24/07/2026
MADA: VITU VINAVYOZUIA KUSUDI LA MUNGU KUTIMIA AU KUCHELEWA KWA VIJANA
(Kusudi likimaanisha wito, huduma, karama, kipawa, taaluma, biashara au kazi ambayo Mungu amemwandalia mtu.)
UTANGULIZI
Mungu hamuumbi mtu kwa bahati mbaya. Kila kijana ana kusudi maalumu aliloliweka ndani yake kabla hajazaliwa. Kusudi hilo linaweza kujidhihirisha kupitia huduma, taaluma, biashara, kazi, uongozi, kipawa au karama.
Hata hivyo, si kila kijana hufikia mwisho wa maisha akiwa ametimiza kusudi hilo. Wengine hulichelewesha, wengine huliacha kabisa, na wengine hufanya mambo mengi mazuri lakini ambayo hayakuwa mapenzi ya Mungu kwa maisha yao.
Ni muhimu kuelewa kuwa si kila jambo jema ndilo kusudi la Mungu. Unaweza kuwa na kazi nzuri, biashara kubwa au taaluma yenye mafanikio, lakini k**a haiko katika mpango ambao Mungu amekuwekea, bado unaweza kuwa unaishi nje ya kusudi lake.
Ndiyo maana jambo la kwanza si kujiuliza, "Nifanye nini?" bali, "Mungu anataka nifanye nini?"
Maandiko ya Msingi
Waefeso 2:10
"Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo."
Yeremia 1:5
"Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua; na kabla hujatoka tumboni nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa."
1. KUTOKUJUA KUSUDI LA MUNGU NDANI YA MAISHA YAKO
Maandiko
Hosea 4:6
"Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa."
Waefeso 5:17
"Basi msiwe wajinga, bali mfahamu mapenzi ya Bwana ni nini."
Ufafanuzi
Kikwazo kikubwa kwa vijana wengi si kukosa uwezo, bali kutokujua kusudi la Mungu juu ya maisha yao.
Wengi huchagua taaluma, biashara, huduma au kazi kwa sababu ya fedha, ushawishi wa marafiki, familia au mazingira. Lakini Mkristo anatakiwa kuhakikisha kila anachofanya kinaendana na mapenzi ya Mungu na kinamtukuza Mungu.
Si kila nafasi nzuri ndiyo kusudi lako.
Si kila biashara ndiyo wito wako.
Si kila huduma ndiyo mahali Mungu amekupanga.
Mungu ndiye anayejua sababu ya kukuumba, hivyo ni lazima umtafute ili akuonyeshe njia yako.
Mfano wa Biblia
Sauli wa Tarso alikuwa na bidii kubwa lakini alikuwa katika mwelekeo usio sahihi. Alikuwa analitesa Kanisa akidhani anamfanyia Mungu kazi.
Alipokutana na Yesu njiani kwenda Damasko ndipo alipotambua kusudi lake halisi na kuwa mtume wa Mataifa (Matendo 9:15–16).
Mfano wa maisha
Kijana anaweza kusomea Uhasibu lakini Mungu amemkusudia kuwa mwalimu wa Neno, mwinjilisti, mfanyabiashara au mjasiriamali atakayebadilisha maisha ya wengi. Bila kumtafuta Mungu, anaweza kutumia maisha yake yote kwenye jambo ambalo si kusudi lake.
Funzo
Usiombe Mungu akubariki tu katika unachofanya; omba akuonyeshe kile anachotaka ufanye.
2. HOFU YA KUITIKIA KUSUDI LA MUNGU NA KUAHIRISHA KUANZA
Maandiko
2 Timotheo 1:7
"Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi."
Mhubiri 11:4
"Auangaliaye upepo hatapanda."
Ufafanuzi
Vijana wengi tayari wanajua Mungu anawaita kufanya jambo fulani, lakini hofu huwafanya wasianze.
Wengine wanaogopa kukataliwa.
Wengine wanaogopa kushindwa.
Wengine wanaogopa kukosolewa.
Wengine wanasema:
"Nikishapata fedha nyingi..."
"Nikimaliza masomo..."
"Nikioa..."
"Nikistaafu..."
Mwisho wa yote, hofu huzalisha kuahirisha, na kuahirisha huzalisha miaka mingi ya kutofanya chochote.
