YANAK Ministry

YANAK Ministry Ni huduma inayotakasa watu na kuwafungua kupitia neno la Mungu kwa maana imeandikwa ktk Biblia Uwatakase kwa ile kweli, neno lako ndiyo kweli. Yohana 17:17

10/05/2023
27/11/2021

KUMTUKUZA MUNGU KABLA YA KUTIMIZIWA AHADI

Mwa 12:7-9 "BWANA akamtokea Abramu akasema, Uzao wako nitawapa nchi hii. Naye huko akamjengea madhabahu BWANA aliyemtokea. Kisha akaondoka huko akaenda mpaka mlima ulio upande wa mashariki wa Betheli, akaipiga hema yake; alikuwa na Betheli upande wa Magharibi, na Ai upande wa Mashariki, akamjengea BWANA Madhabahu huko, akaliitia jina la BWANA. Naye Abramu akasafiri, akazidi kwenda pande za kusini".
Abramu pamoja na kutokuwa na mtoto mpk uzee wake, lakini alikuwa akimtukuza MUNGU aliyemwumba, na alipoahidiwa ahadi ya uzao wake kuirithi nchi ya Kanaani, alimtukuza MUNGU kwa kumjengea Madhabahu, alikuwa ni mcha MUNGU sana anayempenda MUNGU kwa moyo wake wote bila kujali mazingira anayopitia au majaribu aliyonayo, maana hata k**a una hela nyingi bila kuwa na mtoto hilo ni jaribu zito, ni nani wa kuendeleza uzao? Pia Abramu alijawa sana na HOFU ya Mungu. Leo hii watu wengi wanapoahidiwa ahadi na MUNGU wanashindwa Kumtukuza kumsifu na kumshangilia, wanaangalia mazingira waliyonayo au majaribu wanayopitia, hii inamkasirisha sana MUNGU na kuhuzunika moyo. MUNGU anajua ni wakati gani wa kumjibu mtu. Pia yeye MUNGU ni wa kusifiwa atende asitende ukuu wake uko palepale kwamba yeye ni MUNGU WA UTUKUFU na badala yake hakuna mwingine. Aponye asiponye hilo haliwezi kuuondoa ukuu wa MUNGU. Ajibu maombi asijibu wala hilo haliwezi kuuondoa ukuu wa MUNGU, Usipomsifu na Kumtukuza wala haumpunguzii kitu chochote isipokuwa unajipunguzia wewe mwenyewe. Maana wapo watu wengi ambao MUNGU hakuwaponya lakini mpaka sasa MUNGU anatukuzwa. Kuna watu wengi ambao hawakuokolewa, lakini mpaka sasa MUNGU anatukuzwa! Kuna vifo vingi vinatokea vya kabla ya wakati, lakini mpaka sasa MUNGU anatukuzwa! Kuna ajali zinatokea kuna watu wanatolewa misukule lakini mpaka sasa MUNGU anatukuzwa. Kuna watu wengi wamekufa na mipango yao na maono yao bila kutimia, lakini mpaka sasa MUNGU anatukuzwa tena duniani kote. Hivyo usiache kumsifu MUNGU kwa sana, na Kumtukuza kutokana na hali unayopitia, usiwe mnyonge, usiwe dhaifu, usikate tamaa, amka k**a Shujaa paza sauti yako umsifu MUNGU, Mtukuze maana anastahili, na MUNGU WA UTUKUFU ni mwema, atakujibu kwa wakati wake. Mvumilivu hula mbivu. Mchumia juani hulia kivulini, apandaye kwa machozi atavuna kwa kelele za Shangwe, na APANDAYE KWA MAUMIVU MAKALI, ATAVUNA KWA KISHINDO.
MUNGU anaweza, na yeye huwa hanyamazi, anakuwa yuko kazini kwa ajili yako.


