Mwalimu Alex Mushi

Mwalimu Alex Mushi Yote Yanawezekana Kwake Aaminiye.

23/02/2025

SIKU 3 ZA KUFUNGA NA KUOMBA.

KUSHUGHULIKA NA MIUNGANIKO YA KIROHO-GIZA

SEHEMU YA KWANZA: MIUNGANIKO YA KIROHO-GIZA

“Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye.” 1 Wakorintho 6:17
Katika ulimwengu wa roho, unaweza kuungana na Bwana na ukawa roho moja naye au pia unaweza kuungana na nguvu za giza. Bwana Yesu alipotuokoa alikusudia tuungane naye, ili tuweze kuishi maisha ya ushindi, maisha yenye msaada kutoka kwake na tuweze kuzaa matunda yapasayo toba, maana bila Yeye sisi hatuwezi kitu (Yohana 15:5).
Ni wazi maisha ya wokovu bila muunganiko na Bwana, yanakosa matokeo halisi ya wokovu. Pengine maisha ya namna hiyo ni maisha fulani yanayotaka kufananishwa na wokovu lakini si maisha halisi ya wokovu uliokusudiwa na Bwana wetu Yesu Kristo.
Kuungana na Bwana hapa ninazungumza juu ya maisha ya kutembea katika neno la Mungu yaani neno linaongoza matendo yako, maneno yako na mara nyingine mawazo yako. Mtu wa namna hii anaishi ndani ya Yesu, au kwa lugha nyingine ameungana na Bwana na ni roho moja naye, na huyu ndiye mtu huzaa sana.
Sasa katika ulimwengu wa roho kuna pande mbili, upande wa nuru na upande wa giza. Upande wa nuru ni upande wa Bwana, na upande wa giza ni upande wa adui au shetani. K**a hujaungana na Bwana umeungana na upande wa shetani kupitia matendo yako, au matendo ya wahenga wako, kwa kujua au kwakutokujua.
Hivyo kule kuungana na nguvu za giza ndiko tunaita ‘miunganiko’ au ‘fungamano’ la kiroho-giza. Ninapozungumza kuhusu fungamano nina maanisha njia au mlango ambao shetani hutumia kuingiza uharibifu katika maisha ya mtu au katika familia yake. Maana pasipo fungamano shetani hawezi kupata ‘access’ ya kuingia katika maisha ya mtu.
Kwa hiyo unaweza ukawa ndani ya kanisa au wokovu lakini una fungamano la siri ambalo linakuunganisha na nguvu za giza bila wewe kujua. Kwa sababu shetani hufanya kazi kwa siri ili kuzuia asijulikane. Mtu atashangaa tu, anapita katika vita kubwa ya kiroho isiyoisha katika maisha yake. Ataomba sana, atafunga sana na mara nyingine atatoa sadaka sana lakini hakuna kinachobalika.
Shida hapa sio maombi, ama mfungo ama sadaka unazotoa ila ni fungamano ulilonalo. Linalotoa uhalali kwa shetani. Kwa lugha nyepesi una ‘kitu cha adui ndani kwako’, na hicho kitu ndiyo tunaita ‘fungamano’. Sasa Mungu ametupa neema ya kufunga na kuomba kwa ajili kujiondoa katika haya mafungamo, maana yake ametupa fursa ya kuondoa hivi vitu vya adui maisha ni mwetu ili tuweze kuwa na muunganiko uliosawa na Bwana.
Ni yangu imani kwamba katika maombi haya, Mungu atakwenda kuvunja na kukata kila miunganiko tulionayo na adui, tuliojiunganisha kwa kujua au kwakutokujua. Ndipo watu wengi katika mfungo huu wataweza kuvuka katika vita visivyoisha wanavyopigana kiroho. Weka imani kwa Mungu na bila shaka unakwenda kufunguliwa. Hongera kwa mfungo siku ya kwanza.
MAOMBI YA ASUBUHI NA JIONI.
1. Mshukuru sana Mungu kwa ulinzi, afya, na maisha yako kwa ujumla; pia mshukuru sana Mungu kwa kukuwezesha kushiriki mfungo huu wa siku tatu. (1 Nyakati 16:34)
2. Omba toba mbele za Mungu kwa matendo yote yasio mema uliowahi kutenda au yaliyotendwa na wazazi wako na yakakuunganisha na ufalme wa giza, k**a uchawi, ushirikina, uganga, matambiko, mazindiko, ibada za mizimu, uaguzi, zinaa, uganga wa kuchanjwa chale, na mengine unayoyakumbuka. (Yakobo 5:16)
3. Jiondoe kwa kutumia damu ya Yesu kwenye kila muunganiko wa kiroho-giza uliopo. (1 Kor 6:17)
4. Muombe Mungu akupe neema ya kuishi maisha ya muunganiko naye daima yaani neema ya kuishi sawasawa na neno lake siku zote ili: (Yohana 15:4-7)
• Uweze kuishi maisha yenye matunda (uzae sana)
• Uweze kutimiza kusudi uliloumbiwa
• Usije kutupwa nje kweney maisha ya mateso
• Uweze kuomba lolote kwa Mungu na ukapokea.
5. Ombea sana huduma hii ili iweze kufikia watu wengi zaidi katika maeneo zaidi k**a ilivyokufikia, pia niombe mwalimu wako ili Mungu anitunze siku zote kwa ajili ya kazi hii yake.

