23/09/2025
MSIMAMO WA KIBIBLIA KUHUSU UNYAKUO: HAKUNA TAREHE INAYOJULIKANA YA KURUDI KWA YESU
Utangulizi:
Katika nyakati hizi ambapo mafundisho mengi ya uongo yanazidi kuenea, ni muhimu kwa Kanisa kusimama imara katika kweli ya Neno la Mungu. Moja ya mafundisho muhimu katika imani ya Kipentekoste ni kuhusu kurudi kwa Yesu Kristo, maarufu k**a Unyakuo wa Kanisa. K**a waamini wa Biblia, tunatangaza kwa uhakika kwamba hakuna mtu yeyote anayeweza kujua tarehe wala saa ya kurudi kwa Bwana wetu Yesu Kristo.
1. Biblia Inafundisha kwamba Hakuna Anayeijua Siku wala Saa
Maneno ya Bwana Yesu mwenyewe yanathibitisha wazi kwamba tarehe ya kurudi kwake haijulikani:
“Lakini kuhusu siku ile au saa hiyo hakuna ajuaye, wala malaika wa mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake.”
(Mathayo 24:36)
Hii inatufundisha kuwa hatuna mamlaka ya kutangaza tarehe ya Unyakuo. Msimamo wetu wa Kipentekoste ni kwamba kudai kujua tarehe ya kurudi kwa Yesu ni kwenda kinyume na mafundisho ya moja kwa moja ya Biblia.
2. Kurudi kwa Yesu Kutakuwa kwa Ghafla K**a Mwizi ajavyo Usiku
Biblia inaeleza wazi kwamba siku hiyo itakuja kwa ghafla, bila onyo la moja kwa moja:
“Kwa maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana itakuja k**a vile mwivi ajavyo usiku.”
(1 Wathesalonike 5:2)
“Kwa sababu hiyo, ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani, Mwana wa Adamu yuaja.”
(Mathayo 24:44)
Kwa msingi huu, waamini wote wanapaswa kuishi kwa utakatifu na utayari, badala ya kutafuta tarehe au ishara zisizo za kibiblia.
3. Onyo Dhidi ya Mafundisho ya Uongo na Manabii wa Uongo
Bwana Yesu alionya juu ya wale watakaodai kuwa wanajua mahali au wakati wa kuja kwake:
“Na wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa; au, Tazama, yupo kule; msisadiki… angalieni, nimekwisha kuwaonya mambo yote.”
(Marko 13:21-23)
Mafundisho ya aina hii yanapotosha waamini na kuyumbisha imani ya wengi. Kipentekoste inasimama imara kupinga mafundisho ya aina hiyo, na kutetea uaminifu kwa maandiko matakatifu pekee.
4. Wito kwa Waamini: Kuwa Tayari Wakati Wote
Biblia haitupi tarehe ya Unyakuo, bali inatupa maagizo ya namna ya kujiandaa:
“Kesheni basi, kila wakati, mkiomba, mpate kuokoka katika hayo yote yatakayokuja, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu.”
(Luka 21:36)
“Na kila mtu mwenye matumaini haya katika Yeye hujitakasa, k**a Yeye alivyo mtakatifu.”
(1 Yohana 3:3)
Unyakuo sio wazo la kutisha kwa waaminio, bali ni tumaini kuu la waliokombolewa. Hivyo basi, tunapaswa kuishi kila siku kana kwamba Yesu anarudi leo.
HITIMISHO:
Kwa mujibu wa maandiko, Kanisa la Kipentekoste linaamini na kufundisha kwamba:
1. Kurudi kwa Yesu Kristo ni hakika na litakuwa kwa ghafula.
2. Hakuna mtu anayeijua tarehe wala saa ya Unyakuo.
3. Mafundisho yanayodai tarehe ni ya uongo na yapaswa kupingwa.
4. Waamini waitwe kuishi kwa utakatifu, maombi, na matumaini ya kila siku.
“Tazama, naja upesi; heri yeye azishikaye maneno ya unabii wa kitabu hiki.”
(Ufunuo 22:7)
Imetolewa na:
TANZANIA ASSEMBLIES OF GOD
KITENGO CHA TEOLOJIA NA FASIHI
Kwa Utukufu wa Mungu Pekee
Dr. Immaculate Nhigula-Mwenyekiti