Herieth Felix

27/11/2021

MUNGU HUTUPATIA URITHI WA MATAIFA

Mwa 12:6-7 "Abramu akapita katikati ya nchi mpaka mahali Patakatifu pa Shekemu; mpaka mwaloni wa More. Na wakanaani siku zile walikaa katika nchi hiyo. BWANA akamtokea Abramu akasema, uzao wako nitawapa nchi hii. Naye huko akamjengea madhabahu BWANA aliyemtokea".
MUNGU WA UTUKUFU huwapatia watoto wake urithi wa mataifa au milki za watu wengine, hiyo ni desturi yake, kitu alikuwa anamiliki mtu mwingine, anapewa mtu mwingine, eneo lilikuwa linamilikiwa na mtu mwingine, MUNGU WA UTUKUFU anampatia mtoto wake. Gari lilikuwa linamilikiwa na mtu mwingine, anapewa mtu mwingine. Nyumba ilikuwa inamilikiwa na mtu mwingine, anapewa mtu mwingine. Huo ni utaratibu wa MUNGU BABA WA UTUKUFU, na yule naye aliyetoa anapewa vingine. Abramu alitoka kwenda mahali asipopajua maana MUNGU WA UTUKUFU alimwambia toka, akatoka bila kuuliza, na huko alikopita MUNGU akaahidi kuupa uzao wake ile nchi ya Kanaani. Usihofu kuhusu Baraka, Baraka za MUNGU zipo nyingi sana tena Tele maana k**a yasemavyo maandiko kuwa nalikuja ili wawe na Uzima, Kisha wawe nao Tele! Basi hata na Baraka ni hivyo hivyo, nalikuja ili wawe nazo Baraka, Kisha wawe nazo Tele. Kila Kitu MUNGU BABA WA UTUKUFU hutoa Tele, kwake hakuna uchache ni Utele. Uzima Tele! Uponyaji Tele! Wokovu Tele! Ukombozi Tele! Ushindi Tele tena wa Kishindo k**a wa wanaisraeli kwenye bahari ya Shamu. Utajiri Tele! UTUKUFU tele! Maana tunatukuzwa pamoja naye. Amani Tele! Furaha Tele! Raha Tele! Maana pamoja na majaribu yote kuna furaha mbele.


Herieth Felix

05/09/2021

LUTU WA NINI?

Mwanzo 12:1-5 BWANA alimwambia Abramu atoke yeye kwenye nchi yake na kwa jamaa zake na nyumba ya baba yake. Lakini kosa alilolifanya Abramu alitoka pamoja na Lutu mpwa wake. MUNGU hakutaka atoke na Lutu, matokeo yake watumishi wao walianza kugombana njiani maana nchi haikuwatosha kuweza kulisha mifugo yao kwa jinsi ilivyokuwa mingi. MUNGU anapokuita ni lazima utoke wewe peke yako na kumfuata kwa moyo wote. Hicho ulichotoka nacho MUNGU hakihitaji. Wengine wametoka na Kiburi! Lazima kitakuletea Shida njiani. Wengine wametoka na dharau yao! Ni lazima itakuletea Shida. Wengine wametoka na roho ya uzinzi! Ni lazima itakuletea Shida. Wengine wametoka na uongo! Ni lazima utakuletea Shida! Wengine wametoka na vinyago vyao na madhabahu za nyumbani kwao kwa mababu na mabibi! Ni lazima vitakuletea Shida. Wengine wametoka na Umbeya na Fitina na roho ya uchonganishi! Ni lazima itakuletea Shida. Wengine wametoka na Wivu na roho ya kwa nini, ni lazima itakuketea Shida! Wengine wametoka na roho za ugomvi na wengine roho za wizi na dhuluma! Ni lazima itakuletea Shida.
Je! Wewe umetoka na nini?

Herieth Felix
Mtumishi wa MUNGU

05/09/2021

KUBARIKIWA PAMOJA NA MTUMISHI WA MUNGU
Mwanzo 12:3 "Nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani".
Utumishi wa MUNGU unabeba baraka kwa watu wale wanaombariki na kuwa Pamoja naye. Unapombariki Mtumishi wa MUNGU unabarikiwa pamoja naye, unapomlaani MUNGU anakulaani. Unapofanya chochote kwa ajili ya utumishi wa MUNGU unabarikiwa. Kumlaani kunakuja pale unapomfanyia mabaya, unapomnenea mabaya, unapomsimanga, unapokuwa kinyume naye ilihali ameitwa na MUNGU BABA WA UTUKUFU.