MAHUSIANO YA HALI YAKO YA KIROHO NA HALI YA UZAO WAKO.Na Mwal. Alex MushiNilikuwa kijana na sasa ni mzee, lakini sijaona...
07/11/2024

MAHUSIANO YA HALI YAKO YA KIROHO NA HALI YA UZAO WAKO.

Na Mwal. Alex Mushi

Nilikuwa kijana na sasa ni mzee, lakini sijaona kamwe wenye haki wameachwa au watoto wao wakiomba omba chakula.” Zaburi 37:25

Katika mstari wetu wa ufunguzi hapo juu, Daudi anatushudia kuwa katika kipindi alichoishi hajawahi kuona ‘kamwe’ mwenye haki ameachwa na Bwana au uzao wake kuwa ombaomba.

Daudi anamaanisha aliwahi kuona mwenye haki akipita katika nyakati ngumu, au katika mateso, au katika bonde la uvuli wa mauti lakini katika ugumu, mateso, na bonde la uvuli wa mauti alilopita Bwana hakumwacha, alimvusha alimshindia.

Kwa maneno mengine, wenye haki hupita nyakati hizo ngumu kwa kitambo kidogo tu, wakavuka, kwa sababu Mungu hana utamaduni wa kumwacha mwenye haki, maana anawapenda. Kwa hiyo kuwa mwenye haki ni tiketi ya kuvuta umakini wa Mungu katika maisha yako.

Zaburi 37:28 inasema “Kwa kuwa BWANA huwapenda wenye haki naye hatawaacha waaminifu wake. Watalindwa milele, lakini uzao wa waovu utakatiliwa mbali” Upendo wa Bwana kwa mwenye haki unamfanya asiwaache kamwe.

Kuwa mwenye haki, hakumfanyi tu Mungu kutokukuacha wewe bali hauachi pia na uzao wako. Ndicho Daudi anatushuhudia. Kwa hiyo, kumbe hali yako ya kiroho ya leo ina mchango wa moja kwa moja katika matokeo na hali ya uzao wako kesho.

Uzao wako unaweza kuachwa na Bwana na ukapita katika shida, mateso na mikosi isiyokoma kutokana na hali ya kiroho ya wazazi. Kumbe! Aina ya maisha unayoyachagua leo yana mchango kwa aina ya maisha ya uzao wako kesho.

Neno la Mungu linasema “lakini uzao wa waovu utakatiliwa mbali”; maisha ya uovu husababisha uzao wako ukataliwe, au kwa maneno mengine uharibiwe. Maisha ya uovu yataugharimu uzao wako.

Una nafasi kubwa ya kuyajenga maisha ya uzao wako kwa kuchagua kuwa mwenye haki. Maana kuwa mwenye haki kutauhakikishia uzao wako baraka. Uzao wako utapata kibali, uzao wako utaolewa na kuoa, utapata heshima, utairithi nchi, si kwa sababu ya usafi wao wa kiroho, Hapana! Ni kwa sababu ya msingi wa kiroho wa wazazi wao.

Kuwa mwenye haki ni kuamua kutembea pamoja na Mungu. Kuishi maisha ya kumcha Mungu. Kuondokana na maisha ya dhambi na michanganyo, kwa kifupi kuishi maisha matakatifu, maisha ya ibada, maisha ya maombi, maisha ya kusoma neno Lake. Amua sasa kwa faida yako na uzao wako.

