15/10/2023
MCHUNGAJI MICHAEL KYAZEE KUTOKA UGANDA
SOMO: KUWA SALAMA NA KUWA MAKINI KATIKA MASUALA YA KIROHO
Ayubu 1:1-6 “Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu. Kisha walizaliwa kwake wana saba, na binti watatu. Mali yake nayo yalikuwa ni kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu,…….”
Ayubu alikuwa na familia na mali nyingi sana lakini pia kikubwa alikuwa anamcha Mungu.
Ayubu 1:6 -7 “Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao. Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo.”
Mkutano huu haukuwa duniani bali mbinguni, huu ulikuwa ni mkutano wa kiungu ambapo Mungu alikuwa anajadili mambo yanayohusu dunia.
Mungu alikuwa anatoa ushuhuda kuhusu habari za Ayubu, ya kuwa ni mcha Mungu, ndipo Mungu akamuuliza ibilisi unatoka wapi? Akasema “Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo”
Hii inamaana unapaswa kujua kuwa tunaishi huku duniani mahali pa vita, ibilisi yupo na anatembea kwa maana hiyo tunapaswa kuwa makini katika kuenenda kwetu ili tuweze kuwa salama.
Ayubu 1:9-10 “Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi.”
Kuna vitu vitatu ambavyo Mungu alivifanya kwa Ayubu:-
• Mungu aliweka uzio (ukigo) uliomzunguka Ayubu,
• Mungu aliweka uzio katika nyumba ya Ayubu (kwa wote walio nyumbani mwake).
• Uzio wa mali zake
Hii inamaana kuwa kuna maeneo matatu katika maisha yetu ambayo yanahitaji kuwekewa ulinzi (ukigo) wa kiroho, maeneo hayo ni:-
• Wewe mwenyewe unahitaji ulinzi wa kiroho
• Nyumba yako (watu wa nyumbani mwako)
• Vile unavyomiliki