Mtumishi wa MUNGU
Herieth Felix

14/08/2021

MTU MMOJA AZAA WENGI

Mwanzo 12:3 "Nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa".
MUNGU alimwambia Ibrahimu kuwa atawabariki watu wale wanaombariki, na atawalaani watu wale wanaomlaani, nani? Ibrahimu. Hili ni jambo jema kwamba tuwaheshimu wapakwa MAFUTA wa BWANA. watu wengi wanawachukulia poa sana, yaani kikawaida sana, na kuongea nao k**a anaongea na mtu fulani wa hali ya chini. Wapakwa mafuta ni watu wa kuheshimiwa, hasa ambao hawana fedha, wanadharauliwa sana. Namna mtu anavyoongea na mtumishi wa MUNGU mwenye Pesa ni tofauti sana na anavyoongea na Mtumishi wa MUNGU asiye na Fedha wakati Fedha ni makaratasi tu ambayo Mbinguni hatuendi nayo, lakini kile kitu kilicho ndani yetu ndicho chenye thamani na ndicho kinachohusika na utumishi wetu. Hata namna anavyochukuliwa mtumishi wa MUNGU mwenye Fedha ni tofauti sana na anavyochukuliwa Mtumishi wa MUNGU asiye na Fedha, fedha fedheha. Yesu anasema, kadri mlivyowatendea hawa ndivyo mlivyonitendea mimi. Watumishi wa MUNGU, MUNGU mwenyewe ndo yuko ndani yao, YESU mwenyewe ndiye yuko ndani yao! ROHO MTAKATIFU mwenyewe ndiye yuko ndani yao! Sio wao, bali MUNGU. Hivyo ni muhimu sana kuwaheshimu watumishi wa MUNGU. Kuchunga vinywa vyetu, ndimi zetu, kutokuwasengenya kuwateta na kuwasimanga. Ni lazima tuwe na Hofu ya MUNGU ndani yetu, k**a hatuna hofu ya MUNGU tumekufa. Wewe unapata wapi ujasiri wa kumnyoshea kidole Mtumishi wa MUNGU, ambaye MUNGU amemteua? MUNGU ameona anafaa, wewe unaona hafai? Unamzidi MUNGU katika kuchagua? Neno linasema kuwa awapokeaye ninyi anipokea mimi. Ampokeaye Nabii kwa kuwa ni Nabii atapokea thawabu ya Nabii. Halikadhalika ampokeaye Mchungaji kwa kuwa ni Mchungaji atapokea thawabu ya Mchungaji. Ampokeaye Mwalimu kwa kuwa ni mwalimu atapokea thawabu ya Mwalimu; Ampokeaye Mwinjilisti kwa kuwa ni Mwinjilisti, atapokea thawabu ya Mwinjilisti; Ampokeaye Mtume kwa kuwa ni Mtume, atapokea thawabu ya Mtume; Ampokeaye Mwimbaji kwa kuwa ni Mwimbaji, atapokea thawabu ya Mwimbaji. Kile Apandacho mtu ndicho atakachovuna. Wewe badala ya kupanda unafanya kazi ya kutawanya! Oh, maskini! Sijui utavuna nini? Hapo ndipo mnapoona wengine wanapanda juu na wengine kuzidi kudidimia chini au kubaki palepale walipo. Mmoja azaa wengi, MUNGU alimwambia Ibrahimu kupitia wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa. Mtu mmoja anafanyika kuwa Mbegu, tena mbegu iliyo njema. Lazima utamani kufanyika mbegu njema ili uzae sana. Kupitia mtu mmoja maelfu ya watu wabarikiwe! Kupitia mtu mmoja mamilioni ya watu wainuliwe! Kupitia mtu mmoja maendeleo yaje! Kupitia mtu mmoja Taifa liinuliwe! Kupitia mtu mmoja watu wabadilike tabia na kugeuza mienendo yao! Kupitia mtu mmoja watu wapate wokovu! Kupitia mtu mmoja watu wafunguliwe ufahamu! Kupitia mtu mmoja waliofungwa wafunguliwe! MUNGU ana haja na mtu mmoja, na huyo mtu mmoja ni wewe unayesoma ujumbe huu.
MUNGU akubariki sana