🔥🔥🔥🔥🔥*DODOMA DODOMA DODOMA HUU NI MWAKA WA KUTEMBELEWA NA BWANA**HUDUMA YA UINJILISHAJI IMEAANDAA SEMINA KUBWA YA WAFANY...
31/10/2024

🔥🔥🔥🔥🔥

*DODOMA DODOMA DODOMA HUU NI MWAKA WA KUTEMBELEWA NA BWANA*

*HUDUMA YA UINJILISHAJI IMEAANDAA SEMINA KUBWA YA WAFANYAKAZI, WAFANYABIASHARA NA WAJASIRIAMALI*

*SEMINA HII ITAAMBATANA NA MAOMBI YA KINA YA KUFUNGUA LANGO LA UCHUMI*

*HII NI SEMINA YA KUFUNDISHA KANISA KANUNI ZA KUFANIKIWA KIUCHUMI KIBIBLIA*

*BWANA, mkombozi wako, mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Mimi ni BWANA, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata. Isaya 48:17*

*Tarajia kufundishwa na Bwana ili upate faida katika Biashara, Kazi, na Uwekezaji na shughuli zako zote za Uchumi*

*NISAIDIE KUSHARE TANGAZO HILI*

13/10/2024

*SIKU 7 ZA MAOMBI NA MFUNGO WA KUREJESHA VILIVYOIBIWA NA ADUIA*

*SIKU YA KWANZA: TUMRUDIE MUNGU KWA KUFUNGA ILI ATUREJESHEE*

Na Mwal. Alex Mushi

“Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa KUFUNGA, na kwa KULIA, na kwa KUOMBOLEZA.” Yoeli 2:12

Maneno hayo hapo juu ni maneno ambayo mjumbe wa Mungu aliambiwa kuwaambia nyumba ya Yuda. Ni tangazo la kumrudia Mungu kwa nyumba ya Yuda ili vikwazo walivyokuwa navyo viondoke katika nchi yao na kurejesha ushirika wao uliovunjika na Mungu.

Watu hawa walimwasi Mungu, dhambi ikawaweka mbali na Mungu, na kuufunga Uchumi wao kabisa. Maana nchi ilishambuliwa na jeshi kubwa la nzige, hakukusalia na chochote, Biblia inasema “Mashamba yameharibiwa, ardhi imekauka, nafaka imeharibiwa, mvinyo mpya umekauka, mafuta yamekoma.” Yoeli 1:10

“Kilichosazwa na kundi la tunutu nzige wakubwa wamekula, kilichosazwa na nzige wakubwa parare wamekula, kilichosazwa na parare madumadu wamekula.” Yoeli 1:4 Jeshi hili lilimaliza kila kitu. Na ndivyo inavyokuwa pale dhambi inapokuwa hemani mwetu. Inashambulia kila kitu.

Tunapomwasi Mungu na kuabudu miungu katika familia zetu, kwa matambiko, mila Kwenda kwa waganga, na ibada za kimizimu, tunakaribisha jeshi la mapepo kutafuna kila kitu katika maisha yetu. Hata kile kilichosalia ambacho tunaona ni tumaini nacho si muda kinasambaratishwa.

Maisha ya mateso na taabu hayakujii kwa bahati mbaya, bali nyuma yake kuna sababu. Na sababu ni hiyo ya uasi dhidi ya Mungu. Hivyo k**a matokeo ya kuasi, unaingia katika vifungo na upotevu wa baraka zako katika maisha.

Kwa hiyo unamruhusu shetani kuiba na kuchukua kilicho chako. Mfungu huu, ni mwito wa Mungu akitaka ujinyenyekeshe mbele zake kwa toba, ili upate kumrudia. Ni mfungo unaohitaji imani dhabiti, ya kuamini ya kwamba Mungu wetu ni Mungu wa UREJESHO.

Hivyo dhamiria kweli kumrudia Mungu kutoka moyoni, si suala la kufuata mkumbo. Hapana! Dhamiria haswa kumrejea Bwana. Ukisikia kulia mbele za Bwana na hasa wakati wa maombi fanya hivyo, maana haya ni maombolezo.

Kuomboleza ni kuomba kwa kusihi na kuugua juu ya hali iliyopo. Kwa wengi hali si shwari, mambo magumu, furaha ya maisha imekatika hakuna hali nzuri katika kila eneo la maisha. Hakuna ndoa, hakuna uchumi mzuri, hakuna maelewano baina ya ndugu. Kwa hiyo lazima uomboleze.

Mungu amekupa mfungo huu ili kuomba rehema zake maana yeye ni mwingi wa rehema na pia anataka kurejeshea vyote vilivyopotea kwa muda wote ambao umeshambuliwa na jeshi la adui. Anasema “Nami nitawarudishia hiyo miaka iliyoliwa na nzige na parare, na madumadu na tunutu..” Yoeli 2:25.

