22/04/2026
MWANANGU,
YULE MAMA HAKUMALIZA VIZURI SAFARI YAKE!
Hivi ndivyo Mchungaji wangu, alivyoanza kunieleza kwa habari ya kifo cha mama mmoja tuliyekuwa tukisali naye.
Nilimfahamu mama huyu mara tu nilipookoka,
Kwa ufupi alikuwa ni mama mwenye kumpenda sana Mungu, aliyejali ibada na zaidi Mwana maombi mzuri.
Alikuwa ni mama ambaye ni mfano wa kuigwa kwa mambo mengi...
kwa jinsi ya kibinadamu naweza kusema alikuwa Mshirika mwaminifu.
Nimeabudu na mama huyu kwa takribani miaka 3, nilitengana na mama huyu kwa kwenda Mkoa mwingine.
Mwaka fulani niliporudi likizo, nilienda kanisani kwaajili ya ibada ya jioni,
nilipofika kanisani niliambiwa kuwa ibada ya jioni ile itafanyika kwa mama huyu kwani amefariki.
Moyoni mwangu nilihuzunika kupata taarifa ile, ila nilipata tumaini na kuamini kwamba maadam alikuwa ameokoka na endapo aliendelea kuwa mwaminifu kwa Mungu wake basi atakuwa yupo na Bwana akifurahi. Ndipo nikaenda kuungana na washirika wenzangu, kwenda kuwafariji familia ile kwa kuondokewa na ndugu yao.
Kesho yake nilienda kwa Mchungaji wangu kumsalimu na pia kumpa pole kwa kupatwa na msiba huo... Baada ya kumpa pole kwa kuondokewa na mama huyo, ndipo alipoanza kwa kusema
‘Mwanangu, kwa kweli yule mama hakumaliza vizuri safari yake. Mungu ndiye ajuaye yuko wapi, ila nami k**a Mchungaji wake, nasikitika kusema hakumaliza vizuri’.
Kauli hii ilinishtua sana, nami nikamuuliza kwa nini unasema hivyo Pastor?,
Ndipo aliponiambia yote ambayo mama yule aliyafanya miezi kadhaa kabla ya kifo chake.
Baada ya Mchungaji wangu kunielezea maisha yote ya yule mama katika siku zake za mwisho, ndani yangu niliumia sana.
Naam niliumia kwa sababu kubwa mbili;
Moja ni namna nilivyokuwa namfahamu na kumpenda yule mama kutokana na juhudi na imani yake katika Bwana.
Mbili ni ufahamu nilionao kuhusu wapi mtu anakwenda k**a hakufa katika Bwana.
Maana imeandikwa "…Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao."
(Ufunuo 14:13)
K**a mtu hakufa katika Bwana (utakatifu) mahali anapokwenda panaitwa kuzimu.
Kuzimu ni mahali ambapo laiti mwanadamu angejua nini kinaendelea huko, si tu angemwamini Yesu, bali asingeleta mchezo kwenye wokovu na angeishi maisha ya utakatifu kuzidi maelezo,
Jambo moja ambalo nina hakika nalo ni hili, endapo mtu atakufa katika dhambi zake, bila kutengeneza njia au mahusiano yake na Mungu akali hai, basi huyo atakuwa amemaliza safari yake vibaya, na kuzimu ndipo mahali ambapo ataenda.
Mpenzi msomaji, najua watu wengi hawapendi kuambiwa ukweli huu, lakini ni vema uujue kabla hujafa, ili ujifunze kuishi maisha ya kumpendeza Mungu wako.
Biblia inasema
"Na k**a vile watu walivyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu"
(Waebrania 9:27).
Je wewe utamalizaje safari yako hapa duniani?, Je unajua kwamba kifo chako ndio mwanzo wa maisha mapya ya umilele?,
Naam, maisha hayo ni ama ya mateso milele (kuzimu kisha Jehanamu) au raha milele (mbinguni kisha Jerusalemu mpya).
Wapi mtu atataka kwenda baada ya kufa anapaswa kufanya maamuzi akiwa hai.
Naam si tu kuokoka bali kuishi maisha matakatifu, maana wapo wengi ambao waliokoka lakini baada ya kufa kwao wakajikuta kuzimu, na hii ni kwa sababu hawakuwa waaminifu kwa Mungu wao katika kutii amri zake.
K**a unafikiri kuwa Mkristo ni tiketi ya kukupeleka mbinguni siku ukifa, badilisha fikra zako mapema, maana, mbinguni hawaendi Wakristo, bali watakatifu, naam wale wayafanayao mapenzi ya Mungu hapa duniani,
Rejea Mathayo 7:21
Kwa maelezo ya Mchungaji wangu yule mama katika siku zake za mwisho alifika mahala pa kwenda kwa waganga wa kienyeji ili kupata msaada.
Nami moyoni mwangu nilijiuliza maswali mengi kwamba,
kwa nini alienda kwa waganga wa kienyeji kutafuta msaada?,
Je, ni kweli Mungu wake aliyemwamini siku zote alishindwa kumsaidia? Kwa nini aliruhusu Shetani amdanganye kiasi hiki, k**a Hawa alivyodanganywa? (Mwanzo 3:1-19).
Ndipo nikajua kuna mahali yule mama alimpa Ibilisi nafasi (Waefeso 4:27) na Shetani akatumia nafasi hiyo ili kuhakikisha mama yule anamaliza vibaya.
Nilipozidi kutafakari juu ya jambo hili, ndipo mawazo yangu yalipoingia moyoni mwangu na kunikumbusha kile ambacho Mtume Paulo aliwaambia Wagalatia akisema
"Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulubiwa? Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani? Je mmekuwa wajinga namna hii? Baada ya kuanza katika Roho mnataka kukamilishwa sasa katika mwili?.
Wagalatia 3:1-3.
Ukisoma vizuri sentensi za Paulo ambazo nyingi zipo katika mfumo wa maswali ni ishara kuwa,
Paulo mwenyewe alikuwa haamini kile ambacho alikiona kinatokea kwa Wagalatia,
Kwani alijua walivyoanza vizuri na Bwana, lakini hali yao ya mwisho ilikuwa ni mbaya tena ya mwilini. Kwa sababu hii Paulo akaugua sana rohoni, ndipo ikamlazimu kutumia lugha ngumu (kali) sana ili kuwasaidia.
Naam, kwa andiko hili tunajua kwamba mtu anaweza akaanza safari yake vizuri na kisha ak**aliza vibaya, ndiyo maana Mhubiri 7:8a naye anasema
"Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake…"
Ni huzuni kubwa sana kwa mtu aliyemjua Mungu halafu akarudi nyuma na kumaliza katika mwili. Mpendwa wangu jifunze kuchunga na kutunza mguu wako katika Bwana ukiwa makini wapi unakanyaga.
Ni vema tumruhusu Roho Mtakatifu atuongoze na kutufundisha njia itupasayo kuiendea, huku tukiwa watiifu na waaminifu kwake (Zaburi 32:8). Neno la Bwana na liongoze hatua zetu ndani yake kwa kuwa imeandikwa
"Neno la Bwana ni taa ya miguu yangu"
(Zaburi 119:105).
Asomaye na afahamu
Pastor Andrea Benedictor
TAG NIA NJEMA Bagamoyo
0713211635.