Mtumishi wa MUNGU
Herieth Felix

05/08/2021

TOKA

Mwa 12:1-2 "BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika Nchi yako na jamaa zako, na nyumba ya baba zako, uende mpaka Nchi nitakayokuonyesha. Nami nitakufanya wewe kuwa Taifa Kubwa, na kukubariki, na kulikuza Jina lako, nawe uwe BARAKA".
MUNGU WA UTUKUFU alimwambia Abramu (Ibrahimu) atoke kwenye Nchi yake na kwa jamaa zake na kwenye nyumba ya baba zake ili aweze kuijitegemea na kuishi yeye k**a yeye na kwamba Ndipo atakapobarikiwa na kufanyika kuwa BARAKA. Hata sasa MUNGU WA UTUKUFU anawaita watu watoke mahali walipo na waweze kuambatana naye, lkn bado watu wanaifanya mioyo yao kuwa migumu. MUNGU anawaita watu watoke kwenye uzinzi!
Watoke kwenye ulevi! Watoke kwenye uasherati! Watoke kwenye uongo, kusema uongo! Watoke kwenye Ibada za sanamu! Watoke kwenye kuabudu miungu! Watoke kwenye Matambiko! Watoke kwenye roho za mila na desturi! Watoke kwenye anasa za dunia! Watoke kwenye kutumainia hirizi na waganga wa kienyeji! Watoke kwenye Umbeya unafiki na mateto na masengenyo. Ndipo watakapofanyika BARAKA. MUNGU alisema Ibrahimu atoke kwenye nyumba ya baba zake na jamaa zake maana kwenye familia na kwenye koo kuna vitu vingi vinafanyika kinyume na wokovu wa MUNGU, hivyo inabidi kutoshirikiana kwa baadhi ya vitu ambavyo unaona vinatia unajisi. Hasa mambo ya matambiko.

19/06/2021

MAKUSUDI YA MUNGU

Mwa 11:5-8 "BWANA akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu. BWANA akasema, Tazama, watu hawa ni Taifa moja na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. Haya na tushuke huko tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao. Basi BWANA akawatawanya kutoka huko waende usoni pa Nchi yote; wakaacha kuujenga ule mji." MUNGU huwa anatenda jambo ambalo anaona lina faida kwa Upande wake. Mwanadamu anapotenda jambo kwa manufaa yake binafsi basi ni lazima MUNGU ataingilia kati na kupangua mipango yote. Mawazo ya mwanadamu Siku zote ni Tofauti na mawazo ya MUNGU. Ukitaka uendane na mawazo ya MUNGU WA UTUKUFU basi itakupasa kuongozwa na ROHO ALIYE MTAKATIFU, (kuna roho nyingi). Na ukitaka kuenda vizuri na mipango ya MUNGU bila kukosea, itakubidi uwe mtu wa sirini, mambo ya sirini, maombi ya Sirini asiyoyajua mtu yeyote wala hata mapepo hayawezi kuyang'amua! Maombi ya kunena kwa Lugha, ni Siri yako wewe na MUNGU na ROHO MTAKATIFU. Hakuna wa tatu wa kujua umeomba nini. Antena zote zinagonga MWAMBA. Hawa watu walikuwa wakijenga mji na mnara wake ufike Mbinguni kwa urefu wake, lengo wasipate kutawanyika usoni pa nchi. Kwa mawazo ya Kibinadamu walikuwa Sahihi, na hiyo ilikuwa ni faida yao binafsi; ila kwa mawazo ya MUNGU haikuwa Sahihi na hivyo ilimlazimu MUNGU awachafulie usemi ili wasisikilizane na Kitendo hicho kiliwafanya waache kuujenga mji na mnara, maana Lengo la MUNGU alitaka watu watawanyike huku na huko ili dunia izidi kuenea watu, wazidi kujenga miji, na Siyo kukaa mahali Pamoja. Kukaa mahali Pamoja kunadumaza, inatakiwa mtu utoke ndo unajifunza mengi, unapotoka huko unakokwenda kuna vitu watu watafaidika kutoka kwako, na kuna vitu ambavyo utajifunza. Na huku kutoka, siyo kutoka Kiholelaholela, ni kutoka kwa kuongozwa na ROHO MTAKATIFU. MUNGU anatazama moyo na kujua nia ya mtu ni nini pale anapotaka kufanya jambo, akijua nia siyo nzuri au haimpi yeye UTUKUFU, anaghairi na ndio maana watu huanzisha jambo likafa au kuishia njiani. Unapotembea nje ya ROHO MTAKATIFU utaona mawazo ya MUNGU na njia zake ni ngumu, utaona km MUNGU hatendi haki, anakuonea au hayuko sawa, maana mawazo na njia vinatofautiana. Lkn unapotembea ndani ya ROHO MTAKATIFU na kukubali kuongozwa naye, utaona kuwa mawazo ya MUNGU ni mazuri na njia zake ni nzuri. Kwenda sawa na MUNGU kunategemeana na connection uliyonayo na ROHO MTAKATIFU.