Mungu wetu ni mungu wa urejesho, na Mungu anayetimiza ahadi yake. Jinyenyekeze kwake kupitia mfungo huu ili apate kutimiza ahadi yake ya urejesho kwa mtoto wake. Hivyo basi tarajia makubwa katika mfungo huu. Tarajia kupokea tena yale yaliyoshindikana katika maisha yako. Hongera sana kwa mfungo siku ya kwanza.

*MAOMBI YA ASUBUHI NA JIONI*

1. Jongea mbele za Mungu kwa shukrani. Mshukuru Mungu kwa mfungo huu ambao ametupa kwa ajili ya kurejesha vyote vilivyoibiwa na adui (Yoeli 2:25)

2. Nenda mbele za Mungu omba toba ya kina kwa ajili ya yote yasiyo haki ambayo yametendwa katika familia au ukoo wako, kwa unayoyajua na usiyoyajua (matendo 3:19):
 Omba toba kwa matambiko, mila mbaya na mazindiko, ibada za mizimu na matendo ya kishirikina mliofanya na ukashiriki.
 Omba toba kwa kila ibada ya kimiungu iliyofanyika katika familia au ukoo wako.
 Omba toba kwa kwenda kwa waganga na kupelekea kuchanjwa, kupakwa au kunywa akulishwa madawa yao.
 Omba toba kwa ajili kila sadaka iliyotolewa kwenye madhabahu za giza kwa kujua au kutokujua.

3. Soma zaburi yote ya 51 ili kuomba reheme kwa MUngu kwa ajili yako na familia yako.

4. Omba Mungu akupe moyo wa kumpenda yeye peke. Omba Mungu akupe moyo wa kusali, moyo wa ibada, moyo wa kusoma neno na Moyo wa kufunga siku zote.

5. Ombea huduma hii ya NENO LA UZIMa ili iweze kuwafika watu wengi zaidi duniani.

*KWANINI USHIRIKI MAOMBI NA MFUNGO WA SIKU SABA ZA UREJESHO*Mungu wetu ni Mungu wa Urejesho, ni Mungu wa nafasi nyingine...
12/10/2024

*KWANINI USHIRIKI MAOMBI NA MFUNGO WA SIKU SABA ZA UREJESHO*

Mungu wetu ni Mungu wa Urejesho, ni Mungu wa nafasi nyingine, haijalishi umepoteza na umeibiwa nini na shetani, bado Mungu anaweza kukurejeshea, ndiyo maana katupa mfungo wa siku saba wa Urejesho.

Biblia inasema “Nami nitawarudishia hiyo miaka hiyo miaka…” Yoeli 2:25 hii ikiwa na maana wako watu wengi wameshindwa kuingia katika baraka zao kwa sababu kuna miaka yao imeliwa na adui.

Umepoteza miaka mingi kwa sababu ya hila za shetani, umepoteza mali zako kwa sababu ya hila za shetani, umepoteza tumaini lako kwa sababu ya hila za shetani, lakini Mungu sasa ametupatia mfungo maalumu kwa ajili ya kurejesha vyote ambavyo umevipoteza.

Kwahiyo katika mfungo huu funga kwa imani na tarajia makubwa kutoka kwa Mungu kupitia mfungo huu. Usiingie katika mfungo huu ukibahatisha, Hapana! Ingia kwa imani maana Mungu anakwenda kukushangaza katika maisha yako.

Huu ni mfungo wa Mungu kurejesha ndoa yako, kurejesha Uchumi wako, kurejesha kazi yako, kurejesha afya yako, kurejesha kibali chako, kurejesha ukuu wako, kurejesha uzazi wako ulioibiwa na adui kwa muda mrefu. Tarajia makubwa!

Sauti hii ya mfungo ni sauti ya Mungu ikitaka uitikie wito ili Mungu apate kurejesha vyote. Kwa Mungu kurejesha haina maana ya kupata ulichopoteza tu, bali ni kupata maradufu. Mungu atakurejeshea zaidi ya ulivyopoteza maana sharti mwizi akipatikana atalipa mara saba (Mithali 6:37).

Biblia inasema “Bwana naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza” Ayubu 42:10 hii ina maana yale yaliyopote katika maisha yako hayatarejea k**a yalivyokuwa bali utayapata mara mbili zaidi k**a Ayubu alivyopewa.

