01/10/2026
═══════════════════
RHAPSODI YA UKWELI WA KILA SIKU
═══════════════════
UJUMBE WA IBADA ~ MCHUNGAJI CHRIS OYAKHILOME Dsc. Dsc. DD.
══════════════════
IJUMAA, TAREHE 2 OKTOBA 2026
═══════════════════
ALITULETA KWAKE MWENYEWE
═══════════════════
📖Mmeona yale niliyowatendea Wamisri, na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mabawa ya tai, na kuwaleta kwangu mwenyewe (Kutoka 19:4).
Mungu alipowakomboa wana wa Israeli kutoka Misri, kusudi Lake lilikuwa kubwa zaidi kuliko kuwaokoa kutoka katika dhuluma. Ukombozi ulikuwa mwanzo tu. Nia Yake kuu ilifunuliwa katika maneno Yake k**a yalivyoandikwa katika andiko letu la ufunguzi: Aliwachukua juu ya mabawa ya tai, na kuwaleta Kwake mwenyewe. Hakuwatoa tu kutoka Misri.
Hii inafunua moyo wa Mungu. Lengo Lake siku zote limekuwa ushirika na uhusiano na mwanadamu. Alitaka watu watakaokuwa Wake, watakaotembea na Yeye na kuishi wakifahamu upendo na kusudi Lake. Ndiyo maana aliendelea kusema katika mistari iliyofuata: "...nanyi mtakuwa hazina ya pekee kwangu kuliko watu wote; maana dunia yote ni yangu; nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu..." (Kutoka 19:5-6). Walichaguliwa, wakatengwa, na kuwekwa wakfu kwa ajili Yake.
Yale ambayo Mungu aliyaonyesha kimbele kupitia Israeli yamepata utimilifu wake mkuu zaidi katika Kristo na Kanisa! Kupitia kifo, kuzikwa, na kufufuka kwa Yesu Kristo, umeingizwa katika muungano usiotenganishika na Mungu. Hujatenganishwa na Yeye, ukijaribu kutafuta njia ya kuingia katika uwepo Wake. Umeunganishwa na Bwana na kufanywa roho moja na Yeye: "Lakini yeye aliyeunganishwa na Bwana ni roho moja" (1 Wakorintho 6:17). Mtume Petro alirudia maneno yale yale ambayo Mungu alimwambia Musa alipotangaza kwamba wewe ni "...kizazi kiteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu..." (1 Petro 2:9). Kwa Israeli, jambo hili lilitegemea utii wao kwa Sheria, lakini kwetu sisi, ni ahadi iliyotimizwa, urithi wetu ndani ya Kristo.
Sisi ni hazina Yake ya pekee, tukiwa na muungano usioweza kutenganishwa na Yeye. Wewe si mtu wa kawaida anayehangaika na maisha peke yake. Uko ndani Yake, na Yeye yuko ndani yako. Alikutoa gizani na kukuingiza katika nuru Yake ya ajabu, katika maisha ya utukufu, ubora na kusudi la kiungu. Unategemezwa na nguvu Zake, unaongozwa na hekima Yake na kuimarishwa katika baraka Zake. Tembea kwa ujasiri, heshima na kusudi la mtu aliye wa Kristo, Mfalme, na ambaye ametengwa kwa ajili ya utukufu Wake. Haleluya!
SALA
Baba Mpendwa, nakushukuru kwa kunileta katika muungano usioweza kutenganishwa nawe. Nafurahi kujua kwamba mimi ni hazina Yako ya pekee, mtakatifu na niliyetakaswa. Ninatembea nikiwa na ufahamu wa umoja wangu nawe, na ninatimiza kusudi Lako kwa ajili ya maisha yangu kwa ujasiri na furaha, katika Jina la Yesu. Amina.
📚MASOMO YA ZIADA:
Kutoka 19:4-6; 1 Petro 2:9-10; 1 Wakorintho 6:17
MPANGO WA KUSOMA BIBLIA WA MWAKA 1
Wafilipi 1:1-30 & Isaya 33-34
MPANGO WA KUSOMA BIBLIA WA MIAKA 2
Tito 2:1-15 & Yeremia 50