Can't go back in Jesus name!!!

17/06/2021

UMOJA NI NGUVU

Mwanzo 11:1-4 "Nchi yote ilikuwa na lugha moja na usemi mmoja. Ikawa watu waliposafiri pande za mashariki waliona nchi tambarare katika nchi ya Shinari wakakaa huko. Wakaambiana, haya, na tufanye matofali tukayachome moto. Walikuwa na matofali badala ya mawe, na lami badala ya chokaa. Wakasema, haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike Mbinguni. Tujifanyie jina ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote".
Umoja ni Nguvu kubwa sana, palipo na umoja pana mafanikio makubwa na ushindi Tele. Hawa watu walikuwa na umoja na lugha moja na usemi mmoja na ndiyo maana waliweza kuujenga mji na mnara ambao waliazimu ufike Mbinguni kutokana na urefu wake ili iwe ni alama ya kuwafanya wasitawanyike usoni pa nchi. Penye nia pana Njia. Walikuwa na lugha moja na usemi mmoja, Tatizo linalokwamisha maendeleo na watu kutokufika mbali ni kukosekana kwa umoja, kuwa na lugha tofauti na usemi tofauti, huyu anasema hivi, huyu anasema vile! Ni kupishana kauli. Pengine mtu anaweza kutoa wazo lkn wazo lake Siyo zuri ila anataka asikilizwe na wazo lake litendewe kazi, wazo lake lisipotendewa kazi anaona amepuuzwa au haheshimiwi. Hili nalo ni Tatizo kutanguliza heshima ya mtu badala ya kuangalia kazi au matokeo yatakayopatikana kwa kutendea kazi wazo POTOFU. Wengine wanataka wasikilizwe eti kwa kuwa wana umri mkubwa, hawataki mawazo ya vijana yatendewe kazi. Hatuangalii umri wa mtu, tunaangalia Kazi. Hata k**a mtoto wa miaka 5 katoa wazo inabidi litendewe kazi iwapo ni zuri.
Umoja upo sehemu mbalimbali. Kuna umoja wa wanandoa, k**a wanandoa wanapendana na kusikilizana na kuwa na umoja ktk kila jambo, basi watafika mbali. Kuna umoja wa wanafamilia. Familia kuwa na umoja. Siyo familia kila mtu anaishi kivyake anavyojua yeye, hakuna Salam, hakuna kujuana hali, hakuna kutembeleana mara mojamoja, hakuna kusaidiana, hakuna kuombeana! Pia kuna umoja wa ukoo, wanaukoo. Kuna umoja wa Viongozi! Umoja wa wafanyakazi! Umoja wa vijana! Umoja wa wanawake, Umoja wa waombaji, wanamaombi. Hawa ni watu muhimu sana, wanalibeba Taifa nk. Kufanya jambo kwa umoja kunaleta Ushindi.