Kushiriki mfungo huu hakikisha unafuatilia mwongozo wa mfungo katika group letu la whatsapp. K**a hujajiunga kwenye group letu la Whatsapp tuma ujumbe kwenye 0756 364075.

Au Bofya Link hii Kujiunga kwenye Group:

https://chat.whatsapp.com/CcHllvcHH4z8zNmg7GTg8H

*WEKA JUHUDI KATIKA MAARIFA YA MUNGU ILI UMWONE BWANA AKITENDA MAISHANI MWAKO.*Maarifa ni nyenzo muhimu ya kiroho, maana...
25/09/2024

*WEKA JUHUDI KATIKA MAARIFA YA MUNGU ILI UMWONE BWANA AKITENDA MAISHANI MWAKO.*

Maarifa ni nyenzo muhimu ya kiroho, maana ndiyo yanayomruhusu Mungu kutenda katika maisha yako. Ukubwa na upana ambao Mungu ataonekana katika maisha yako unategemea sana kiwango cha maarifa kumhusu ulichonacho.

Bidii pekee kwa ajili ya Mungu pasipo maarifa haina maana. Watu wengi wana juhudu kubwa kwa ajili ya Mungu lakini hawana maarifa ya kutosha kumhusu huyo Mungu wanayemwekea juhudi, na kwa sababu hiyo wamekwama.

Paulo alisema hivi juu ya Warumi “Kwa maana ninaweza nikashuhudia wazi kwamba wao wanajuhudi kubwa kwa ajili ya Mungu, lakini juhudi yao haina maarifa.” Warumi 10:2 Hapa Paulo alikuwa na maana kwamba hawa watu waliwekeza juhudi katika kumtumikia Mungu lakini si katika maarifa ya kumjua wanayesema wanamwekea juhudi.

Kwa kifupi hakuna mbadala wa maarifa ya Mungu. Huwezi kufunika ujinga wa kiroho kwa maombi mengi, ukadhani Mungu atapotezea ujinga ulionao. Huwezi kufunika ujinga wa kiroho ulionao kwa kutoa sana, au kushinda muda wote kanisani, la hasha!

Yesu anataka uwekeze juhudi zako katika maarifa yatakayokufanya umjue Yeye. Ndicho ambacho Yesu alimwambia Martha dadaye Mariamu, baada ya kumwona ameweka juhudi kwa ajili ya Mungu na kushindwa kukaa katika neno la Mungu na kujifunza k**a Mariamu.

Ndiyo maana Yesu akamwambia Martha “Martha,Martha, mbona unasumbuka na kuhangaika na mengi? Lakini kunahitajika kitu kimoja tu. Maria amechagua kile kilicho bora, wala hakuna mtu atakayemwondolea.” Luka 10:41-42

Kuchagua kupata maarifa ya Mungu, ni kuchagua kilicho bora, ni kuchagua fungu jema ambalo hutaondolewa. Kaa chini ujifunze neno la Mungu upate maarifa acha kuangaika na kujisumbua kwa utumishi mwingi ukidhani ndio njia ya kumpendeza Mungu.

Utalalamika kila mara humwoni Mungu katika maisha yako, pamoja na utumishi mwingi unaoufanya kanisani kwa ajili ya Mungu, kumbe unafanya hayo yote pasipo maarifa ya Mungu. Wekeza juhudi yako kujifunza neno la Mungu.

Tunafundisha kwa kuandika na kwa sauti kila siku ili upate maarifa ya Ki-Mungu kwa sababu tunajua ndiyo sehemu itayokusaidia kutembea na Mungu. Jifunze neno Lake upate maarifa yake ili usiangamie!

Ubarikiwe sana, nakutakia siku njema!

Mwal. Alex Mushi
0756 364 075.

*MFUNGO WA SIKU 3 WA KUVUNJA VIFUNGO.**SIKU YA PILI: KUVUNJA VIFUNGO VYA KURITHI*Na Mwal. Alex Mushi“ Je! Saumu niliyoic...
16/09/2024

*MFUNGO WA SIKU 3 WA KUVUNJA VIFUNGO.*

*SIKU YA PILI: KUVUNJA VIFUNGO VYA KURITHI*

Na Mwal. Alex Mushi

“ Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza Kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?” Isaya 58:6

K**a tulivyosema katika sehemu ya kwanza kwamba vifungo ni vizuizi vya kiroho vinavyomzuia mtu kutembea kwa uhuru au kusonga mbele katika safari yake ya maisha. Vifungo ni k**a kuta za kiroho zinazomwekea mtu mpaka kati yake na baraka zake kutoka kwa Mungu. Hata k**a mtu huyo atafanya bidii na jitihadi mbalimbali lakini hawezi kupiga hatua au kuwa huru kufanya anachotamani.