Mungu hawaiti watu kwa sababu wamekamilika; huwakamilisha wale wanaoitikia wito wake.
Mfano wa Biblia
Yeremia alisema:
"Mimi ni mtoto."
Lakini Mungu akamwambia:
"Usiseme, Mimi ni mtoto... usiogope." (Yeremia 1:6–8)
Yona naye alikimbia wito wake akidhani angeuchelewesha. Mwishowe alijifunza kwamba hakuna anayeweza kukimbia kusudi la Mungu bila gharama.
Mfano wa maisha
Kijana ana kipawa cha kuhubiri, kuimba, kuandika vitabu au kuanzisha biashara, lakini kila mwaka anasema:
"Nitaanza baadaye."
Miaka inapita huku kusudi likisubiri.
Funzo
Anza na kile ulichonacho leo. Mungu hubariki hatua ya imani kuliko visingizio vya kusubiri.
3. KUKOSA MAANDALIZI YA KUSUDI
Maandiko
Luka 16:10
"Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana huwa mwaminifu pia katika lililo kubwa."
Mithali 22:29
"Je, wamwona mtu mwenye bidii katika kazi yake? Atasimama mbele ya wafalme."
Ufafanuzi
Watu wengi wanataka kufika juu lakini hawataki kupitia hatua za maandalizi.
Hakuna kusudi kubwa bila maandalizi makubwa.
Mungu huandaa tabia, maarifa, nidhamu, uvumilivu na uaminifu kabla hajakabidhi majukumu makubwa.
Ukikataa kujifunza ukiwa chini, utashindwa kusimama ukiwa juu.
Mfano wa Biblia
Daudi hakuanza kuwa mfalme.
Alianza kuchunga kondoo kwa uaminifu.
Huko ndipo alikojifunza ujasiri, uvumilivu, uongozi na kumtegemea Mungu kabla hajaketi kwenye kiti cha enzi.
Yusufu pia alipitia utumwa na gerezani kabla ya kuwa waziri wa Misri.
Mfano wa maisha
Kijana anatamani kuwa mhubiri mkubwa lakini hasomi Biblia.
Anataka kuwa mfanyabiashara mkubwa lakini hajifunzi uongozi wala usimamizi wa fedha.
Anataka kuajiriwa sehemu kubwa lakini hataki kujifunza wala kupata uzoefu.
Funzo
Usidharau mwanzo mdogo. Maandalizi ndiyo daraja linalokupeleka kwenye kusudi.
4. MAHUSIANO MABOVU NA MUNGU
Maandiko
Yohana 15:5
"Maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote."
Isaya 59:1–2
"Maovu yenu yamewatenga ninyi na Mungu wenu."
Ufafanuzi
Kusudi la Mungu haliwezi kudumu bila uhusiano wa karibu na Mungu.
Mahusiano mabovu na Mungu husababisha mtu kupoteza nguvu za kiroho, uongozi wa Roho Mtakatifu, kibali cha Mungu, ulinzi wa Mungu, hekima ya kufanya maamuzi sahihi na uwezo wa kushinda majaribu.
Unaweza kuwa na kipawa lakini ukakosa upako.
Unaweza kuwa na elimu lakini ukakosa mwelekeo.
Unaweza kuwa na uwezo lakini ukakosa kibali.
Unaweza kuwa na fursa lakini ukakosa matunda ya kudumu.
Mahusiano mazuri na Mungu ndiyo yanayofanya kusudi lako liwe na nguvu, ulinzi, mafanikio na matokeo yanayomtukuza Mungu.
Mfano wa Biblia
Samsoni alikuwa na wito mkubwa sana, lakini maisha yake ya kutotii Mungu yaliharibu nguvu zake na ushuhuda wake. Mwishowe alipoteza kibali, nguvu na uhuru wake (Waamuzi 13–16).
Mfano wa maisha
Kiongozi wa vijana ana kipawa kikubwa cha kuhubiri lakini ameacha maombi, kusoma Neno na anaishi maisha ya siri ya dhambi. Polepole huduma yake hupoteza nguvu, watu hawabadiliki na ushuhuda wake huharibika.
Funzo
Kipawa kinaweza kukufungulia mlango, lakini uhusiano wako na Mungu ndio unaokufanya udumu katika kusudi lake.
MUNGU akubariki sana