21/04/2021

USIKUBALI KUTOLEWA MBUZI WA KAFARA
Mwanzo 9:24-27 "Nuhu akalevuka katika ulevi wake, akajua mwana wake mdogo alivyomtendea, akasema, na alaaniwe Kanaani, atakuwa mtumwa kabisa wa ndugu zake. Na akasema, atukuzwe BWANA MUNGU wa Shemu, na Kanaani awe mtumwa wake. MUNGU akamnafisishe Yafethi, na akae katika hema za Shemu; na Kanaani awe mtumwa wake". Kosa la Hamu la kuuchungulia uchi wa Baba yake, lilimgharimu na kumfanya mtoto wake alaaniwe, maana Kanaani ni mtoto wa Hamu. Kanaani akafanyika kuwa mtumwa wa ndugu zake.Ukisoma katika Biblia utaona Kizazi cha Kanaani kilivyoijaza Africa, yaani walizaliana Africa, na Kizazi cha Shemu na Yafethi Ulaya, ndipo Mataifa ya Ulaya yakaonekana MAKUBWA yana NGUVU na Baraka Tele, alafu Africa tukawa watumwa, mataifa yetu yakaonekana hayana nguvu, mpaka tupate misaada Toka Ulaya. Ni kwa Sababu Hamu alitolewa Mbuzi wa kafara, alifanya kosa lililomfanya ashuke chini na ndugu zake kupanda juu. Maana tunaposema kuwa kuna MATAIFA MAKUBWA YENYE NGUVU NA MATAJIRI, ina maanisha kuna mataifa ya chini, mataifa maskini na dhaifu. Ina maana haya mataifa yametolewa kuwa mbuzi wa kafara. Ili kiwepo kitu bora lazima kiwepo kitu dhaifu ili kilicho bora kionekane. Ili awepo mshindi wa kwanza lazima wawepo waliofeli ili mshindi wa kwanza apatikane. Hawa waliofeli wametolewa mbuzi wa kafara kwa ajili ya Mshindi wa kwanza. Ili wawepo watu wanaofanya vizuri, ni lazima wawepo wanaofanya vibaya ili wanaofanya vizuri waonekane. Usikubali kutolewa Mbuzi wa kafara, kwa kosa la Hamu ndugu zake waliinuliwa! Kwa makosa ya ususi wako unamfanya mwingine aonekane kuwa msusi maafuru, k**a hayupo yeye watu hawasuki! Mtu anaulizia, fulani yupo? Akiambiwa hayupo anarudi bila kusuka, je wengine Siyo wasusi? Lazima kila mtu aonekane kuwa bora, na inawezekana kila mtu kuwa bora. Hata Mataifa ya Africa yaliyo mengi yameshainuka na kuwa bora, na inawezekana Kila Taifa kuwa bora, ni mipango na utendaji kazi ukiwepo ubunifu na ujuzi au utaalamu. Inawezekana wanafunzi wote kuwa bora, ndiyo maana nafasi ya kwanza inaweza ikashikiliwa na watu 3, hivyo wakijitahidi wote wanaweza kuwa namba 1 asiwepo wa 2 wala wa 3. Kuna Shule unakuta karibu wote wamepata Division 1. Hivyo hilo linawezekana wote kuwa bora. Kuna mashindano ya urembo yanaweza kufanyika majaji wakachanganyikiwa wasijue yupi anastahili kuwa kwanza, yupi anastahili kuwa wa pili. Hivyo inawezekana wote kuwa bora. Mtu mmoja anapoimba sana kuliko wote, akashangiliwa yeye peke yake, ina maana hao wengine walioimba wanaonekana hamna kitu, maana wangeimba vizuri wangekonga mioyo ya watu. Usikubali kuonekana hamna kitu. Mtu anapohubiri sana au kufundisha akapendwa sana kiasi kwamba akihama watu wanahama naye, ina maana wengine wanaonekana hamna kitu, wangekuwa na kitu watu wasingehama, maana watu wana tabia ya kuwafuata watu badala ya kumfuata MUNGU. Hivyo ni lazima kila mtu asimamie nafasi yake IPASAVYO ili kuonekana bora. Wanaposifia kuhusu mke mwema au mume mwema, ina maana kuna wake bomu na wame bomu. Mtu anapoitwa mfanyakazi bora, kuna wasio bora! Mtu anapoitwa Kiongozi bora, kuna kiongozi asiye bora, watu wanatamani hata ajiuzuru au afukuzwe. Mtu anaposifiwa ni muumini mzuri mtiifu, kuna waumini pasua kichwa! Ni mbuzi mwenye mapembe hata viongozi wa dini wanalia! Wanaumia. Kiongozi yoyote wa dini anapenda waumini wake wawe wazuri watiifu wenye Tabia njema, na Siyo wenye kuaibisha. Inawezekana watu wote kuwa bora, k**a ni mke mwema usifiwe wewe! K**a ni mume mwema usifiwe wewe! K**a mtoto bora usifiwe wewe! K**a ni mama bora usifiwe wewe! K**a ni baba bora usifiwe wewe! K**a ni jirani mzuri usifiwe wewe! K**a ni mchungaji mwema usifiwe wewe! K**a ni muumini mwema mfano wa kuigwa usifiwe wewe! K**a ni Kiongozi bora usifiwe wewe! K**a ni mfanyakazi bora usifiwe wewe! K**a ni Mwinjilisti mzuri uwe wewe! K**a ni Mwalimu mzuri uwe wewe! K**a ni mpishi mzuri uwe wewe! K**a ni mtangazaji bora uwe wewe! K**a ni mwandishi bora uwe wewe! K**a ni msusi bora uwe wewe! Katika jitihada za kila mtu kuutafuta ubora wake, basi tutajikuta wote tunakuwa bora. Na ubora unakuja kwa kuwa na bidii na kujituma, na kufanya kila kinachohitajika kwenye Sekta yako. MUNGU akubariki, akujalie kuwa bora.