Sasa vifungu hivi vingine ni vifungo vya kurithi kutoka kwa wazazi au ukoo. Unakuta mtu anasumbuliwa na baadhi ya tabia mbaya ambayo ukiichunguza utagundua ameirithi kutoka kwa wazazi wake, na tabia hiyo inamtesa kwa maisha yake yote. Mfano mtu anasumbuliwa na tabia za uzinzi, ulevi, kuoa mitala, hasira na tabia nyingine k**a hizo lakini akijikagua anagundua wazazi au babu au bibi zake pia walikuwa na tabia hizo hizo.

Biblia inasema “Kwa maana mnafahamu kwamba mlikombolewa kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mliurithi kutoka kwa baba zenu, si kwa vitu viharibikavyo, yaani, kwa fedha na dhahabu, bali kwa damu ya thamani ya Kristo, k**a ile ya Mwana-Kondoo asiye na dosari wala doa.” 1 Petro 1:18-19. Andiko hili linaonyesha kuna mienendo ambayo unaweza kuirithi kutoka kwa wazazi wako na ikawa kizuizi kwa wewe kusimama vile unataka.

Lakini tumaini ni kwamba pamoja na kwamba kuna mienendo umerithi kutoka kwa wazazi, Yesu alimwaga damu yake kwa ajili ya kukukomboa kutoka kwenye hiyo mienendo. Ni vyema kujua pamoja na kwamba tunazaliwa mara nyingine tukifanana kwa nje na wa wazazi wetu, lakini kuna vingi ambavyo havionekani pia tunarithi kutoka kwa wazazi hao ambavyo vinaweza kuwa vizuri au vibaya. Mojawapo ya tunavyoweza kurithi ni tabia au mwenendo mbaya ambao imekuwa ni kifungo.

Kadhalika kuna vifungo pia tunarithi moja kwa moja kutoka kwenye koo zetu kutokana na yale yaliyotendwa na wale waliotutangulia. Mfano unaweza kusoma mstari huu “Hapatakuwa na Mwamori au Mmoabu au ye yote wa wazao wao atakayeruhusiwa kuingia katika kusanyiko la BWANA, hata mpaka kizazi cha kumi.” Kumbukumbu 23:3. Mstari huu unaonyesha kwamba karibu vizazi kumi vya koo hizi za Mwamori na Mmoabu vinakatazwa kuingia kwenye kusanyiko la Bwana kwa kosa walilofanya mababu zao.

Unaweza kuzaliwa katika ukoo k**a huo ukajitaidi sana kumtumikia Mungu lakini ikashindikana kabisa na usijue sababu. Ukafanya kila aina ya juhudi lakini ukakwama. Kumbe kuna kifungo ambacho umerithi kwa kuzaliwa kwenye hiyo familia. Usipotambua hilo na kufanyia kazi utaendelea kukwama.

Kwa hiyo, mfungo wetu huu ni maalumu kabisa kwa ajili ya kuhakikisha vifungo vya namna hii vinavunjika maana Biblia inasema Israeli walipomlilia Mungu aliwatoa katika mateso yao na kuyavunja mafungo yao (Zaburi 107:13-14). Hii ina maana katika maombi yetu haya Mungu anaweza kuvunja vifungo vyetu ambavyo tumerithi.

Kwa sababu saumu ambayo Mungu ameichagua ni ya “Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza Kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira” kwa hiyo kuwa na tumaini ya kwamba baada ya mfungo huu utatembea katika uhuru wako maana Mungu atatenda na kila kilichokuzuia kitaondoka.

*MAOMBI YA ASUBUHI NA JIONI*
1. Ingia mbele za Mungu kwa moyo wa shukrani kwa siku nyingine ya mfungo ambayo Bwana kakupa. Shukuru kwa yote kwenye maisha yako, kwa mabaya na mazuri (1 Thes 5:18)
2. Omba toba kwa yale yote ambayo yalitendwa na waliokutangulia kwenye ukoo wako na kusababisha na ninyi kurithi mienendo yao mibaya ( Mdo 3:16).

