09/06/2021
NAMI NIENDAKO MWAIJUA NJIA.
"4. Nami niendako mwaijua NJIA. 6 Yesu akamwambia, Mimi ndimi NJIA, na kweli, na uzima; MTU HAJI KWA BABA ILA KWA NJIA YA MIMI"(YOHANA 14:4,6).
Katika mistari iliyotangulia kabla ya wa 4,yaani YOHANA 14:1-3,Bwana Yesu alianza kuwaambia wanafunzi na wafuasi wake; "Msifadhaike mioyoni mwenu... Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; k**a sivyo ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi Mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo Mimi, nanyi mwepo". Katika mistari hii kimsingi alikuwa anasema anakwenda Mbinguni au Peponi kwenye Makao ya Furaha na raha tele. Halafu ndipo ukafuata huo mstari wa 4; "NAMI NIENDAKO(yaani huko Mbinguni) MWAIJUA NJIA". Katika mstari wa 5 Mwanafunzi Tomaso akamwomba Bwana awafahamishe bayana juu ya hiyo NJIA. Ndipo mstari wa 6 Bwana Yesu akatanabaisha bila chenga juu ya NJIA hiyo ya kwenda Mbinguni; "Yesu akamwambia, Mimi ndimi NJIA, na kweli, na uzima; MTU HAJI KWA BABA, ILA KWA NJIA YA MIMI".
Wengi wetu tunafahamu juu ya Njia. Njia ni kiongozi yaani hutuongoza kufika kule tulikokusudia kufika/kwenda.
Duniani zipo njia za namna mnalimbali ambazo kwazo mtu huweza kufika kule aendako. Mtu akitaka kwenda kazini, shambani au kwenye shughuri zake za kila siku sharti aifuate njia ya kwenda huko. Iwapo mtu anataka kurudi nyumbani kwake au pale anapoishi, sharti aifuate njia ya kwenda kwake. Ipo njia ya kwenda sokoni, dukani, bombani au kisimani, Kanisani au kwenye nyumba ya ibada nk.
Ili mtu aweze kufika kule alikoazimia kwenda/kufika ni lazima aifuate njia sahihi ya kumfikisha huko. Iwapo mtu ataamua kuifuata njia yoyote ilimradi itakuwa vugumu sana kufika kule alikoazimia kufika. K**a mtu yupo DSM na anataka kufika Arusha sharti aifuate njia ya kwenda Arusha; k**a ataamua kuifuata njia iendayo Mbeya au Mtwara ni vigumu kwa mtu huyo kufika Arusha. Kwanini? Kwa sababu hakuifuata njia sahihi iendayo Arusha.
Vyivyo hivyo ipo NJIA ya kwenda Mbinguni. Ili mtu aweze kufika Mbinguni ni lazima aifuate NJIA sahihi ya kwenda Mbinguni. K**a mtu ataamua kufuata njia yoyote ilimradi kwa matarajio ya kufika Mbinguni, kamwe hataweza kufika huko.
Tofauti na hapa duniani, mtu anaweza kufika mahali fulani kwa kutumia njia tofauti tofauti; lakini katika suala zima la kufika Mbinguni NJIA IPO MOJA TU. Hapa duniani mtu anaweza akafika mahari fulani kwa kutumia usafiri wa Gari yaani njia ya barabara; lakini anaweza kuamua kutumia Treni au gari moshi yaani njia ya reli; au anaweza akapanda Ndege kwa njia ya anga :katika mazingira mengine akaamua kupanda Meli au boti kwa njia ya majini. Lakini linapokuja suala la kwenda Mbinguni NJIA ipo moja tu nayo ni Bwana Yesu Kristo; "MTU HAJI KWA BABA ILA KWA NJIA YA MIMI" asema Bwana Yesu. Katika MATENDO YA MITUME 4:12,Biblia inasema; "Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo". Ni Jina la Yesu Kristo pekee ndipo tunapoweza kuhesabiwa haki na kupata wokovu wa roho zetu. Mistari iliyotangulia anatajwa kuwa ni Jiwe lilikataliwa na waashi ambalo ni Jiwe Kuu la pembeni.
Mpendwa msomaji, je ungependa kufika Mbinguni, kwenye Makao ya milele? Huyu Yesu ndiyo NJIA. Ukitubu dhambi zako na kumpokea Yesu Kristo k**a Mwokozi na Bwana wa maisha yako utakuwa unatembea katika Njia ya Uzimani/Mbinguni. Damu Yake ya thamani kuu itakusafisha kabisa. Jina lako litafutwa kwenye kitabu kimojawapo cha Hukumu na kuandikwa kwenye Kitabu cha Uzima cha Mwanakondoo. Utahesabiwa haki bure ya kuingia Mbunguni nk nk. K**a upo tayari fuatisha sala hii ya kutubu dhambi na kuokoka. Sema: "BWANA YESU, NIOSHE KWA DAMU YAKO. NAKUPOKEA K**A MWOKOZI NA BWANA WA NAISHA YANGU. KATIKA JINA KUU LA BWANA YESU AMEN". Tayari. Jiunge na kanisa la wokovu kwa msaada zaidi. Kwa maulizo au msaada zaidi wa kiroho unaweza kunipigia kwa Simu/WhatsApp 0783 75 26 31(+255 783 752 631). Ndimi ndugu yako Pastor Sume Mbena.