14/09/2023
WAZEE NI HAZINA!!!
Ugeni, ugeni!
Mafrateri 52 wa Jimbo Katoliki la Bukoba, pamoja Mkurugenzi wa miito wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Padre Edson Mtembei, watembelea mapadre wazee katika kituo chao cha watakatifu Oscar na Wilbard, kilichopo katika Parokia ya Kagondo.
Matembezi hayo yaliambatana na Adhimisho la Misa Takatifu la Kutukuka kwa Msalaba lililoongozwa na Paroko wa Parokia ya Kagondo, Padre Medericus Kyaruzi, akisaidiana na Askofu Mstaafu wa Jimbo la Bukoba, Mhashamu Askofu Desiderius Rwoma, Padre Edson Mtembei pamoja mapadre wazee.
Mafrateri walishirikishana mengi na mapadre hao wazee wakichota hekima, ujuzi, uelewa, maadili, historia, na ustaarabu wa Maisha ufaao kwa padre katika ujana wake na katika muda wote wa kumtumikia Mungu. Mapadre wazee wamewasisitiza vijana hao kuwa karibu zaidi na Yesu Kristo pamoja na kumpenda Bikira Maria ili waweze kustawi vema katika utume na kuwa kweli mbegu, chumvi na mwanga kwa ulimwengu.
Aidha, wazee wameeleza furaha yao ya kuona kuwa kazi aliyoiacha Kristo ambayo nao waliishiriki bado zina watu wenye nia ya kuziendeleza, yote kwa ajili ya kukuza na kueneza ufalme wa Mungu duniani. Baada ya Adhimisho la Misa na mawaidha ya wazee, burudani zilifuata pamoja na kidedea kikali kutoka kwa mafrateri kwa nia ya kuwachangamsha wazee na kuwashirikisha furaha za vijana.
Mapadre wazee waliopo katika kituo hicho kwa sasa ni:
1. Msgr. Deogratias Rweyongeza
2. Pd. Gotfried Kamala
3. Pd. Thomas Tibainuguka
4. Pd. Potentine
5. Pd. Odilon Kajwahura
6. Pd. Audax Rutakyamirwa
7. Pd. Leopold Mushuga
8. Pd. Edward Furahisha