3. Tumia damu ya Yesu kufuta tabia zote mbaya ambazo unaona zinafanya kazi katika ukoo na famili yako, ni uzinzi, ulevi, kuoa mitala, hasira, chuki, wivu na tabia nyinginezo (1 Petro 1:18-19)

4. Vunja kwa jina la Yesu vifungo vyote ambavyo ulirithi kutoka kwa wazazi au ukoo. Ni vifungo vya kutooa au kutoolewa, vifungo vya umaskini, kutojenga, kutokuzaa na vinginevyo vunja kwa jina la Yesu.

5. Omba Mungu akusaidie utoke kwenye tabia mbaya ambazo unaona zinakugharimu kiroho. Fanya ombi hili ukimsihi Mungu akusaidie kutoka kabisa (Isaya 58:6)

6. Ombea nchi ya Tanzania iwe na amani, kemea roho zote za mauaji na utekaji unaoendelea katika nchi yetu. (Mithali 14:34).

*MFUNGO WA SIKU 3 WA KUVUNJA VIFUNGO.**SIKU YA KWANZA: VIFUNGO NI VIZUIZI VYA KIROHO*Na Mwal. Alex Mushi“ Je! Saumu nili...
16/09/2024

*MFUNGO WA SIKU 3 WA KUVUNJA VIFUNGO.*

*SIKU YA KWANZA: VIFUNGO NI VIZUIZI VYA KIROHO*

Na Mwal. Alex Mushi

“ Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza Kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?” Isaya 58:6

Vifungo ni vizuizi vya kiroho ambazo humfanya mtu kukwama asisogee, asivuke hatua fulani katika maisha, au asiende kwa ukubwa na umbali anaostahili. Mtu anapambana na kuweka juhudi ili aongezeke kihatua katika nyanja fulani ya maisha lakini kwa sababu ya vifungo haendi wala hasongi popote.

Pia tunaweza kusema vifungo ni vizuizi vya kiroho ambavyo humfanya mtu asiweze kufanya jambo kwa uhuru. Yaani unapambana kufanya jambo fulani ambalo una uhakika ni muhimu katika maisha yako na ukilifanya litakuletea matokeo makubwa lakini kila ukijaribu kulifanya huwezi unaishia njiani au huwezi kulifanya kabisa.

Sasa k**a matokeo ya vifungo, watu wanakata tamaa ya maisha na kujiona wasio na bahati katika maisha, na kupelekea watu kuridhika na maisha ya udogo na ya uwastani ambayo wameyafikia kutokana na vifungo. Wengine kutokana na vifungo wamepoteza kabisa imani zao kwa Mungu maana wanaona pamoja na jtihada zote walizoweka kwenye maisha bado wamekwama.

Kwa hiyo vifungo ni vibaya sana katika maisha ya mwamini, hasa katika eneo la kuongezeka na kutenda yale yalio mema. Watu wanakwama katika hatua moja bila kujua sababu; na wengine wamekwama katika kufanya jambo fulani kwa sababu ya vifungo. Unaweza usijue k**a hivi vifungo pia vinatenda kazi ndani yako. Lakini kuna njia rahisi ya kujikagua na ukajua.

Angalia ni eneo gani la maisha ambalo umeweka jitihada za kutosha lakini halizai matunda, au angalia ni eneo gani la maisha ambalo unatamani kulibadilisha lakini inashindikana? Yaani una shauku ya kubadilika katika hilo eneo na unaweka mikakati lakini inashindikana, na umefanya zaidi ya mara moja, mara mbili, mara tatu lakini bado imeshindikana kuleta badiliko.

Ni eneo la biashara, unafanya kwa bidii kubwa lakini hufanikishi, unafanya unabadili mbinu, au unabadili bishara lakini bado hutoboi? Au ni eneo la uchumba, umejitahidi kuwa bora uwezavyo ili kubakisha mahusiano yako lakini kila uchumba unavunjika na haufanikiwi kuingia kwenye ndoa? Au ni eneo la fedha, umekuwa ni mtu wa madeni tu, umejaribu kutoka lakini bado umeng’ang’niwa, ijapo tabia hiyo inakuchukiza sana sana!

Sikia! Vyote hivyo ni vifungo. Havionekani lakini matokeo yake utayaona kwenye maisha yako. Vifungo ni kamba au kuta au mipaka ya kiroho ambayo mtu huwekewa na shetani ili asivuke na kushuhudia neema na baraka za Mungu katika maisha yake. Vifungo hivi havishughulikiwi kimwili ila kiroho maana na vyenyewe ni vya kiroho.