19/04/2021

KUUSHINDA MWILI

Mwanzo 9:20-23 "Nuhu akaanza kuwa Mkulima, akapanda mizabibu; akanywa divai akalewa, akawa uchi katika hema yake. Hamu baba wa Kanaani akauona uchi wa baba yake, akawaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje. Shemu na Yafeth wakatwaa vazi wakalitanda mabegani mwao wote wawili wakaenda kinyumenyume wakaufunika uchi wa baba yao; na nyuso zao zilielekea nyuma, wala hawakuuona uchi wa baba yao".
Kuushinda mwili ni lazima. Hamu aliuona uchi wa baba yake akawaeleza ndugu zake, badala ya kumfunika yeye anatangaza, kuna watu huwa wanawashwa, badala ya mtu mmoja kuona aibu yako, anataka watu wote waone aibu yako na wajue aibu yako, yaani mtu anaona jambo la siri badala atunze akae nalo moyoni yeye anatangaza. Je hiyo aibu ingekuwa ya kwake au ya mtoto wake angependa watu wajue? Ni lazima kuwa na kifua cha kusitiri mambo na kutunza siri. Alitaka na kaka zake nao wajue, hili jambo lingebaki kwake, mwisho akaambulia laana. Kuushinda mwili ni lazima, mwili una ushawishi mwingi, mtu anaona mdada anatembea nusu uchi lazima ageuke, mtu kavaa Suruali inabana unageuka unatazama, unaangalia mapichapicha ya ajabu macho hayatulii njiani, mwisho ufahamu wako unatekwa unaanza kukumbuka mwanamke uliyepishana naye amevaa kimini, unapatwa na hisia mbaya unajitia kwenye uzinzi wa kupitia ufahamu unamkosea MUNGU. Ni kwa sababu haukubali kupitwa, mambo mengine yaache yapite, lazima kutulia. Katika maisha Siyo kila unachokiona ni cha kusema, Siyo Kila unachokisikia ni cha kutangaza, utasema visivyosemeka, utatangaza visivyotangazika mwisho vitaleta madhara. Hamu alisema alichokiona akaambulia laana. Watu wengi huongea maneno ya kujitia unajisi, husikia maneno watu wanaongea juu ya watu wakati mwingine ni ya uongo watu wanachonga, mwisho wanaambulia laana, wakati mwingine ni ya ukweli ila Siyo kila jambo ni la kushabikia inatakiwa utulivu wa rohoni. Kuushinda mwili na Tamaa zake ni lazima, macho siyo ya kutazama Kila kitu, kuna vitu hutakiwi kuviona; Masikio siyo ya kusikia kila kitu, kuna vitu hautakiwi kuvisikia; Mdomo siyo wa kuongea kila neno, kuna maneno hautakiwi kuyaongea; Pua siyo za kunusa kila harufu, kuna ukizikia utaumwa au utakufa. Ufahamu siyo wa kuwaza kila kitu, kuna vitu ukiviwaza unakosea au unapotea. Mikono siyo ya kushika kila kitu, miguu siyo ya kwenda kila mahali, kuna mahali hutakiwi kwenda. USHINDE MWILI NA TAMAA ZAKE.

