31/05/2026
SIFA ZA HIJABU YA KISHERIA (صفات الحجاب الشرعي)
Assalamu Alaykum warahmatullah wabarakatuh.
Hijabu si mavazi tu ya kitamaduni, bali ni ibada na utii kwa Allah (Subhanahu wa Ta'ala). Ili hijabu ikidhi vigezo vya kisheria na kukubaliwa, ni lazima iwe na sifa zifuatazo kwa mujibu wa Qur'ani na Sunnah:
1. Kufunika Mwili Mzima (استيعاب جميع البدن)
Hijabu ya kisheria ni lazima isitiri mwili wote wa mwanamke isipokuwa kile kilichovuliwa (k**a mikono na uso kwa baadhi ya wanachuoni).
Dalili:
Allah Amesema:
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَّحِيمًا
"Ewe Nabii! Waambie wakezo, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao (jilbāb). Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana (kuwa ni watu heshima) wasiudhiwe. Na Allah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu."
(Al-Ahzab: 59)
──────────────────
2. Isiwemo Pambo Ndani Yake (أن لا يكون زينة في نفسه)
Nguo yenyewe ya hijabu isilete mvuto au kurembwa kwa namna inayovutia macho ya wanaume wa kando (ajnabiy).
Dalili:
Allah Amesema:
وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ
"...Wala wasidhihirishe mapambo yao..."
(An-Nur: 31)
──────────────────
3. Iwe Nzito Isiyoonyesha Ndani (أن يكون صفيقا لا يشف)
Nguo haitofanya sitara ikiwa ni nyepesi kiasi cha kuonyesha rangi ya ngozi au mwili wa mwanamke.
Dalili:
Mtume (صلى الله عليه وسلم) amesema:
سيكون في آخر أمتي نساء كاسيات عاريات... لا يدخلن الجنة ولا يجدن ريحها
"Watakuwepo mwisho wa umma wangu wanawake waliovaa nguo lakini wako uchi... Hawataingia Peponi wala hawatasikia harufu yake."
(Hadithi ya Muslim)
──────────────────
4. Iwe Pana Isiyobana (أن يكون فضفاضا غير ضيق)
Lengo la hijabu ni kuzuia fitna, hivyo nguo inayobana na kuchora maumbo ya mwili haikidhi sifa ya hijabu.
Dalili:
Mtume (صلى الله عليه وسلم) alimwambia Usamah bin Zaid kuhusu nguo nene aliyompa mke wake:
مُرْهَا فَلْتَجْعَلْ تَحْتَهَا غِلَالَةً، فَإِنِّي أَخَافُ أَنْ تَصِفَ حَجْمَ عِظَامِهَا
"Mwambie aweke nguo ya ndani chini yake (hiyo nguo nene), kwani mimi nachelea isichore ukubwa wa mifupa yake (umbo lake)."
(Hadithi ya Ahmad na Al-Bayhaqi)
──────────────────
5. Isitiwe Marashi wala Manukato (أن لا يكون مبخرا مطيبا)
Mwanamke haruhusiwi kutoka nje akiwa amejipaka manukato kwenye mwili au nguo zake kwa namna inayovutia watu.
Dalili:
Mtume (صلى الله عليه وسلم) amesema:
أَيَّمَا امْرَأَةٍ اسْتَعْطَرَتْ فَمَرَّتْ عَلَى قَوْمٍ لِيَجِدُوا مِنْ رِيحِهَا فَهِيَ زَانِيَةٌ
"Mwanamke yeyote atakayejipaka manukato kisha akapita mbele ya watu ili wasikie harufu yake, basi huyo ni mzinifu."
(Hadithi ya Abu Musa Al-Ash'ari)
──────────────────
6. Isifanane na Mavazi ya Wanaume (أن لا يشبه لباس الرجل)
Ni haramu kwa mwanamke kuvaa mavazi yaliyohusishwa mahususi kwa wanaume.
Dalili:
لَعَنَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ الرَّجُلَ يَلْبَسُ لِبْسَةَ الْمَرْأَةِ، وَالْمَرْأَةَ تَلْبَسُ لِبْسَةَ الرَّجُلِ
"Mtume (صلى الله عليه وسلم) amemlaani mwanamume anayevaa vazi la mwanamke, na mwanamke anayevaa vazi la mwanamume."
(Hadithi ya Abu Hurairah)
──────────────────
7. Isifanane na Mavazi ya Wanawake wa Kikafiri (أن لا يشبه لباس الكافرات)
Mavazi ya mwanamke wa Kiislamu yanatakiwa kuwa na utambulisho wake wa kiimani na yasifanane na nembo au mitindo maalumu ya makafiri.
──────────────────
8. Isiwe Nguo ya Umaarufu/Kujionesha (أن لا يكون لباس شهرة)
Kujiepusha na nguo inayovaliwa kwa lengo la kujivunia, kujionyesha, au kuwa tofauti na watu ili tu kupata umaarufu au sifa.
Dalili:
Mtume (صلى الله عليه وسلم) amesema:
مَنْ لَبِسَ ثَوْبَ شُهْرَةٍ فِي الدُّنْيَا أَلْبَسَهُ اللَّهُ ثَوْبَ مَذَلَّةٍ يَوْمَ الْقِيَامَةِ
"Mwenye kuvaa nguo ya umaarufu (kujifakhiri) hapa duniani, Allah Atamvisha nguo ya udhalili Siku ya Kiyama."
(Hadithi ya Ibn Umar)