Mstari wetu wa ufunguzi hapo juu unaweka bayana, kwamba moja ya nyezo ya kiroho ambayo Mungu ametupa kuvunja na kufungua vifungo hivi ni KUFUNGA. Kufunga au Saumu kazi yake moja wapo ni kufungua vifungo vya uovu. Vifungo ambavyo shetani ameweka katika maisha yako. Au kufungua tabia ovu ambazo zimekufunga ili usiiendee njia safi ya Mungu.

Kwa hiyo ‘NIA’ ya mfungo wetu wa siku tatu ni kuvunja vizuizi hivi vya kiroho ili tuvuke, tusonge, na kuenenda kwa uhuru ambao Bwana ametukusudia. Nikutie moyo kwamba kila kifungo ambacho unahisi kimekwamisha maisha yako Bwana anakwenda kukivunja maana hiyo ndio moja ya kazi ambayo Yesu alikufa kwa ajili yake.Weka imani yako kwa Bwana na jenga matarajio makubwa ya kupokea kufunguliwa katika mfungo huu.

HONGERA SANA KWA MFUNGO SIKU YA KWANZA. TUONANE SIKU YA PILI. HAKIKISHA UNAOMBA KWELI KWELI KUVUNJA VIFUNGO HIVI K**A MAELEKEZO YALIVYO HAPO CHINI.

*MAOMBI YA KUOMBA ASUBUHI NA JIONI*

1. Mshukuru sana Mungu kwa kukuwezesha kufunga mfungo wa siku tatu, kumbuka si kwa uwezo wako bali ni kwa neema yake. ( 1 Mambo ya Nyakati 16:34)

2. Ingia kwenye maombi vunja na sambaratisha vifungo vyote unavyoviona katika maisha yako katika kila eneo: katika Uchumi, mahusiano, ndoa, afya, maendeleo, ujenzi, mafaniko na maeneo mengineo. (Isaya 58:6)

3. Amuru roho zote za giza (mapepo, majini, mizimu) zilizo nyuma ya vifungo ulivyonavyo zikuachia kwa Damu ya Yesu. (Ufunuo 12:11)

4. Futa mipaka yote ya kiroho uliyochorewa na vunja kuta zote za kiroho uliwekewa k**a kizuizi katika njia yako ya kusonga mbele. (Ayubu 38:11)

5. Ombea huduma hii ili iweze kuwafikia watu wengi zaidi na waokolewe, niombe na mimi k**a kiongozi wake ili niweze kutembea na Mungu siku zote za maisha yangu, ombea familia yangu pia.

6. Funika kila kitu chako kwa Damu ya Yesu. Na mshukuru Mungu kwa ajili ya mfungo siku ya kwanza. (1 Wathesalonike 5:18)

Tushiriki wote mfungo huu muhimu kwa hatua zaidi za kiroho katika maisha yako. Popote ulipo unaweza kuungana nasi kufung...
14/09/2024

Tushiriki wote mfungo huu muhimu kwa hatua zaidi za kiroho katika maisha yako. Popote ulipo unaweza kuungana nasi kufunga, maana Muongozo na mafundisho utayapata ulipo kupitia group la Whatsapp. Kujiunga na group la mfungo tuma jina lako wahtsapp kwa namba hii 0756364075.

Mungu Ametubariki kwa zawadi ya utumishi uliotukuka katika Kanisa wa Baba yetu Askofu Mkuu Mstaafu Josaphat Lebulu. Amet...
20/08/2024

Mungu Ametubariki kwa zawadi ya utumishi uliotukuka katika Kanisa wa Baba yetu Askofu Mkuu Mstaafu Josaphat Lebulu. Ametoa Maisha yake kwa Ajili ya Injili, yaani pamoja na Umri Mkubwa alionao lakini anachapa Injili Kwa Ujasiri na Nguvu Kubwa sana. Hili funzo na darasa Kubwa Kwetu Vijana. BABA, MUNGU AKUPE MAISHA MAREFU ZAIDI NA ZAIDI.

TUKUTANE KATIKA KONGAMANO LA INJILI KWA WATU WOTE MWAKANI 2025.

MAISHA YA WATU YANAENDELEA KUGUSWA KWA NGUVU YA INJILI INAYOENDELEA KUHUBIRIWA KATIKA KONGAMANO LA INJILI.
16/08/2024

MAISHA YA WATU YANAENDELEA KUGUSWA KWA NGUVU YA INJILI INAYOENDELEA KUHUBIRIWA KATIKA KONGAMANO LA INJILI.

Address

Inukamtanzania. Blogspot. Com
Dodoma
255

Telephone

+255735364075

Website

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when Mwalimu Alex Mushi posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Share