya maumivu mabaya na maumivu mazuri ni Kusudi lililopo nyuma yake. Maumivu mabaya yanakuja kuharibu, lakini maumivu mazuri yanakuja kukutengeneza kuwa bora zaidi.
Pastor Bampele Nathanael
GOOD NEWS CENTRE
MOROGORO