21/01/2020
IMARISHA NDOA YAKO SEHEMU YA ISHIRINI NA SITA
Karibu katika mfululizo wa masomo ya IMARISHA NDOA YAKO, somo lililopita tulianza sura ya TANO sehemu ya Ishirini na Tano yenye kichwa cha UMOJA UNAOIMARISHWA KWA MUME NA MKE KUWA SHIRIKA KATIKA FEDHA. Tuliishia kwa kusema hakuna haja ya kutengeneza maswali ya kujiuliza jinsi gani wanandoa wanaweza kuwa na umoja katika eneo la fedha kwa sababu hili si suala la elimu, halihitaji mtu aingine darasani na kujifunza maswali ya nadharia juu ya utatuzi wa migogoro ya kifedha katika ndoa. Hili linahitaji maswali ya vitendo ambayo yanaibuliwa na maisha ya wanandoa hao. Ni lazima yaibuke na ni lazima yapatiwe majibu kwa vitendo. Leo tutaendelea kujifunza sehemu ya Ishirini na Sita katika Sura yaTano ya somo hili.
I. Bila shaka, msingi wa umoja fedha katika ndoa ni jambo la muhimu sana, limezingatiwa kikamilifu katika falsafa ya Biblia kuhusu fedha. Wanandoa wa Kikirsto lazima wakubaliane na falsafa ya Bibiblia kuhusu fedha, si kwa sababu inafanya kazi au kwa sababu inatengeneza umoja wa ndoa yao, bali kwa sababu Mungu anataka wafanye hivyo. Wanandoa wakiamua kwa dhati kuchukua Biblia na kusoma falsafa au mwongozo wa Mungu kuhusu mapato na matumizi ya fedha wanazopata, hakika ndoa zitadumu, umoja utaimarishwa na uhasama au migogoro ya kifedha pamoja na ubinafsi wa wanandoa hao utakoma. Migogoro mingi ya kifedha katika ndoa inatokea kutokana na kukosekana kwa uelewa au elimu ya kiroho juu ya mapato na matumizi sahihi ya fedha, kila mmoja husoma biblia kwa kuangalia faida kwa upande wa maisha yake mwenyewe siyo kwa kuangalia maisha ya wote wawili (mume au mke).
Sasa hebu, tushiriki sote, mimi na wewe kujifunza msimamo wa Biblia (Mungu) kuhusu mapato na matumizi ya fedha, ili kanuni au falsafa hiyo itusaidie kumaliza tofauti zetu za mapato na matumizi ya fedha katika ndoa zetu;
A. Mungu ndiye aliyempa mtu uwezo wa kutengeneza fedha. Mungu ndiye anayempatia mtu utajiri na heshima, mume au mke anatakiwa kujua kuwa fedha au mali alizonazo amepewa na Mungu na anatakiwa ashirikiane na mwenzi wake kupanga na kutumia pamoja kwa sababu wao ni mwili mmoja, wameunganishwa na Mungu mwenyewe. Soma; Kumbukumbu la Torati 8:18, 1 Nyakati 29:11-12, Mithali 10:22 na 1 Wakorintho 4:7? Mume au mke hatakiwi kujivunia fedha zake kwa mwenzake, kwa sababu amepewa na Mungu ili watumie katika ndoa yao.
B. Kila tulicho nacho ni mali ya Mungu. Sisi (mume na mke) ni mawakili wa mali za Mungu, wanandoa wanatakiwa watumie rasilimali za Mungu ambazo amewapatia kwa kuomba na kwa uangalifu na uaminifu k**a Mungu atakavyo. Wanandoa wawe shirika katika kila kitu maishani mwao mpaka kifo kiwatenganishe zikiwemo fedha (Soma Zaburi 24:1 na 1 Nyakati 29:11, 14).
C. Kuna vitu vingi ambavyo ni vya thamani kuliko dhahabu au fedha. Kwa hiyo, usiuze upendo wako kwa mkeo au mumeo kwa sababu ya fedha, usivunje ndoa yako kwa sababu ya kutokuwa tayari kuwa shirika na mumeo au mkeo katika fedha, kwa sababu kufanya hivyo unamkosea Mungu pamoja na mume au mkeo. Unajitengenezea njia ya uharibifu. Kuweka kipaumbele fedha kuliko maagizo ya Mungu ya kumpenda mkeo au kumtii mumeo na kuwa mwili mmoja hakuwezi kukupeleka mbinginu kwa sababu fedha na mali ni vitu vya muda mfupi tu, kuna wakati wa kupanda na wakati wa kushuka kiuchumi lakini kwenye suala la upendo au umoja wa ndoa hakuna nyakati hizo za kuongeza upendo na kupunguza upendo au kuwa mwili mmoja (Soma vitabu hivi kwa msaada zaidi wa kiroho; Mathayo 16:26; 6:19-20, Luka 12:15,20-21, Mithali 15:16-17; 22:1; 19:1; 31:10; 19:14 na Zaburi 127:3,5. Pia kukosekana kwa hofu ya Mungu kwa mume au mke kunasababisha pia waingie katika majaribu na kutapanya fedha katika mambo ya anasa; soma 1Timotheo 6:6-9; 6:17-19. Ukiona mume au mke yupo tayari kutumia fedha kwa ajili ya mambo ya anasa ikiwemo uasherati na uzinzi ujue rohoni mwake ameharibika, amevamiwa na Ibilishi.
D. Tamaa mbaya, kukosa kiasi (kutokuridhika) na mashaka/woga katika kufanya maamuzi sahihi ya mapato na matumizi ya familia (makubaliano ya kuwa shirika katika fedha) ni dhambi. Kuna baadhi ya waume kwa wake wanawaka tamaa juu ya fedha za mwenzi wake na yupo tayari kumuua ili arithi mali au fedha, mume yupo tayari kumpoteza mke kwa sababu ya fedha, hiyo ni tamaa mbaya na ni dhambi, umoja wa ndoa hauwezi kupatikana. Mume na mke mnatakiwa muwe na kiasi, ridhikeni na aminiana ninyi kwa ninyi katika fedha zenu na kuweni na bajeti ya pamoja (mpange mapato na matumizi ya familia). Kila mmoja wenu ajue mnaingiza kipato kiasi gani kwa siku, kwa wiki, kwa mwezi na kwa mwaka na matumizi yenu ni kiasi gani kwa siku, kwa wiki, kwa mwezi na kwa mwaka pamoja na kuweka vipaumbele vyenu kwa pamoja (Soma, Kutoka 20:17, Luka 12:15, Mathayo 6:25, 31, 34, Wakolosai 3:5 na Waebrania 13:5).
Namshukuru Mungu kwa leo naishia hapo lakini ni matumaini yangu umefurahia somo hili na nikuahidi Mungu akipenda kipindi kijacho tutaendelea kujifunza sehemu ya Ishirini na Saba katika Sura yaTano ya somo hili yenye kichwa cha UMOJA UNAOIMARISHWA KWA MUME NA MKE KUWA SHIRIKA KATIKA FEDHA.
Jina langu naitwa Steward Dominicus Mkisi, a.k.a Baba Jebediah S. Mkisi na k**a una maswali, maoni au ushauri usisite kunitafuta kwa njia ya baruapepe [email protected] au nipigie kupitia simu ya mkononi +255764539949 au +255692485203
Mungu wa Mbinguni akubariki na tukutane Mungu akipenda kipindi kijacho, kwa herini na uwe na siku njema