16/04/2021

UTATU WENYE NGUVU

Si mara ya 1 kuona utatu kwenye biblia, utatu wa kwanza tunauona kwa MUNGU mwenyewe na BWANA YESU na ROHO MTAKATIFU.
Mwanzo 9:18-19 "Wana wa Nuhu waliotoka katika Safina ni, Shemu, Hamu na Yafeth, na Hamu ndiye baba wa Kanaani. Hawa watatu walikuwa wana wa Nuhu, na kwa hao nchi yote ikaenea watu". Watu wengi sana huwa wanahangaikia namba maana Kila namba huwa ina maana yake. Mtu anapotumia namba fulani huwa kuna kitu anamaanisha, hata rangi pia, si kwamba watu wanatumia rangi ovyo, mtu anapotumia rangi fulani au anapopendelea rangi fulani ana maana yake. Namba inaongea, rangi inaongea. Hapa tunaona utatu wenye nguvu, kwa kuwatumia Shemu Hamu na Yafeth Nchi ilijaa watu, yaani kuzaliwa kimwili. Tukienda kwa upande wa kiroho, kwa kumtumia MUNGU MTUKUFU, ROHO MTAKATIFU na BWANA YESU MWOKOZI, watu wanaokolewa, pia katika uumbaji walishirikiana na kutenda kazi kwa Pamoja, na katika kumwokoa mtu na kumtengeneza wanashirikiana kila mmoja na sehemu yake, ni sawa na mafundi ujenzi, nyumba moja inajengwa na mafundi tofauti kila mmoja na utaalamu wake ukianzia msingi mpaka nyumba kukamilika hatimaye kuwavutia watu. Kwa kuwatumia Shemu Hamu na Yafeth Nchi ilijaa watu, kwa kumtumia MUNGU MTUKUFU, MUNGU ROHO, MUNGU MWANA, watu wanaokolewa, watu wanatengenezwa na kufanywa upya. Huo ndio UTATU MTAKATIFU wenye NGUVU. Kila mmoja ni muhimu. Hata kazi yoyote ili ionekane kuwa bora inahitaji ushirikiano, hakuna mtu anaweza kufanya kitu kizuri peke yake. Fundi wewe unajenga matofali unajihudumia mwenyewe unapanda juu na kushuka chini kuchukua tofali! Msusi wewe huku unamtengeneza mtu nywele mara kaja wa kusafisha kucha, utasubili mpaka umalize kumsuka mtu ndo umsafishe huyu wa kucha? Kiongozi wa familia ni wewe! Kiongozi wa Serikali ni wewe! Inatakiwa awepo mtu wa kushughulikia maswala ya nyumbani, anakupa tu taarifa. Kanisani mhubiri ni wewe, mwimbaji ni wewe, mpiga vyombo ni wewe, mwombaji ni wewe, ukitoka hapo uko hoi! Ndo maana MUSA alishauriwa na babamkwe wake kwamba aweke wasaidizi, la sivyo atakonda. MUNGU katuumba tusaidiane, huyu hivi na huyu hivi, huyu anafanya hiki, na huyu anafanya kile ndo mambo yanakuwa mazuri. Ukifanya kila kitu peke yako unaweza kuharibu, au unaweza kukosea asiwepo mtu wa kukukosoa. Ndiyo maana sisi ni viungo. Na mtu anapofikiri kuwa yeye ni babukubwa anajua zaidi kuliko wote, kumbe kuna watu zaidi yake. Ujuzi unatoka kwa Baba wa mianga, na kila mtu hufanya kwa sehemu.

Address

Dar Es Salaam

Telephone

+255713174677

Website

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when YANAK Ministry posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Share